Na Beda Msimbe,TBN, St Peterburg, Urusi
Tanzania inatarajia kuwasha kinu chake cha kwanza kabisa cha nishati ya nyuklia ifikapo mwaka 2029, hatua itakayoliondoa taifa katika utegemezi wa nishati ya mazoea na kuingia kwenye ukurasa mpya wa nishati ya uhakika kwa ajili ya mapinduzi ya viwanda na kiuchumi.
Hayo yamebainishwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na waandishi wa habari waliombatana naye katika ziara ya kikazi nchini Urusi.
Rais Samia alisisitiza kuwa azma ya serikali ni kuona kuwa kabla ya mwaka 2029, kinu hicho kiwe kimeanza shughuli zake rasmi, huku nchi ikidhamiria kutumia nishati hiyo inayotokana na madini ya urani (uranium) yaliyopo nchini.
Akijibu swali kuhusu hitaji la kwanza katika teknolojia ya nyukilia Rais Samia alisema taifa linahitaji sana uzoefu wao (Urusi), katika nyanja zote zinazohusu teknolojia ya nyukilia ikiwa ni kujipanga kwa taifa kutumia umeme unaozalishwa na urani.
Nishati ya nyuklia inatazamwa kama nguzo kuu ya "nishati ya uhakika wa maendeleo" (reliable energy for development). Tofauti na vyanzo vya maji vinavyotegemea mabadiliko ya tabianchi au mafuta yanayoyumba bei sokoni, nyuklia inatoa umeme thabiti (baseload power) wa mfululizo unaohitajika kuendesha viwanda vizito, mifumo ya usafirishaji kama SGR, na miji ya kisasa. Huu ndio msingi wa nishati endelevu inayochochea maendeleo ya haraka bila kukwama.
Katika mazungumzo yaliyofanywa tayari Kampuni ya Tanesco imeingia makubaliano ya kutrunza faragha ya mazungumzo na kampuni ya Kirusi ya Rostam ambayo imesema kwamba iko tayari kuwezesha watanzania kuwa na umeme wa kuitosha na uhakika.
Katika kufanikisha azma hiyo ya kuwa na nishati ya nyukilia kwa mujibu wa makubaliano ya kimatraifa martumizi ya amani, Rais Samia alieleza kuwa kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni kujenga uwezo wa ndani (local capacity) kupitia elimu.
Alibainisha kuwa tayari kuna kundi la Watanzania wanaosomeshwa uhandisi wa nyuklia nchini Urusi chini ya udhamini wa kampuni ya Mantra Tanzania, lengo likiwa ni kuwa na wataalamu wazawa watakaofahamu mifumo yote na kuweza kuendesha mitambo hiyo hata baada ya wataalamu wa kigeni kuondoka.
Mbali na nishati, makubaliano hayo mapya yanakusudia pia kufufua miradi ya kiteknolojia iliyokuwa imesimama. Rais aligusia azma ya kufufua ushirikiano wa kinyuklia katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), mradi ambao huko nyuma ulisuasua kutokana na changamoto za washirika wa mwanzo, lakini sasa Urusi ipo tayari kuingia kati na kuusukuma mbele kwa matumizi ya amani ya nyuklia.


No comments:
Post a Comment