Utalii : WCS Yatoa Msaada kwa Uhifadhi wa Wanyamapori - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


6 Jul 2017

Utalii : WCS Yatoa Msaada kwa Uhifadhi wa Wanyamapori



Katibu mkuu (mwenye koti nyeusi) akikata utepe wa uzinduzi wa ofisi ya pori la piti kulia kwake ni kaimu mkurugenzi mkuu wa tawa bw.martin loibooki na kushoto nimeneja wa pori la rukwa/piti bw.ambrose mungo’ng’o .


Na Mwandishi wetu Songwe


Taasisi ya Kimataifa ya kijamii ya uhifadhi wa wanyamapori ya World Concervation Society- WCS imetoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni 936 kwa mapori ya akiba ya Lukwati- Piti ambazo zimetumika kujenga jengo la kisasa la ofisi, ununuzi wa magari matatu ya doria na kuendesha mafunzo ya askari wa wanyamapori wa mapori hayo yaliyoko mkoani Songwe.


Akiongea katika halfa ya kukabidhi miradi hiyo kwa serikali ya Tanzania, Mkurugenzi wa WCS Aaron Nicholaus amesema taaisisi hiyo inajivunia kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuendeleza shughuli za uhifadhi wa wanayamapori wakiwemo tembo ambao ni maliasili muhimu kitaifa na kimataifa ambapo shirika la misaada la watu wa Marekani USAID nalo ni mdau mkubwa katika ufadhili huo.

katibu mkuu akipokea magari 3 aina ya toyota l/cruiser pickup toka kwa mratibu wa mradi wa cws bw. Aaron nicholaus.


Bwana Nicholaus alisema msaada huo umetilia mkazo suala la mafuzo ambayo yatawaongezea askari ujuzi na weledi wa kukabiliana na majangili ambao wamekuwa wakiua tembo na wanyamapori wengine kwa maslahi yao binafsi na kusababisha hasara kwa serikali ambayo inawategemea wanyamapori kwa maendeleo ya jamii na taifa.


“Tunapofikiria uhifadhi, tuangalie pia masuala ya mapito ya wanyamapori kama tembo ambayo yamekuwa yakitoweka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu na hivyo kuathiri uhifadhi maana tembo huhitaji eneo kubwa kwa malisho” alisme abwana Nicholaus.


Taarifa ya miradi hiyo iliyotolewa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudance Milanzi ilieleza kuwa miradi hiyo ina thamani kubwa kwa uhifadhi wa mapori hayo yenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 6,119 ambayo yanapakana na Hifadhi ya taifa ya Ruaha na pori la akiba la Rungwa.

Katibu mkuu akiongea na baadhi ya kikosi cha askari waliyopata mafunzo ya kukabiliana na ujangili.


Meneja wa Mapori ya Lukwati Piti Bwana Alphonce Ambroce Mung’ong’o akitoa ufafanuzo na mchanganuo wa gharama za miradi hiyo alisema jengo la kisasa la ofisi limegharimu zaidi ya shilingi milioni 227, magari matatu kwaajili ya doria yana thamni ya dola 255,000 za kimarekani boti na mfumo wa radio call una thamani ya zaidi ya shilingi milioni 234.


Aidha Bwana Ambroce alisema wafadhili hao pia wamenunua boti mbili za doria ambazo zimegharimu zaidi ya shilingi milioni 134 ambazo zitatumika kuimarisha doria katika ziwa Rukwa ambalo ni miongoni mwa maeneo muhimu ya mapori hayo ya Lukwati Piti.


Kuhusu ujangili, Bwana Ambroce alisema katika kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2013 mpaka sasa zaidi ya tembo 23 wameuwawa kwa ujangili katika mapori hayo ingawa alisema kwa sasa baada ya mafunzo hayo mapori hayo yameimarisha doria na amewaonya majangili kuwa sasa serikali imejipanga kupambana nao kikamilifu.

Bw.martin loibooki (kaimu mkurugenzi mkuu-tawa) akitoa taarifa fupi ya mapori ya akiba rukwa/piti mbele ya katibu mkuu.


“Nawaonya majangili, sasa tumejipanga kupambana nao na kamwe hatuwezi kuwaacha waendelee kutamba humu na kumaliza rasilimali zetu kwa manufaa yao, hii haikubaliki na kamwe hatutawavumilia, tumepata mafunzo na vitendea kazi lazima tutashinda na kuwaacha wanyamapori watumike kwa shughuli za kitaifa na kwa maslahi ya watanzania walio wengi” alisisitiza Ambroce.


Akiongea baada ya kupokea misaada hiyo, Katibu Mkuu wizara ya maliasili na utalii Meja Jenerali Gaudance Milazi amewashukuru wadau wa uhifadhi ikiwemo WCS kwa kusaidia juhudi za kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania kwani mchango wao umeanza kuzaa matunda.


Meja Jenerali Gaudance Milanzi alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali za wanyamapori wengi sana ambao wakitunzwa na kutumika vizuri wana nafasi kubwa ya kuchangia kwa kiwango kikubwa kuliondoa taifa katika umasikini uliokithiri na hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa kaika pato la taifa na maendeleo ya nchi.

Baadhi ya kikosi cha askari kilichohudhuria mafunzo ya kukabiliana na ujangili (rapid response team).


“Kazi kubwa tuliyonayo ni kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa ipasavyo kwa manufaa ya vizazi vyote na kamwe asiwepo mtu mwenye uroho wa kutumia rasilimali hizi kwa manufaa yake binafsi” alisisitiza Meja Jenrali Gaudance Milanzi.


Alisema anatambua kabla ya kituo cha Lukwati Piti kuanza mwaka 2013 wavuvi walikuwa wamesheheni katika fukwe za ziwa Rukwa upande wa pori la akiba la Likwati, “Hivi sasa kambi hizo za wavuvi zilishaondolewa na fukwe hizo zimebaki kuwa mazalia mazuri ya mamba ya samaki na malisho ya wanyamapori hali inayoleta matumaini ya kuimarika kwa uhifadhi wa wanyamapori” alisema Meja jenerali Milanzi.


Meja jenerali Gudance Milanzi alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya wananchi wakorofi wajiepushe kufanya za binadamu ikiwemo uanzishaji wa makazi, kilimo, uvuvi, uchimbaji wa madini na uingizaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za uhifadhi.


“Sasa maeneo mengi ya hifadhi yanakumbwa na changamoto za ongezeko la shughuli za binadamu ikiwemo uingizaji wa mifug itambulike kwamba maeneo ya hifadi yametengwa kisheria kwa shughuli za uhifadhi na wanaofanya mchezo huo waache mara moja na sheria itaendelea kuchukua mkono wake kwa wafugaji na mifugo inayokamatwa” alionya.


Meja jenerali Gudance Milanzi alisema serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha masuala ya ujangili yanadhibitiwa ikiwa ni kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa watumishi wake, kununua vitendea kazi ikiwemo magari ya doria.


Alisema juhudi hizo ni pamoja na kugeuza mfumo wa kiutendaji kutoka ule kiraia na kwenda mfumo wa jeshi usu na akaipongeza Mamlaka ya wanyamapori TAWA kwa kutoa kipaumbele katika mafunzo kuelekea mfumo wa jeshi usu ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja TAWA imetoa mafunzo kwa watumishi 236.


Mapema katika taarifa yake kwenye hafla ya kupokea miradi hiyo kutoka WCS iliyofanyika kwenye ofisi za pori hilo zilizoko Lupatingatinga wilayani Songwe, kaimu Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya Wanyamapori TAWA Martini Loibooki alisema ufadhi wa WCS katika mapori hayo ni matokeo ya ushirikiano unaoendelea kati ya TAWA na wadau wa uhifadhi.


Bwana Loibooki alisema WCS imekuwa mfadhili wa kwanza kuingia kufadhili mapori ya Lukwati Piti ambayo hko nyuma yalikuwa na changamoto nyingi ikiwemo ujangili na uwindaji haramu lakini kutokana na ufadhili huo sasa uhifadhi umeanza kuimarika.


Alisema amepokea changamoto za kituo cha Lukwati Piti lakini Mamlaka imeweka mipango ya muda mfupi na muda mrefu kuhakikisha changamoto hizo zinaendelea kupungua kadri upatikanaji wa fedha na kwamba mazingira ya kazi yameanza kuwa bora na vitendea kazi vimeongezeka na kuwa bora kuliko miaka ya nyuma.


Alieleza kuwa mapori ya Lukwati Piti yana umuhimu mkubwa na yamekuwa chanco muhimu cha mapato ya serikali kutokana na uwindaji wa kitalii ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mapori hayo yameliingizia taifa mapato ya zaidi ya shilingi bilioni mbili na milioni mia tisa.


Bwana Loibooki alisema fedha hizo zinazotokana na uwindaji wa kitalii ni nyingi na zimeisaidia serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye mikoa mbalimbali nchini ikiwemo afya , elimu na ujenzi wa miradi ya kijamii.




Kaimu mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya wanyamapori tanzania tawa, martin loibooki amesema tawa inatambua wajibu wake na malengo ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ya kusaidia kuchochea maendeleo ya jamii na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya wanyamapori na ameishukuru wcs kwa kuwa mfadhili wa kwanza kufadhili shughuli za uhifadhi katika mapori ya lukwati- piti.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad