Maisha: LHRC kuwanoa kisheria wasichana Shinyanga kupambana na maambukizi ya VVU - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


18 Sept 2017

Maisha: LHRC kuwanoa kisheria wasichana Shinyanga kupambana na maambukizi ya VVU



Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga Bw. Charles Maugila akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa Dreams Innovation Challenge wilayani humo.

Baadhi ya wasichana na wanawake wadogo watakaofikiwa na mradi katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wilayani Kahama.



Na Mwandishi Wetu,

LHRC kuwanoa kisheria wasichana Shinyanga kupambana na maambukizi ya VVU

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la IDLO kimezindua mradi wa Kuwajengea Uwezo wa Kisheria Wasichana na Wanawake Wadogo mkoani Shinyanga ili Kuweza Kuiwajibisha Jamii Kutoa Huduma Bora za Afya ya UKIMWI.

Katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Septemba 14 katika manispaa ya Shinyanga na Septemba 15 katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, makundi lengwa ya mradi huo ikiwemo wasichana na wanawake wadogo, wazazi, viongozi wa serikali na Jamii kwa ujumla yameonyesha kuvutiwa na malengo na matokeo tarajiwa ya mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga wakati wa kuzindua mradi huo Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga Bw. Charles Maugila amesema ujio wa mradi huo katika Manispaa ya Shinyanga ni wa kufurahiwa kwani mkoa wa Shinyanga kwa ujumla unakabiliwa na changamoto kubwa ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI hususani kwa wasichana na wanawake wadogo. “Kumekuwa na miradi mingi inayolenga kukabiliana na ukatili wa kijinsia na UKIMWI lakini mradi huu ni wa kipekee kwa vile unalenga kuwajengea uwezo wa kisheria wasichana na wanawake wadogo ambao ndio wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI waweze kuwajibisha jamii kwa kudai huduma bora za afya ya UKIMWI” Alisema Maugila.

Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Bw. Anthony Ndanya ameitaka Jamii ya Kahama kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo ili kuweza kufikia malengo ya mradi huo na kupata matoke tarajiwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Bw. Ezekiel Massanja alisema “kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2016, ukatili wa kijinsia ukijumuisha ukatili wa majumbani, ukatili wa kingono, mimba za utotoni, ndoa za utotoni pamoja na vitendo vingine vya kikatili kwa watoto na wanawake vimezidi kuongezeka maradufu mbali na kuwepo kwa sheria zinazolinda kundi hilo. Moja ya matokeo ya changamoto za ukatili kwa wanawake ni kuambukizwa virusi vya UKIMWI”.

“Sambamba na ongezeko la vitendo vya kikatili, Jamii inakosa uwezo wa kuwawajibisha watekelezaji wa vitendo vya kikatili na kushindwa kukabilianan na madhara ya ukatili wa kijinsia kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria na namna ya kudai upatikanaji wa huduma bora za afya” – Aliongeza Massanja.

Mradi huu ni moja ya miradi mingi ya Dreams Innovation Challenge inayotekelezwa nchini. Mradi umejikita kuwajengea uwezo wasichana wa miaka 15 hadi 24 na jamii kwa ujumla juu ya masula ya kisheria, afya na ukatili wa kijinsia. Mradi unalenga kuwapa uwezo wasichana kuiwajibisha jamii pale haki zao za msingi zinapokosekana hasa kwenye masuala ya afya ya UKIMWI.

Lengo kuu la mradi ni kuimarisha uwezo wa jamii kuboresha huduma za afya ya UKIMWI kwa wasichana na wanawake wadogo kupitia mbinu ya uwezeshaji kisheria na uwajibikaji kijamii.

Mradi unalenga kufikia jumla ya wasichana 1000 wenye umri kati ya miaka 15 – 24. Wasichana 500 Shinyanga na 500 wilayani Kahama. Wanufaika wengine ni pamoja na wanaume ambao ni wapenzi wa wasichana hao, wazazi, watoto, vyombo vya sheria, wahudumu afya pamoja na jamii yote kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad