Elimu : Wanafunzi elimu ya juu watengewa zaidi ya Bilioni 480 za Mikopo - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Friday, 4 November 2016

Elimu : Wanafunzi elimu ya juu watengewa zaidi ya Bilioni 480 za Mikopo

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.

Jumla ya wanafunzi 119,012 wa Elimu ya Juu nchini wametengewa kiasi cha shilingi bilioni 483 Katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kupewa mikopo itakayowasaidia kujikimu pindi watakapokuwa vyuoni.

Kiasi hicho cha fedha kimetajwa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017.

Prof. Ndalichako amesema kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa kuzingatia malengo ya Mfuko wa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo kigezo kikuu kimekuwa ni uhitaji wa mwanafunzi pamoja na fani za kipaumbele anayosoma mwanafunzi.

Fani za kipaumbele kwa mujibu wa Wizara hiyo ni pamoja na Sayansi za Tiba na Afya, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mifugo, Uhandisi wa Viwanda pamoja na Kilimo na Umwagiliaji.

Prof. Ndalichako ameongeza kuwa kuna baadhi ya wanafunzi ambao wamedahiliwa kwenye fani za kipaumbele lakini hawana vigezo vya kupewa mikopo kutokana na tathmini ya uhitaji kuonesha kuwa wanaweza kusomeshwa na wazazi au walezi wao. 

“Kwa mwaka huu wa fedha, Serikali imeongeza kiasi cha fedha zinazotakiwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu waliochaguliwa na wanaondelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini kutoka shilingi bilioni 473 hadi bilioni 483 ambayo itaweza kugharamia wanafunzi wanaoanza 25,717 na wanaoendelea na masomo 93, 295”, alisema Prof. Ndalichako.

Ameongeza kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali za utoaji mikopo ambazo pamoja na mambo mengine zinachangiwa na mfumo wa udahili wa wanafunzi katika Vyuo vya Elimu ya Juu ambapo kwa sasa kuna mgongano kati ya Tume ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu pia kutokuwa na tarehe moja ya Taasisi zote za Elimu juu ya kufungua vyuo kunaleta mkanganyiko.

Akiongelea kuhusu wanafunzi wanaoanza chuo mwaka huu, Prof. Ndalichako amesema kuwa jumla ya wanafunzi 58,010 wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu na orodha yao tayari ilishawasilishwa katika Bodi ya Mikopo na hadi kufikia Novemba 2 mwaka huu jumla ya wanafunzi 21,190 wameshapewa fedha hizo.

Waziri amefafanua idadi ya wanafunzi hao waliopata mikopo kuwa 4,321 ni yatima,118 wana ulemavu na wanafunzi 87 ni wale waliosoma shule za Sekondari kwa ufadhili wa watu binafsi au Taasisi mbalimbali.Aidha, Prof. Ndalichako amesisitiza kuwa jumla ya wanafunzi 25,717 wanaoendelea na masomo waliokuwa na mikopo wataendelea kupatiwa mikopo hiyo kama ilivyokuwa katika mwaka wa masomo uliopita.

“Napenda kuwatoa hofu wanafunzi wanaoendelea kuwa Serikali haijafuta mkopo kwa mwanafunzi yoyote anayeendelea na masomo, kwa wanafunzi ambao vyuo vyao vimewasilisha taarifa za matokeo ya wanafunzi wao Bodi imekwishawatumia fedha zao za mkopo”, alisema Prof Ndalichako.

Katika taarifa hiyo, Prof, Ndalichako ameelezea kuwa taratibu za kuwabaini wanafunzi wasio na sifa stahiki zinaendelea na zitakapokamilika wanafunzi hao hawatopewa mkopo, ameahidi kufanya mapitio ya udahili wa wanafunzi vyuoni pamoja na utaratibu mzima wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo kwa lengo la kuwa na mfumo bora zaidi.

No comments:

Post a Comment