Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeishauri Serikali kuanzisha
mfumo maalum wa uwekezaji ili fedha zitakazowekwa katika mfuko huo
zitumike kama mtaji katika maeneo ambayo nchi inataka kuwekeza.
Ushauri
huo umetolewa mjini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Naghenjwa
Kaboyoka alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo iliyochambuliwa
kwa kina juu ya changamoto, maombi na mapendekezo yatakayoiwezesha nchi
kusonga mbele.
Mwenyekiti
Mhe. Kaboyoka amesema kuwa ushauri huo umetolewa baada ya kukwama kwa
baadhi ya miradi pamoja na shughuli nyingine za Serikali zinazofanywa
ili kuwasaidia wananchi kutokana na ukosefu wa fedha za kufanyia
shughuli hizo hivyo kuanzishwa kwa mfuko huo kutahakikisha faida ya
uwekezaji inaonekana.
“Sisi
kama kamati tunaishauri Serikali kuanzisha mfuko maalum wa uwekezaji
kwani utaisaidia Serikali kupata fedha za kufanyia maendeleo na kupata
mitaji ya kuwekeza sehemu mbalimbali ili kuhakikisha maslahi ya nchi
yanalindwa na watanzania wanaiona faida ya uwekezaji”, alisema Mhe.
Kaboyoka.
Mhe.
Kaboyoka aliongeza kuwa kamati hiyo imependekeza kuwa mfuko huo
uanzishwe chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kutumia mfumo wa
kubakisha mapato kwa sababu ofisi hiyo ndiyo ina mamlaka ya kugawa fedha
za Serikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Aidha,
taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali imebaini kuwa pamoja na kuwa Idara
ya Uhamiaji imeweka usimamizi wa utoaji wa viza katika Makao Makuu ya
Idara, kwenye Balozi pamoja na maeneo ya mipaka ya nchi lakini mfumo wa
kutoa viza kwa wageni wanaowasili nchini hauna mawasiliano mazuri.
Kukosekana
kwa mawasiliano hayo kunasababisha mianya ya upotevu wa mapato ya
Serikali yanayotakiwa kukusanywa kutokana na utoaji wa viza hivyo kamati
pia imeiomba Serikali kukamilisha haraka mradi wa Uhamiaji Mtandao (E-
Migration) ili kuboresha njia za ukusanyaji wa mapato katika Idara hiyo.
Kwa
upande wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
iliyowasilishwa Bungeni hapo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vedasto
Ngombale Mwiru ambaye ameelezea matatizo sugu ya matumizi mabaya ya
fedha za Umma katika Serikali za Mitaa pamoja na ushauri wa kamati hiyo
katika kuhakikisha tatizo hilo linakoma.
Mhe.
Ngombale Mwiru ameeleza kuwa Kamati imebaini udhaifu wa watendaji wa
Halmashauri mbalimbali nchini katika usimamizi wa mikataba ya
utekelezaji wa maendeleo unaopelekea miradi hiyo kuchelewa kukamilika,
kukamilika kwa kiwango cha chini au kutokukamilika kabisa.
“Kulingana
na taarifa hiyo, kamati imezishauri Halmashauri zote nchini kutofanya
kazi kwa mazoea na badala yake kusimamia miradi hiyo kwa ukaribu ili
iweze kukamilika kwa wakati na kutumika kama ilivyo kusudiwa”, alisema
Mhe.Ngombale Mwiru.
Ameongeza
kuwa kumekuwa na tatizo katika Halmashauri hizo la kutotenga asilimia
10 ya fedha za mapato kutoka katika vyanzo vya ndani kwa ajili ya mfuko
wa wanawake na vijana ambapo kuna baadhi ya Halmashauri hazijawasilisha
michango hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu.
Kutokana
na tatizo hilo, Kamati imetoa agizo kwa Halmashauri zote kuandika barua
ya kuthibitisha kulipa madeni hayo pia kuelezea mipango watakayotumia
katika kutekeleza ulipaji huo.
Pia
Kamati imeishauri Serikali kuleta Bungeni Muswada wa Sheria ya Mfuko wa
Maendeleo ya wanawake na vijana ili iwe sheria ambayo itatekelezwa kwa
lazima hivyo kuendelea kuinua maisha ya wanawake na vijana kama
ilivyokusudiwa.
Baada
ya kamati zote mbili kuwasilisha taarifa hizo mbele ya Bunge,sasa ni
zamu ya wabunge kujadili kwa kina masuala yaliyozungumziwa katika
taarifa hizo kwa kutoa maoni yao na kuishauri Serikali kuhusu mapungufu
yaliyojitokeza katika matumizi ya fedha kwa kuyapatia ufumbuzi ili
yasijirudie katika taarifa zijazo.
No comments:
Post a Comment