Nishati : Gesi Asilia Yashusha Gharama za Umeme - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


8 Feb 2017

Nishati : Gesi Asilia Yashusha Gharama za Umeme



Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.


Ugunduzi wa gesi asilia nchini umepelekea kushuka kwa gharama za umeme kwa asilimia 33.26 kwa mwaka 2014 hadi 2016.


Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani ameyasema hayo leo Bungeni, Mjiji Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge viti Maalum Maida Hamad Abdallah kuhusu faida zilizopatikana tangu kugundulika kwa gesi asilia.


“Faida kubwa iliyopatikana kutokana na ugunduzi na matumizi ya gesi asilia nchini ni uzalishaji wa umeme wa bei nafuu kwa kutumia Gesi Asilia ikilinganishwa na mafuta. Uzalishaji umeme kwa kutumia Gesi Asilia umeongezeka kutoka uniti 2,714.25 milioni kwa mwaka 2014 hadi uniti 4,196.4 milioni mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 54.61,” alifafanua Dkt. Kalemani.


Aliendelea kwa kusema kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa Gesi Asilia umepelekea kushuka kwa bei ya umeme kutoka wastani wa shilingi 188.56 kwa uniti mwaka 2014 hadi wastani wa shilingi 125.85 kwa uniti mwaka 2016.


Akitolea ufafanuzi zaidi juu ya faida zinazopatikana kutokana na matumizi ya Gesi Asilia, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa maeneo ya Mikocheni, Jijini Dar es Salaam zikiwemo nyumba za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wanatumia Gesi Asilia ambapo gharama wanayoitumia kwa mwezi haizidi shilingi elfu 25,000, na wanatumia kwa kupikia aina zote za vyakula hata vile vinavyotumia muda mrefu kuiva kama vile maharage na makongoro.


Aliendelea kwa kusema kuwa, mpaka sasa jumla ya viwanda 37 vinatumia nishati inayotokana na Gesi Asilia, ambayo gharama yake ni nafuu ukilinganisha na gharama ya nishati nyingine.Aidha, amesema kuwa Wizara yake imepata ufadhili wa Dola Mil. 150 kutoka Afrikan Development Bank kwa ajili ya kusambaza gesi katika mikoa Dar es Salaam, Mtwara na Lindi.


Prof. Muhongo amesema kuwa usambazaji huo utakapoanza na kufika maeneo ya Kinyerezi, Jijini Dar es Salaam yatafungwa mabomba mengine kwa ajili ya kupeleka gesi katika mikoa mingine kama vile Morogoro, Mbeya na Iringa.Aidha amesema gesi ambazo zinatumika kwa sasa ni gesi salama ambazo hazilipuki ukilinganisha na gesi za miaka ya nyuma.


Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lilianza utafiti wa masuala ya mafuta na Gesi Asilia nchini mwaka 1950, ikihusisha utafiti katika maeneo ya bahari ya kina kirefu, maziwa na nchi kavu. Gesi Asilia iliyogundulika katika maeneo ya bahari ya kina kirefu ni futi za ujazo trilioni 47.08 na katika nchi kavu ni futi za ujazo trilioni 10.17 hivyo kuwa na jumla ya futi za ujazo trilioni 57.25 za Gesi Asilia inayojulika kama “sweet gas” yaani gesi yenye kiwango kidogo sana cha salfa (sulphur).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad