Sheria : Waziri Mkuu, Majaliwa afungua mkutano wa 21 wa Wanasheria wa Afrika Mashariki - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


26 Nov 2016

Sheria : Waziri Mkuu, Majaliwa afungua mkutano wa 21 wa Wanasheria wa Afrika Mashariki


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wiki moja kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe kumpa maelezo kuhusu sababu za Tanzania kutokukamilisha mkataba wa Mawakili wa Afrika Mashariki kutambuana katika utendaji wao.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Novemba 25, 2016) wakati akimuwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika ufunguzi wa mkutano wa 21 wa mwaka wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Nimeshtushwa kidogo kusikia kwenye taarifa yenu kuwa mkataba huo uliolenga nchi zote za Afrika Mashariki hautaihusisha Tanzania kutokana na kutokukamilisha sehemu yao ya kuufanyia kazi, nitahitaji maelezo,”
“Nitapenda kupata maoni yako wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania kwa vile wewe ni Mwanasheria mwandamizi na siyo Mwanasheria  wa Tanganyika Law Society peke yake kwa nini Tanzania haijakamilisha mkataba huu,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa maelezo ya awali aliyopewa kuhusu mkataba huo, utakuwa na umuhimu mkubwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kama ilivyo kwenye sekta nyingine zinazoshirikiana ikiwemo uhandisi, uhasibu, uthamini na uchoraji wa majengo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka Wanasheria hao kuzisaidia nchi zao ili ziondokane na umaskini uliokithiri na Serikali zipate muda wa kushirikisha watu wake katika kufanya kazi kwa lengo la kuwapatia maendeleo.

Amesema nchi zilizoendelea na zinazoendelea, baada ya chaguzi hufanya shughuli za ujenzi wa taifa lao na maendeleo ya watu wake. Ili kudumisha demokrasia wana muda wa mikutano na maandamano na kazi.

“Hawaandamani tu bila kupata kibali cha Polisi, hawaruhusiwi kuzuia magari yasipite, kuzuia kazi isifanyike. Mfano kifungu cha 115 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kinataka kesi zinazotokana na uchaguzi ziwe zimefunguliwa mahakamani ndani ya siku thelathini tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi na ziwe zimesikilizwa na kutolewa maamuzi ndani ya miezi kumi na miwili tangu tarehe ya kufunguliwa mahakamani,” amesema..

Amesema “kwa uelewa wa kawaida, Kifungu hiki ni kuwa jamii inataka masuala ya siasa za uchaguzi yawe na muda wake wenye ukomo maalum ili baada ya hapo wananchi waelekeze muda, nguvu na rasilimali zao nyingine katika kazi au shughuli nyingine za maendeleo na ujenzi wa Taifa lao”.

Aidha, Waziri Mkuu amesema eneo jingine ambalo ni muhimu kulitupia jicho ili kukuza ushindani wa kibiashara katika Jumuia ya Afrika Mashariki ni la uendeshaji wa mashauri mahakamani hasa kwa mashauri ya madai.

“Wote tunakubaliana kuhusu misingi na haki za kidemokrasia kuwa kila mtu anayo haki kikatiba na kisheria kusikilizwa madai yake na kutetea haki zake; na kuwa chombo chenye mamlaka ya kutoa haki ni Mahakama”. Amesema.

Amesema kuna taarifa za kuwepo kwa kesi zenye kuhusisha mali za thamani kubwa zinazochukua muda mrefu sana kumalizika mahakamani huku baadhi ya sababu za kuchelewa kwa kesi hizo ni utoaji wa maombi ya kuziahirisha mara kwa mara kwa sababu binafsi jambo linalosababisha uendeshaji wa kesi kuwa mgumu na kuchukua muda mrefu.

Waziri Mkuu amesema wakati mwingine hata kesi zilizosikilizwa huendelea kubaki mahakamani muda mrefu kutokana na maombi na rufaa za hapa na pale zinazoishia kumnyima mwenye haki fursa ya kutekelezewa haki yake.

“Ni wazi kesi kama hizi zinapohusisha mahusiano ya kibiashara na au mitaji mikubwa ya biashara, matokeo yake ni kudumaza na hata kuua biashara, achilia mbali ushindani wa kibiashara. Ni wajibu wenu Wanasheria kupata ufumbuzi wa tatizo hili lenye athari hasi kibiashara,’ amesema.

Amesema haki ya wadaiwa kusikilizwa kikamilifu na Mahakama, haki na uhuru mlionao Mawakili kuwawakilisha wadaiwa wao bila hofu au shinikizo lolote, viwe chachu ya maendeleo ya ushindani wa kibiashara na visiwe kikwazo.

 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, NOVEMBA 25, 2016.


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Naibu Spika, Dkt.Tulia Ackson baada ya kuwasili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam kufungua  Mkutano wa 21 wa Chama cha Wanansheria wa Afrika ya Mashariki Novemba 25, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Rais wa  Chama cha Wanansheria Afrika ya Mashariki, Wakili Nassor Hamis baada ya kuwasili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam kufungua  Mkutano wa 21 wa Chama cha Wanansheria wa Afrika ya Mashariki Novemba 25, 2016.  Wapili kushoto ni Naibu Spika, Dkt.Tulia Ackson, Watatu kushoto  Jaji Kiongozi, Frednand Wamabali,  wanne kushoto ni Mwanansheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria,Dkt Harrison Mwakyembe.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt, Harrison Mwakyembe (kushoto) na Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ​baada ya kuwasili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam kufungua  Mkutano wa 21 wa Chama cha Wanansheria wa Afrika ya Mashariki Novemba 25, 2016.
 


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Mwaka wa 21 wa Chama cha Wanasheria Afika ya Mashariki   kwenye ​ Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 25, 2016.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.  Harrison Mwakyembe akizungumza katika mkutano wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 25, 2016.

 Baadhi ya washiriki wa Mkutano   wa 21 wa mwaka wa Chama cha Wanansheria Afrika Mashariki wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipofungua mkutano huo  kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 25, 2016.
 aziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Rais wa Chama cha Wanansheria Afrika  Mashariki Wakili Nassor Hamis Mohmmed (kushoto) na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Harrison Mwakyembe (kulia)  baada ya kufungua ​Mkutano wa Mwaka wa 21 wa Chama cha Wanasheria Afrika ya Mashariki  kwenye ​ Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 25, 2016. 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kiwa katika picha na ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa 21 wa Wanansheria Afrika ya Mahariki kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 25, 2016.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.  Harrison Mwakyembe baada ya kufungua mkutano wa 21 wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 25, 2016.

Post Top Ad