Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akifunua kitambaa
kuashiria uzinduzi rasmi wa Mradi wa Umeme wa Maji wa Kilowati 430
katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi (wa kwanza kushoto), Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (wa pili kushoto), Mwakilishi
wa Umoja wa Ulaya (EU), Jane Nunes (wa Tatu kulia), Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt Gideon Kaunda (wa pili kulia)
na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni (wa Nne kulia).
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kutoka
kulia) akipiga makofi mara baada ya uzinduzi rasmi wa Mradi wa Umeme wa
Maji wa Kilowati 430 katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi (wa kwanza kushoto), Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (wa Tatu kushoto), Mwakilishi
wa Umoja wa Ulaya (EU), Jane Nunes (wa Nne kushoto) na Mwenyekiti wa
Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt Gideon Kaunda (wa pili
kushoto).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kushoto) akiangalia moja ya mitambo ya kuzalisha umeme Umeme wa Maji wa Kilowati 430 katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe. Wa
kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema na wa kwanza kulia ni
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Gissima
Nyamo-Hanga.
Na Teresia Mhagama
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amezindua mradi wa
umeme wa Kilowati 430 unaotokana na maporomoko ya maji katika Kata ya
Ikondo mkoani Njombe ambapo mpaka sasa zaidi ya wateja 1140
wameunganishiwa umeme huku zoezi hilo likiwa ni endelevu.
Uzinduzi
huo uliofanyika katika Kata hiyo ulihudhuriwa na Balozi wa Italia
nchini Tanzania, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Mkuu wa Mkoa na Mkuu
wa wilaya ya Njombe, wananchi wa Kata ya Ikondo, Shirika lililotekeleza
mradi huo la CEFA, watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO).
Dkt.
Kalemani alisema kuwa mradi huo umetekelezwa na Taasisi isiyo ya
kiserikali ya CEFA kutoka Italia na kugharamiwa kwa pamoja kati ya
Jumuiya ya Ulaya na Serikali ya Tanzania kwa jumla ya Dola za Marekani
110,209.
Aliongeza
kuwa mradi huo wa umeme utasambazwa katika vijiji vilivyoko kata za
Ikondo, Matembwe na Lupembe na ziada itakayobaki inaingizwa kwenye gridi
ya Taifa.
"
Habari njema ni kuwa tayari vijiji Saba vimeunganishiwa umeme kupitia
mradi huu, hii inatimiza moja ya malengo ya Serikali ya kuhamasisha na
kuwezesha upatikanaji wa nishati bora katika maeneo ya vijijini kupitia
asasi za kiraia," alisema Dkt. Kalemani.
Alisema
kuwa, hadi kufikia mwezi Juni, 2016 idadi ya wananchi wanaopata huduma
ya umeme imefikia asilimia 40 huku vijijini ikiwa ni asilimia 24 na
kueleza kuwa juhudi zaidi zinafanyika ili kufikia lengo la kuunganisha
umeme kwa asilimia 75 ya wananchi ifikapo mwaka 2025.
Aidha,
Dkt. Kalemani aliwasisitiza wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya
maji, kuhakikisha kuwa wanavitunza vyanzo hivyo na mazingira kwa ujumla
ili kuweza kuwa na miradi ya mafanikio kama huo wa Ikondo.
Awali
Meneja Mradi kutoka CEFA, Jacopo Pendezza alisema kuwa Taasisi hiyo ipo
nchini kutoka mwaka 1976 na imejikita katika miradi ya umeme vijijini
na ina miradi mbali mbali ya umeme inayofanya kazi katika Kata ya
Matembwe, Boma la Ng'ombe na Ikondo mkoani Njombe.
Alisema
kuwa awali mradi huo wa umeme wa Ikondo ulikuwa unazalisha Kilowati 80
za umeme lakini kutokana na mahitaji ya wananchi kuongezeka, CEFA kwa
kushirikiana na kampuni ya kijiji cha Matembwe (MVP) inayosimamia mradi
huo, waliamua kuongeza mtambo wa Kilowati 350 na hivyo kupelekea mradi
huo kuzalisha jumla ya kilowati 430 za umeme.
Alisema
kuwa umeme huo umeleta faida mbalimbali ikiwemo uanzishwaji wa miradi
mbalimbali ambayo inawaletea wananchi kipato ikiwemo kiwanda cha
kutengeneza chakula cha mifugo, soseji, mafuta ya kupikia, na kutumika
katika shughuli za useremala na ushonaji wa nguo.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa EU katika uzinduzi huo, Jenny Nunes alisema
kuwa mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kuboresha maisha
ya wananchi kiuchumi, kusaidia wanafunzi katika masomo na huduma
nyingine muhimu za kijamii, na kusaidia juhudi za kupambana na
mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema
kuwa EU itaendelea kusaidia miradi ya umeme nchini ili wananchi wengi
wapate nishati hiyo muhimu na kwamba zaidi ya shilingi bilioni 400
zitatumika kwa ajili ya sekta husika.
Aidha,
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi alisema kuwa makao makuu ya
wilaya zote mkoani Njombe, yameunganishwa na huduma ya umeme na kwamba
vijiji 250 kati ya 384 katika Mkoa huo tayari vinapata huduma ya umeme.
Alisema
kuwa mkoa huo unazalisha mazao mbalimbali ikiwemo Chai, ambapo ili
kuongezea thamani ya mazao hayo, lazima kuwe na umeme wa uhakika
utakaosambazwa katika vijiji vyote vya Mkoa husika.
No comments:
Post a Comment