Uchumi : Serikali Kutumbua Wahujumu wa TAZARA - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


28 Jan 2017

Uchumi : Serikali Kutumbua Wahujumu wa TAZARA



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akimsikiliza mmoja wa wataalam wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), akimweleza namna wanavyosimamia mafuta yanayotumika kwenye treni za Mamlaka hiyo, alipowatembelea jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Karakana ya Dar es Salaaam ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Eng. Timothy Kayani, akimwonyesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa vipuri vya treni vilivyotengenezwa katika karakana hiyo jijini Dar es Salaam, alipotembelea karakana ya Mamlaka hiyo kuona utendaji wake.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akiangalia behewa la treni lililofanyiwa ukarabati na kukamilika katika karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), alipotembelea karakana hiyo jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Karakana ya Reli Dar es Salaaam ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Eng. Timothy Kayani, akifafanua namna behewa la treni linavyoanza kufanyiwa ukarabati kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) katika karakana hiyo, wakati Waziri huyo alipotembelea kuona utendaji wake. Wa pili kushoto ni Meneja wa TAZARA Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Fuad Abdalla.

Mtaalam wa mifumo ya Tehama wa Kampuni ya Qmax Bi. Jenirose Jabakila akimweleza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, namnamfumo walioutengeneza wa kufatilia treni inapokuwa njiani unavyofanya kazi, wakati alipotembea Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambokwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), alipotembelea mamlaka hiyo kuona utendaji kazi.

Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


Na Chalila Chibuda


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali haitamvumilia mtumishi yoyote ambaye ataendelea kuisababishia hasara Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kwa kuendelea kuihujumu na kusababisha mamlaka kujiendesha kwa hasara.


Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo wakati alipotembelea Tazara, kuangalia utendaji ambapo amebaini matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na Serikali na kuahidi kuchukua hatua stahiki.


“Ninafahamu kuna watu 10 hapa ambao wao ni chanzo kikubwa cha matumizi mabaya ya fedha na miongoni mwao wapo Watanzania na Wazambia, nawahakikishia kuwa kila atakayetumia vibaya fedha zinazotolewa na Serikali hatutamvumilia kwenye Serikali hii’, amesema Prof. Mbarawa.


Profesa Mbarawa amesema kumekuwa na idadi kubwa ya watumishi ambao hawana tija na kuagiza menejimenti ifanye uhakiki na kubaini mahitaji halisi ya Watumishi na watakaobainika kuzidi wahamishiwe ofisi ya tazara Mkoa waDar es Salaam.


Aidha Prof. Mbarawa ameuagiza uongozi wa Tazara Makao Makuu kuacha mara moja kutumia mtandao ya kampuni binafsi kutuma taarifa za Ofisi na kuagiza kuanza kutumia mtandao wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) mara moja.


‘Nikirudi tena hapa sitaki kuona mnatumia mitandao wa Kampuni binafsi kutuma taarifa za kiofisi ninawaomba muhakikishe mnatumia mtandao wa TTCL’ amesisitiza Prof. Mbarawa.


Kwa upande Meneja wa TAZARA Mkoa wa Tanzania, Bw. Fuad Abdalla amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa mkoa umejipanga vizuri kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa na Mamlaka inajiendesha kibiashara.


‘Kama mkoa tumekuja na mikakati mizuri ya kutumia mifumo ya Tehama kama njia ya udhibiti wa mapato, kama ulivyona hivi sasa tunakamilisha mfumo wa Tehama tunaoutumia kufatilia treni kila inapoondoka kwenye Stesheni ya Makao Makuu Dar es Salaam na mfumo huu ukikamilika tutawaashawishi na wenzetu wa Zambia kutumia mfumo huu ili tuweze kudhibiti upotevu wa mapato’ Amesisitiza Bw. Fuad Abdalla.

Bw. Fuad ameongeza kuwa pamoja na mifumo mipya ya Tehama Tazara inaendeleza kwa kasi ukarabati wa mabehewa ya abiria na mizigo ili kuongeza tija na kuiwezesha Mamlaka kupata faida.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad