Kimataifa : Hotuba ya Rais Samia Urusi ni Ushindi wa Kiuchumi, Kijamii na Kidiplomasia - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Sunday, 7 June 2026

Kimataifa : Hotuba ya Rais Samia Urusi ni Ushindi wa Kiuchumi, Kijamii na Kidiplomasia



Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Urusi

IJUMAA, Juni 5, 2026, ilikuwa siku ya kihistoria na ya kipekee wakati Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akizungumza mbele ya viongozi wa dunia katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (St. Petersburg International Economic Forum) na kuwasilisha hoja nzito zenye mashiko, akibeba sauti ya Watanzania wote huku akiweka wazi fursa zinazopatikana Tanzania pamoja na mwelekeo mpya wa nchi katika kujenga uchumi wa kisasa.

Jukwaa hilo lilikuwa sehemu muhimu ya ziara ya Rais Samia ambayo haikuwa tu ya kiitifaki, bali pia ya kufungua milango ya fursa za kiuchumi na kijamii.

Jinsi Rais Samia alivyopokewa na kukirimiwa nchini Urusi katika shughuli zote zilizomhusu, ilionesha taswira ya urafiki wa dhati na uelewano mkubwa kati yake na mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin. Ziara hiyo ilifufua historia ya ushirikiano wa mataifa hayo mawili na kuweka wazi haja ya sasa ya kusaidiana katika kuleta ukombozi wa kiuchumi na ustawi wa jamii baada ya ukombozi wa kisiasa.

Akiwa katika jukwaa hilo la kiuchumi, hotuba ya Rais Samia iliwafanya washiriki wengi kutafakari kwa kina kutokana na hoja zake zilizojikita katika uchambuzi wa masuala ya dunia na umuhimu wa mabadiliko ya kimfumo katika uchumi wa kimataifa.

Rais Samia alitoa hoja yenye kuchokoza fikra aliposema kuwa ifikapo mwaka 2050, mtu mmoja kati ya wanne duniani atakuwa Mwafrika. Takwimu hiyo iliambatana na swali lenye uzito mkubwa: “Je, Afrika itastawi na kukua kwa masharti ya nani, na kwa modeli ipi ya uchumi?”

Swali hilo lilikuwa na mantiki kubwa katika kipindi ambacho siasa za kijiografia zimeendelea kuyumbisha ushirikiano wa kawaida wa kimataifa na kujaza mazingira ya masharti, ushindani na udhibiti wa kiuchumi unaozikandamiza nchi maskini.

Katika msingi huo wa kimantiki, Rais Samia alikuwa akiitaka dunia isiisitiri Afrika wala kuipangia mustakabali wake, bali itambue ukweli na kuiacha Afrika ijiamulie mambo yake yenyewe.

Mathalani, Afrika kwa sasa ina Ajenda 2063 pamoja na soko la pamoja la AfCFTA, lakini bado kuna mataifa yanayoendelea kuingilia masuala ya bara hilo na kuwagawa Waafrika ili waendelee kuonekana wanahitaji msaada wa kudumu katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Rais Vladimir Putin aliunga mkono hoja hiyo, jambo lililoibua miguno ya ridhaa na vigelegele ukumbini. Kwa hakika, yapo mambo mengi ambayo Waafrika wanaweza kuyafanya wenyewe kwa manufaa yao na ya dunia kwa ujumla.

Mambo yaliyoguswa

Katika hotuba yake na ziara hiyo ya Urusi, Rais Samia aligusa masuala mengi muhimu. Hapa tunaweza kuangazia maeneo makubwa yaliyobebwa na ziara hiyo pamoja na namna makubaliano mbalimbali yalivyohitimishwa kwa mafanikio makubwa kwa Tanzania.

Ikumbukwe kuwa ziara ya Rais Samia, ambayo pia aliambatana na wafanyabiashara wa Tanzania, imeikumbusha dunia kuhusu mizizi imara ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi. Mahusiano hayo yana historia ndefu tangu miaka ya mwanzo ya uhuru, ambapo siku mbili tu baada ya Tanganyika kupata uhuru, Urusi ilituma salamu za pongezi; hali iliyojirudia pia wakati wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Mbele ya wawekezaji, Rais Samia alibainisha kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya takribani asilimia sita, hali inayoiweka nchi miongoni mwa uchumi unaokua kwa kasi zaidi barani Afrika.

Aidha, alitangaza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kumfikisha kila Mtanzania kwenye kipato cha wastani cha dola za Marekani 7,000 huku akielezea kwa kina fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara zilizopo nchini Tanzania.

Hotuba hiyo iliyopigiwa makofi mara kwa mara iliwavutia wawekezaji wengi wa Kirusi, ambapo sekta binafsi ya Urusi ilikiri kuwa Tanzania ni soko salama lenye utulivu wa kisiasa unaowezesha ukuaji wa mitaji na biashara.

Mbali na hayo, Rais Samia alieleza kuhusu mapinduzi makubwa ya miundombinu yanayoendelea nchini, hususan katika sekta ya reli na bandari. Katika mikutano ya pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania na Urusi, alifafanua kwa kina kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na manufaa yake kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.

Pia alieleza mpango wa miaka mitano wa kuipanua reli hiyo kuanzia mwaka 2026 hadi 2031 kuelekea Musoma na kuunganisha ukanda wa kusini kupitia Malawi hadi Msumbiji. Urusi, ikiwa na uzoefu mkubwa katika teknolojia ya reli na usafirishaji, ilionesha nia ya kutoa utaalamu wa kihandisi pamoja na mitambo ya kusaidia kuharakisha ujenzi wa reli hizo za kikanda.

Suala la maboresho ya mazingira ya uwekezaji na mfumo wa usajili wa saa 24 lilizua msisimko mkubwa miongoni mwa washiriki. Rais Samia alieleza kuwa uwekezaji umeongezeka kutoka dola bilioni tatu mwaka 2021 hadi dola bilioni 12 mwaka 2025 kutokana na maboresho ya mifumo ya uwekezaji, ikiwemo usajili wa kampuni unaokamilika ndani ya saa 24.

Kutokana na mafanikio hayo, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na taasisi za uwekezaji za Urusi zilisaini mikataba ya ushirikiano. Hatua hiyo ilipokelewa kwa furaha kubwa, ikionesha namna Tanzania ilivyojidhatiti kupunguza urasimu katika uwekezaji.

Aidha, miradi ya Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo pamoja na Bandari ya Kimataifa ya Mizigo ya Mangapwani Zanzibar ilipewa kipaumbele na makampuni makubwa ya Urusi yanayojihusisha na usafirishaji wa baharini. Makampuni hayo yalikubali kutuma timu za wataalamu nchini Tanzania kufanya upembuzi yakinifu wa namna ya kuwekeza katika miradi hiyo.

Katika sekta ya madini, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi. Tanzania ina utajiri mkubwa wa dhahabu, uranium, nickel, graphite, helium pamoja na madini adimu.

“Hatutaki tena kuuza malighafi pekee; tunataka viwanda vya usindikaji hapa nchini,” alisema Rais Samia.

Urusi, ambayo ni miongoni mwa mataifa yenye nguvu katika sekta ya madini, ilionesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika kujenga viwanda vya uchakataji na kuongeza thamani ya madini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Katika ziara hiyo, Rais Samia alidhihirisha wazi namna Tanzania ilivyo tayari kwa biashara, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa unaolenga kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wake.

Wakati Rais Samia akihitimisha hotuba yake katika jukwaa la St. Petersburg kwa kutoa shukrani za dhati kwa Rais Vladimir Putin kwa ukarimu wake, viongozi hao wawili walionesha tabasamu la furaha, ishara iliyotafsiriwa kama mwanzo mpya wa ushirikiano wa dhahabu kati ya Tanzania na Urusi.

No comments:

Post a Comment