Michezo /Riadha : Health Nusu Marathon Kufanyika Dar Aprili 26 - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


21 Apr 2017

Michezo /Riadha : Health Nusu Marathon Kufanyika Dar Aprili 26



Katibu Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Bi. Rebecca John (katikati) akisisitiza jambo kwa wandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea maandalizi ya mbio za heart marathon na upimaji wa afya yenye lengo la kuisaidia serikali kupunguza magonjwa yasiyoambukizika mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Riadha Tanzania Bi. Ombeni Zavara na kulia ni Katibu Mkuu Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Lucas Nkungu.
Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Riadha Tanzania Bi. Ombeni Zavara akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya ya mbio za heart marathon na upimaji wa afya yenye lengo la kuisaidia serikali kupunguza magonjwa yasiyoambukizika mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Bi. Rebecca John.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Dkt. Omary Chillo (kulia) akifafanua jambo kwa wandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea maandalizi ya mbio za heart marathon na upimaji wa afya yenye lengo la kuisaidia serikali kupunguza magonjwa yasiyoambukizika mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Katibu Mkuu Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Lucas Nkungu na kushoto ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Health Summit Bi. Rebecca John.

……………..

Na Nuru Juma-Maelezo

Taasisi ya Tanzania Health Summit yaandaa mbio za nusu Marathon na Upimaji wa afya kwa lengo la kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza magonjwa yasioambukiza, mbio hizo zinazotarajia kufanyika Aprili 26 katika barabara ya Kaole iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Rebecca John wakati alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha jamii kushiriki.

“Kamati ya maandalizi ya ya mbio za Heart Marathon inapenda kuwa taarifu wadau wote wa sekta ya afya hapa nchini na jamii kwa ujumla juu ya mbio za Heart Marathon na upimaji wa afya ili kuungana na serikali katika juhudi za kupunguza magonjwa yasiyoambukiza” alisema Rebecca.

Aliongeza kuwa kwa mwaka huu mbio hizi zitashirikisha washiriki zaidi ya elfu mbili kutoka rika mbalimbali wakiwemo vijana, watoto, wazee, makundi ya watu wenye ulemavu na watu wenye magonjwa yasiyoambukiza.

Pia washiriki watapata nafasi ya kupima afya magonjwa mbalimbali kama vile shinikizo la damu ,wingi wa sukari katika damu, kiasi cha mafuta mwilini, uchunguzi wa uvimbe katika matiti na kupata ushauri wa wataalam kuhusiana na vyakula bora, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Aidha Bi. Rebecca aliongeza kuwa washiriki watakimbia umbali tofauti, kwani kuna mbio ndefu za kilometa 21.1 kwa ajili ya wakimbiaji wazoefu, kilometa 10 kwa wakimbiaji wa kati, kilometa 5 kwa wakimbiaji wa kawaida, kifamilia na kampuni na mbio za watoto chini ya miaka 12 ni meta 700 na zawadi itatolewa kwa mshindi wa kilometa 21.1 pekee kwa kiasi cha shilingi laki tano.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania Health Summit Dr.Omary Chillo alisema kuwa washiriki watatakiwa kutoa kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kununua flana pamoja na kifaaa maalum cha kuhesabia muda wakati wa kukimbia ila maji ya kutosha yatatolewa bure kwa ajili ya wakimbiaji.

Aliongeza kuwa wameimarisha ulinzi kwa kushirikiana na jeshi la polisi na ili kulinda usalama kwa washiriki na wananchi watakaokuwepo katika mashindano hayo.

“wananchi wasiwe na wasiwasi wa usalama kwani tutashirikiana na jeshi la polisi ili kuimarisha usalama na tumeweza kupata baraka nyingi kutoka kwao kwa kuweza kushirikiana nao” aliongeza Chillo.

Pia Katibu msaidizi wa Chama cha Riadha nchini Bi Ombeni Zavala alisema anashukuru wananchi wanavyoweza kujitokeza katika mashindano hayo na pia anawaomba wananchi hasa vijana waendelee kujitokeza kwa wingi kwani wanaweza kupata nafasi ya kuunda timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17.

Naye Sajenti Isaya Mlokozi kutoka kanda ya usalama barabarani alisema jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani litahusika vizuri katika sehem inayowahusu kuhakikisha watu wanafanya zoezi hilo kwa hali ya usalama na litajumuika na wananchi popote pale watakapokuwa wanakwenda.

Mashindano haya mwaka jana yalifanyika katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam lakini kutokana na kuongezeka kwa watu mwaka huu yatafanyikia barabara ya kaole yenye kauli mbiu ‘piga hatua moja mbele ya magonjwa sugu’

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad