Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akifuatilia kwa makini
wakati Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji kutoka kituo cha uwekezaji
Tanzania-TIC, John Mnali, akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji
zinazopatikana Tanzania, wakati wa mkutano wa 5 wa ushirikiano wa
kiuchumi kati ya Korea ya Kusini na nchi za Afrika (KOAFEC), Mjini
Seoul, Korea Kusini. Kulia kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Utafutaji
Rasilimali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Zanzibar-Sabra Issa
Machano.
Mkurugenzi
wa Uhamasishaji uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC, John
Mnali (Katikati), akibadilishana mawasiliano na mmoja wa
wafanyabiashara walioonesha nia ya kuweka nchini Tanzania baada ya
Mkurugenzi huyo kuwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji
zinazopatikana Tanzania, wakati wa mkutano wa 5 wa ushirikiano wa
kiuchumi kati ya Korea ya Kusini na nchi za Afrika (KOAFEC), Jijini
Seoul, Korea Kusini.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), akibadilishana mawasiliano
na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MarineBio, Heo Yun-Young, ambaye
kampuni yake inataka kuwekeza kiwanda cha kusindika zao la mwani
linalopatikana katika Bahari Kuu ya Hindi nchini Tanzania.
Msaidizi
wa Waziri wa Fedha na Mipango, Edwin Makamba, akiwa katika picha ya
pamoja na Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Benki ya EXIM ya Korea
Kusini, Lee Duk-Hoon baada ya hafla ya usiku ya kuagana kwa washiriki wa
mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za
Kiafrika, Jijini Seoul, nchini Korea kusini.
Mkurugenzi
wa Uhamasishaji uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC, John
Mnali, akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana
Tanzania, wakati wa mkutano wa 5 wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya
Korea ya Kusini na nchi za Afrika (KOAFEC), Jijini Seoul, Korea Kusini
Maofisa
kutoka wizara ya Fedha na Mipango, Edwin Makamba ambaye ni msaidizi wa
Waziri wa Fedha na MIpango, kushoto, na Mkuu wa idara ya Sera, Shogolo
Msangi, wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kuhusu fursa za uwekezaji
zilizopo Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, wakati wakati wa mkutano wa
5 wa ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na nchi za Kiafrika,
uliomalizika leo Jijini Seoul, Korea Kusini
Mkuu wa
kitengo cha utafutaji Rasilimali, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango,
Zanzibar, Sabra Issa Machano, akiwasilisha mada kuhusu fursa za
uwekezaji zinazopatikana Tanzania Zanzibar, wakati wa mkutano wa 5 wa
ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea ya Kusini na nchi za Afrika
(KOAFEC), Jijini Seoul, Korea Kusini.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akimpongeza Mkuu wa
kitengo cha utafutaji Rasilimali, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango,
Zanzibar, Sabra Issa Machano, baada ya akiwasilisha mada kuhusu fursa za
uwekezaji zinazopatikana Tanzania Zanzibar, wakati wa mkutano wa 5 wa
ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea ya Kusini na nchi za Afrika
(KOAFEC), Jijini Seoul, Korea Kusini.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), akisalimiana na mwanafunzi
wa Kitanzania anayesomea Chuo Kikuu kimoja nchini Korea Kusini kuhusu
masuala ya biashara ya kimataifa na uchumi, Alice Mwamzanya, baada ya
kushiriki mkutano wa 5 wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea Kusini
na Nchi za Afrika (KOAFEC), Jijini Seoul nchini Korea Kusini.(Picha na Benny Mwaipaja-Wizara ya Fedha na Mipango)
…………………………………………………..
Benny Mwaipaja,WFM, Seoul, Korea
WAFANYABIASHARA
wakubwa kutoka KOREA ya Kusini, wamekaribishwa kuja kuwekeza nchini
Tanzania katika sekta ya viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa za
kilimo, mifugo, mazao ya bahari pamoja na kutumia malighafi
zinazopatikana nchini ili kusisimua uchumi wa taifa na kukuza ajira.
Wito huo
umetolewa Jijini Seoul nchini Korea, na Mkurugenzi wa Uhamasishaji
uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC, JOHN MNALI, wakati
akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania,
wakati wa mkutano wa 5 wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea ya
Kusini na nchi za Afrika(KOAFEC).
Mnali
amesema kuwa Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo
kuondoa urasimu wa upatikanaji wa vibali vya kuwekeza na ardhi kwa ajili
ya uwekezaji huo ili kuvutia mitaji na teknolojia kutoka nje ya mipaka
yake.
Amewashauri
wawekezaji hao kufufua viwanda ambavyo havifanyi vizuri nchini, ili
kuanza uzalishaji wa bidhaa zitakazotumia malighafi zinazopatikana
nchini pamoja na kutumia soko kubwa lililopo katika ukanda wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na soko la AGOA la Marekani.
Kwa
upande wake Mkuu wa Idara ya Utafutaji Rasilimali, kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango Zanzibar, Sabra Issa Machano, amewahimiza wawekezaji wa
Korea kwenda kuwekeza Visiwani humo na Tanzania kwa ujumla katika sekta
za kilimo, viwanda na uvuvi wa samaki na mwani katika Bahari Kuu ili
wakazi wa nchi hiyo na wawekezaji waweze kunufaika na rasilimali
zilizoko visiwani humo.
Amewahimiza
wawekezaji hao kujenga hoteli za kisasa kwa ajili ya kuhudumia soko la
utalii ambalo ni kubwa nchini humo, pamoja na kutumia mandhari ya Mji
Mkongwe wa Zanzibar ambao ni kivutio kikubwa cha watalii baada ya
kutangangazwa na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya
sayansi na utamaduni-UNESCO kuwa mji wa urithi wa Dunia.
Baadhi ya
wawekezaji ikiwemo kampuni ya Youngsan, inayojihusisha na utengenezaji
na usambazaji wa vipuri vya magari pamoja na kampuni ya MarineBio
inayojihusisha na biashara ya utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na
mwani, wameonesha nia ya kuwekeza Tanzania baada ya kuvutiwa na
mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania.
“ Kampuni
yetu imetafuta kwa muda mrefu fursa ya kuwekeza Tanzania lakini
tulikuwa hatufahamu ipasavyo njia za kutumia kufikia uwekezaji huo
ambapo sisi tunajihusisha na biashara itokanayo na zao la mwani
linalozalishwa kwa wingi Zanzibar ambapo tunatengeneza bidhaa za
karatasi, urembo, karatasi na vitu vingine vingi” alisema Yun-Young
Amesema
kuwa wanatarajia kufungua kiwanda kikubwa ambacho kitazalisha ajira kwa
wakulima na wafugaji wa samaki nchini Tanzania kwakuwa kampuni yake
itajihusisha na biashara kubwa itakayochangia kukuza ajira na kuwafanya
watu wengi hususan wanawake, waondokane na umasikini wa kipato.
Katika
Mkutano huo uliomalizika leo, Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ambaye amemwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ambapo,
Tanzania imesaini mkataba mmoja pamoja na Makubaliano ya ushirikiano wa
pamoja kwa ya upanuzi wa miundombinu ya maji taka katika Jiji la Dar es
salaam na ujenzi wa njia ya umeme yenye msongo wa kV400 kutoka Mbeya,
Kigoma hadi Nyakanazi.
No comments:
Post a Comment