WAZIRI MKUU Kassim Mjaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 15 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana zaidi 2,500 ili kuwajengea uwezo waweze kushiriki kama nguvu kazi kwenye viwanda vinavyotarajiwa kujengwa nchini.
Alitoa kauli hiyo jana usiku (Alhamis, Desemba 8, 2016) kwenye sherehe za utoaji wa tuzo ya muajiri bora wa mwaka 2016, zilizofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Tuzo hizo zimeandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kujielekeza katika kutoa mafunzo kwenye sekta za kipaumbele kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo kama kilimo biashara, mafuta, gesi, utalii, usafirishaji, ushonaji na bidhaa za ngozi.
Alisema jitihada zinaendelea kwenye maeneo mengine ili waajiri wawe na wigo mpana wa kuwapata wafanyakazi wenye stadi stahiki kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wao kuwa nguvu kazi yenye ujuzi na umahiri mkubwa kwa lengo la kuongeza tija.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia changamoto inayolalamikiwa na waajiri ya uwepo wa tozo mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka tofauti za Serikali kwa huduma ileile kuwa wanaitambua na tayari mchakato wa kuainisha sheria zote zinazoonekana kukwamisha uwekezaji pamoja na mazingira ya biashara nchini.
“Lengo letu ni kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili yaweze kuvutia zaidi na mchakato huu unashughulikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Tunaomba mvumilie na mshirikiane nasi katika kuendelea kuziainisha sheria zinazokwaza biashara ili tuweze kuzijumuisha kwenye mapitio hayo,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwashauri waajiri wote nchini waendelee kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi. Pia aliwasihi wafanyakazi wote kufanyakazi kwa bidii na uaminifu mkubwa ili waajiri waweze kupata faida, hivyo kuwaboreshea maslahi yao.
Alisema “tunaposema Hapa Kazi Tu, tunamaanisha kazi kwenye sekta zote za uzalishaji na utoaji wa huduma bora nchini, iwe sekta ya binafsi au kwenye utumishi wa umma. Nawasihi ndugu zangu Watanzania, wekeni nadhiri kwamba katika mwaka 2017 mtafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuongeza tija na ufanisi mahala pa kazi,”.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama aliwaomba waajiri wawasaidie kuweka msukumo katika juhudi za kutoa mafunzo kwa ajili ya uzoefu na kuongeza ujuzi kwa kutoa nafasi kwa wahitimu kupata uzoefu kwenye maeneo yao ya kazi.
Hata hivyo Mheshimiwa Jenista alisema anatambua umuhimu wa waajiri na wafanyakazi katika utekelezaji wa sera ya maendendeleo ya nchi hasa kwa kuongeza ajira kupitia sekta ya viwanda kwa asilimia 40 kufikia mwaka 2020, mafanikio ya mpango huo yanategemea mchango wa waajiri kutoka sekta binafsi.
Pia aliwapongeza ATE kwa kutambua umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu hasa kwa kutoa tuzo katika eneo la kuendeleza vipaji, ambapo aliwaomba tuzo ijayo waongeze kigezo cha kumpata mwajiri aliyetumia rasilimali zake kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi wake ambao ndio chanzo cha kuinua tija na ushindani kibiashara.
“Natambua kuwa ATE mnatoa mafunzo katika sheria za kazi na usimamizi wa rasilimali watu ambayo husaidia kupunguza migogoro mahali pa kazi na hivyo kujenga mazingira tulivu maeneo ya kazi. Naomba kutumia wasaa huu kuwakumbusha waajiri kuwawezesha wafanyakazi kwenda kuhudhuria mafunzo mbalimbali ili kuweza kukidhi ushindani katika mazingira ya biashara,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka alisema lengo la uaandaji wa tuzo hiyo ni kutambua wanachama wenye sera nzuri za usimamizi wa rasilimali watu katika taasisi na makampuni mbalimbali mwanachama hapa nchini.
Alisema kuwa tuzo hizo zinafuata mbinu za Kisayansi na kitaalamu ili kuangalia umuhimu wa Rasilimali watu katika makampuni ya Kibiashara makubwa na madogo na yale ya kati ili kuinua ujuzi wa wafanyakazi wanaofanya kazi kwa kujituma sehemu za kazi.
Dk. Mlimuka alisema kuwa tuzo hio pia ilijikita zaidi katika kuangalia maeneo muhimu ya rasilimali watu, uongozi, utawala, usimamizi wa Rasilimali watu, kusaidia jamii pamoja na kuwajibika katika jamii, ubora na uzalishaji.