Kimataifa : Dakika Tatu za Dhahabu za Rais Samia Urusi Zafungua Milango ya Shilingi Trilioni 5 - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Sunday, 7 June 2026

Kimataifa : Dakika Tatu za Dhahabu za Rais Samia Urusi Zafungua Milango ya Shilingi Trilioni 5

 


Na Mwandishi Wetu, TBN, Dar es salaam


Ziara ya kihistoria ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imeendelea kuzaa matunda makubwa baada ya Serikali kutangaza kuwa kampuni kubwa za nchi hiyo zimeonesha nia thabiti ya kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni mbili (sawa na Shilingi za Kitanzania trilioni tano) ndani ya miaka mitatu ijayo. 

Uwekezaji huu mkubwa unalenga kimkakati sekta tano kuu za kipaumbele, huku ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na ushawishi wa kipekee wa Rais Samia kiuchumi.

Akitolea ufafanuzi mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi John Ulanga, alifichua siri ya mafanikio hayo kuwa ni "dakika tatu za dhahabu" alizopewa Rais Samia kuzungumza katika Jukwaa la Uchumi la Kimataifa la Petersburg nchini Urusi. 

Kupitia ubunifu na maono yake makubwa, Rais alitumia muda huo mfupi kwa umahiri mkubwa kutangaza fursa za Tanzania, hatua iliyoziteka akili za miamba ya biashara nchini Urusi na kuamsha hamu kubwa ya kuwekeza nchini.


Miamba ya Nishati na Madini Kuja kwa Kasi

Katika sekta ya madini na nishati, Urusi tayari imeweka mguu wake nchini kupitia Shirika lake la Nishati ya Atomiki la Serikali (ROSATOM), ambalo limewekeza Dola bilioni 1.2 katika mradi wa kimkakati wa madini ya Urani, Nickel na madini mengine. Kasi hii inatarajiwa kuongezeka kufuatia ziara hiyo, kwani kampuni nyingi zaidi zilizotembelea banda la Tanzania zimeonesha nia ya kuja kuwekeza.

Sambamba na hilo, kampuni kubwa ya nishati duniani, Gazprom, inayomiliki soko kubwa la gesi asilia Ulaya Magharibi, imeingia kwenye mazungumzo na Tanzania ikieleza nia yake thabiti ya kushirikiana na kuwekeza katika sekta ya gesi nchini.


Mapinduzi ya Chanjo, Kilimo cha Kisasa na Tehama

Sekta ya afya na dawa nayo inatarajiwa kushuhudia mapinduzi makubwa. Kampuni za Urusi zilizotangulia kuwekeza nchini katika uzalishaji wa chanjo zimebainisha kuwa, ndani ya miaka mitano ijayo, zikishirikiana na makampuni mengine ya Urusi, zitakuwa na uwezo wa kuzalisha chanjo milioni 20 za magonjwa mbalimbali nchini Tanzania.

Kwenye kilimo na uongezaji thamani, makubaliano yamejikita katika kilimo endelevu kinachotunza mazingira na ununuzi wa bidhaa za Tanzania kama kahawa, korosho na chai kwa ajili ya soko la Urusi. Tayari wafanyabiashara zaidi ya 50 wa Kitanzania waliokuwa Urusi wameingia makubaliano ya kuleta mbolea, vinywaji vikali, na kuuza mazao yetu huko. Katika Tehama, taasisi za sayansi za Urusi ziko tayari kuja nchini kukuza uchumi wa kidijiti kwa kufundisha teknolojia hii kuanzia shuleni hadi vyuoni.

Angani Kufunguka: ATCL Kuanza Safari za Moja kwa Moja Moscow

Kama kilele cha mafanikio ya ziara hiyo, sekta ya utalii inatarajiwa kulipuka kwa mafanikio kufuatia tangazo la kihistoria kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) litaanza safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Moscow ifikapo Julai 2, mwaka huu.

"Tuliona mtiririko mkubwa wa kampuni za waongoza utalii kutoka Urusi wakivutiwa na tangazo hili. Moja ya vitu vinavyovutia watalii ni upatikanaji wa usafiri wa uhakika, wa moja kwa moja na rahisi zaidi," alisisitiza Balozi Ulanga.

Hatua hii ya ATCL si tu kwamba inarahisisha usafiri, bali inafungua njia ya moja kwa moja kwa maelfu ya watalii na wawekezaji kutoka Urusi kumiminika nchini, ikithibitisha nguvu ya diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

No comments:

Post a Comment