Uchumi : Uanzishwaji Mahakama ya Mafisadi Kukomesha Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini. - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


3 Nov 2016

Uchumi : Uanzishwaji Mahakama ya Mafisadi Kukomesha Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini.


Na Eliphace Marwa - Maelezo

Ni mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani na kutekeleza kwa vitendo moja ya ahadi alizozitoa Mgombea Urais wakati ule, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuanzisha Mahakama ya Rushwa na Mafisadi.
 

Mahakama ambayo imeanza miezi michache iliyopita inaleta matumaini kwa watanzania hasa wanaipenda nchi yao wakiwa na uzalendo na fikira za kiutaifa. Katika ahadi za TANU, baadae CCM imetamkwa wazi kuwa Rushwa ni adui wa Haki, Sitapokea wala Kutoa Rushwa.

Rais John Pombe Magufuli anatekeleza kwa vitendo anachokiahidi. Leo naomba nizungumzie utekelezaji wa ahadi yake ya kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kushughulikia mafisadi na wahujumu uchumi wa nchi yetu.

Ni dhahiri kuwa Dkt. Magufuli anafuata nyayo za muasisi wa Taifa letu, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alithubutu kukemea na kuwaadhibu viongozi wote wala rushwa.

Mwalimu Nyerere alichukia sana rushwa na alichukua hatua kali sana kwawala rushwa wote bila kujali nyadhifa zao au uwezo wao wa kifedha kwani nakumbuka kuna waziri wake mmoja alihukumiwa kifungo na viboko baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa .

Watumishi wa umma, waliohusika na ufisadi walichukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufungwa jela na kufilisiwa mali zao na hiyo ilipunguza sana rushwa na ifisadi serikalini. Mwalimu aliamini kwamba mtu hawezi kupanda farasi wawili kwa wakati mmoja na alikuwa sahihi kabisa. Kitendo cha kuruhusu wafanyabiashara kuingia kwenye siasa, na viongozi kuruhusiwa kufanya biashara ndio chanzo cha wizi na ufisadi wa mali na fedha za umma.

Katika hotuba ya kufungua Bunge la 11 mjini Dodoma Novemba 20,2015, Rais  Magufuli jambo moja alilolisitiza na kulisemea kwa nguvu ni juu ya ahadi yake wakati wa kampeni ya mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

“Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia”, alisema Dkt. Magufuli.

Ni kweli kuwa wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo na hata yeye pia anachukia rushwa na ufisadi na wala hafurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini kwani vitendo hivyo vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo..

Rais Magufuli aliongeza kuwa Chama chake, Chama cha Mapinduzi, kimejengwa katika misingi ya kukataa rushwa na ufisadi na ndiyo maana moja ya Imani kuu za CCM ni ile isemayo, “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa” na hivyo Mtanzania mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na kigugumizi katika kuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na ufisadi.

Rais Magufuli alimnukuu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuwa aliwahi kuifananisha rushwa na ufisadi ‘Kama Adui Mkubwa wa Watu’.

Akiongea Bungeni Mei 1960, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo kuhusu rushwa, “Rushwa [na ufisadi] havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa Amani rushwa na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.”

Haya ni maneno makali ya mtu na kiongozi aliyeichukia na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya uongozi. Ni maneno yanayotukumbusha tu nini kinaweza kikatutokea kama taifa endapo tutaendekeza rushwa na ufisadi. Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri. Watanzania wamechoka kabisa, wamechoka sana, hawako tayari kuvumilia serikali inayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.

“Nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote na Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua majipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine, hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na mniunge mkono wakati natumbua majipu haya”, aliongeza Rais Magufuli.

Aidha, katika siku ya kilele cha Wiki ya Mwaka Mpya wa Mahakama Jijini Dar es Salaam mapema mwaka huu, Rais Magufuli alimtakia Jaji Mkuu, Othman Chande kutosubiri Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, badala yake mahakama hiyo ianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo.

Alisema kuchelewesha kuanza kwa mahakama hiyo kunatoa mwanya kwa mafisadi kuendelea kuangamiza nchi na kuifanya kuwa masikini wakati ina rasilimali za kutosha ambazo zinaweza kuiendesha nchi bila kutegemea fedha za wafadhili.

Rais Magufuli alisisitiza umuhimu wa uanzishwaji wa mahakama hiyo ambayo alitaka ifanye kazi ndani ya mahakama kuu kama zilivyo Mahakama za Ardhi na Biashara.

Akifunga maadhimisho hayo, Rais Magufuli alisema azma yake ni kuona nchi inakuwa na uchumi mzuri ambao utamnufaisha kila mtanzania na rasilimali zilizopo badala ya kumilikiwa na watu wachache.

Tamko la kuanza kazi kwa Mahakama hiyo lilitolewa bungeni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi yake.

“Kuhusu ahadi ya kuanzisha Mahakama Maalum ya Ufisadi napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi mwezi Julai 2016,” alisema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema pia Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki kwa kesi zitakazofikishwa kwenye mahakama hiyo.

Akizungumza Bungeni Majaliwa alisema katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa majengo ya mahakama na vitendea kazi katika ngazi zote, Rais Magufuli ametekeleza ahadi yake aliyoitoa Februari 4, mwaka huu ya kutoa fedha za maendeleo ya mahakama Sh. bilioni 12.3.

Alisema hatua hiyo imewezesha mahakama kuendelea na ukarabati na ujenzi wa mahakama katika ngazi mbalimbali pamoja na ununuzi wa vitendea kazi kwani Serikali imedhamiria kupunguza kero ya mlundikano wa mashauri mahakamani ili wananchi wapate haki kwa wakati.

Katika kufanikisha dhamira hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali imeimarisha  utendaji wa mhimili wa mahakama kwa kuongeza rasilimali watu na fedha.

“Serikali pia imeboresha na kuongeza ufanisi katika upelelezi na uendeshaji wa mashauri kwa kutenganisha jukumu la upelelezi na uendeshaji mashuari kwa majaji na mahakimu kujiwekea utaratibu wa kuwa na malengo ya idadi ya mashauri ambayo wanapaswa kuyasikiliza kila mwaka,” alisema Majaliwa.

Aidha Tarehe 24 Juni 2016 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho Mbalimbali, ambayo pamoja na mambo mengine, yamempa Jaji Mkuu mamlaka ya kuanzisha Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa muswada huo uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, adhabu kwa watakaokutwa na hatia zimeongezwa, huku mahakama hiyo ikiwekewa mazingira wezeshi ili iendeshe kesi hizo kwa haraka.

Muswada huo wa sheria ambao kwa sasa utakuwa ukisubiri Rais ausaini ili iwe sheria kamili, umekusudia kuanzisha divisheni hiyo ya mahakama, ambayo itakuwa na majaji wake na watumishi wake wanaojitegemea.

“Divisheni Maalumu ya Mahakama Kuu, itakuwa na majaji pamoja na watumishi wengine, ambao wanahusika moja kwa moja na kesi za rushwa na uhujumu uchumi tu, hatua hii itawezesha kesi za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kusikilizwa kwa urahisi, ufanisi na kwa haraka,” alisema Masaju wakati alipokuwa akisoma muswada huo kabla ya kupitishwa na Bunge.

Hatua hiyo ya kuwa na majaji maalumu na wafanyakazi wake, Masaju alisema imelenga kuondoa udhaifu uliojitokeza wakati wa kushughulikia kesi za rushwa na uhujumu uchumi, kwa kuwa majaji waliokuwa wakisikiliza mashauri hayo, walikuwa hao hao wanaosikiliza mashauri mengine ya jinai, madai, katiba na mengine yanayofunguliwa Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa Masaju, hali hiyo ilisababisha uendeshaji wa kesi za rushwa na uhujumu uchumi, kutokuwa na tofauti na uendeshaji na usikilizwaji wa kesi zingine.

Aidha Masaju aliongeza kuwaMazingira mengine wezeshi yanayotengenezwa na sheria hiyo kwa divisheni hiyo, ni thamani ya fedha inayohusishwa na makosa hayo, kuwa inaanzia Sh bilioni moja.

“Inapendekezwa kuwa pale makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yanapohusisha thamani ya fedha, basi makosa yatakayofunguliwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, yawe ni yale ambayo thamani yake haipungui Sh bilioni moja,” alisema Masaju.

Lengo la kuweka thamani hiyo ya fedha, limeelezwa kuwa ni kuiwezesha divisheni hiyo kujikita kusikiliza makosa makubwa ya rushwa na uhujumu uchumi, ili makosa madogo yasiyofikia thamani hiyo, yasikilizwe na mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi na Mahakama Kuu.

Hata hivyo, divisheni hiyo pia kwa mujibu wa sheria hiyo itasikiliza makosa mengine ya rushwa na uhujumu uchumi bila kujali thamani ya fedha, kutokana na namna makosa hayo yalivyotendeka, asili yake na ugumu wa kuyawekea thamani ya fedha.

Pia, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amepewa mamlaka ya kutoa hati ambayo itataka mashauri mengine yatakayofunguliwa, yasikilizwe katika divisheni hiyo kwa maslahi ya umma.

Marekebisho mengine yaliyopendekezwa ni pamoja na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi chini ya sheria hii iwe ni kifungo cha gerezani, kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja na hatua nyingine za kijinai, ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zilizopatikana kutokana na makosa hayo.

Kifungo hicho kimeongezwa kutoka katika sheria ya sasa ambayo ndiyo inayorekebishwa, ambayo ilitaka kifungo kisizidi miaka 15. Kwa mujibu wa Masaju, maneno hayo “kifungo kisichozidi miaka 15”, yaliipa Mahakama mamlaka ya kutoa adhabu ndogo zaidi, ilimradi tu adhabu hiyo haizidi miaka 15, jambo lililoonekana kuwa baadhi ya adhabu zilikuwa ndogo kuliko uzito wa makosa.

Katika kutaifisha mali za waliokutwa na hatia, sheria hiyo imeweka masharti ya kuzuia kutumika kwa sheria zinazohusu ufilisi au uamuzi wa kufilisi kampuni, kwa mali ambayo inachunguzwa chini ya Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi.

“Marekebisho hayo yanalenga kukabili vitendo vya watu au kampuni kujifilisisha wakati uchunguzi unapoanza dhidi yao na pia kuhakikisha kuwa mali zote zinazohusika na kosa linalochunguzwa, au linaloendelea mahakamani, inaendelea kuwepo hadi uchunguzi au kesi husika itakapohitimishwa,” alisema Masaju.

Hatua hiyo imetajwa kuwa na nia ya kuiwezesha serikali kutaifisha mali hiyo, wakati kesi husika itakapokamilika na ikathibitika kuwa ina uhusiano na kosa la rushwa na uhujumu uchumi lililothibitishwa mahakamani.

“Kwa ujumla hatua hii ni njia mojawapo ya kuwafanya watu waogope kutenda makosa ya rushwa na uhujumu uchumi na pia kuhakikisha kuwa mhalifu, hanufaiki na uhalifu alioutenda kwa kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi,” alisema Masaju.

Hata hivyo Masaju aliongeza kuwa Marekebisho mengine yaliyoingia katika sheria hiyo, yanahusu ulinzi wa mashahidi, ambapo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), kwa kushauriana na Mkurugenzi wa Mashitaka, wanatakiwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha usalama wa shahidi pamoja na familia yake ikiwa na lengo ni kusaidia usalama wa mashahidi wa kesi hizo, ili mashahidi wawezeshwe kutoa ushahidi wao bila woga, kwa kuwa kesi hizo zinahusisha watu wenye fedha na makosa yanayofanyika ni ya kupanga.

Awali Rais Magufuli alipoahidi kuanzisha mahakama hiyo, wengi walichukulia kama ni suala lisilowezekana, lakini kasi yake ya kusimamia suala hilo, imewafanya baadhi ya mafisadi waingiwe na kihoro na kuanza kutafuta njia za kujinusuru ikiwemo kutoroka nchini.

Mpaka sasa serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha mwaka mmoja imefanikiwa kufungua majalada zaidi ya 300 yanayohusiana na kesi mbalimbali za ufisadi ambayo yako mezani kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ikiwa ni sehemu ya hatua muhimu kabla ya kufikishwa mahakamani.

Post Top Ad