Matukio : Viongozi wa Vyama vya Siasa watakiwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa Vitendo - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Monday, 26 September 2016

Matukio : Viongozi wa Vyama vya Siasa watakiwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa Vitendo


Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani akiwasili nyumbani kwa familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Butiama Musoma akiwa ameambatana na watumishi wa NEC na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa ALAT kutoka maeneo mbalimbali kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Mwitongo wilayani Butiama. Tume ya Taifa ya Uchaguzi iko mkoani Mara kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi. 
Na. Aron Msigwa – NEC, Musoma.
Viongozi wa vyama vya Siasa wametakiwa kuiga kwa vitendo uzalendo na moyo wa kujitoa aliokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake ili kuliwezesha Taifa kupiga hatua kimaendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani mara baada kutembelea Kaburi na Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo wilayani Butiama.
Amesema kuwa kumbukumbu za Baba wa Taifa zilizohifadhiwa vizuri katika makumbusho hiyo zina mambo mengi ya kujifunza ambayo wanasiasa wanatakiwa kuyafanya kwa vitendo hasa uzalendo kwa nchi, uvumilivu, upendo na moyo wa kujitoa kwa dhati kuwatumikia wananchi.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani (Kushoto) akisalimiana na Msemaji Mkuu na kiongozi wa familia ya Baba wa Taifa Chifu Japhet Wanzagi (kulia) mara baada ya kuwasili eneo la Mwitongo wilayani Butiama. Wa Pili kutoka Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Butiama Bi. Annarose Nyamubi.
“Kupitia kumbukumbu hizi sisi watumishi wa Tume tumejifunza ukomavu wa demokrasia aliokuwa nao Mwalimu Nyerere akiwa ndani na nje ya Bara la Afrika, wengi wanadhani Demokrasia ni wakati wa uchaguzi tu, kumbe demokrasia ni pamoja na kuheshimu watu wengine” Amesema Kailima.
Ameeleza kuwa maisha aliyoishi Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa na viongozi na watanzania wote hasa pale alipojitofautisha na viongozi wengi wa Bara la Afrika alipoepuka tamaa ya madaraka na mali kwa manufaa ya taifa.
“Sote ni mashahidi kupitia kumbukumbu zake tumeona mahali alipokuwa anaishi mwalimu Nyerere kabla hajajengewa nyumba na Jeshi, kama Rais mstaafu wengi walitegemea asingeishi katika eneo lile, kumbukumbu hii nzuri aliyoiacha inatufundisha watanzania kuwa mwalimu aliitanguliza Tanzania mbele kuliko maslahi yake binafsi” Amesisitiza Kailima.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani akiwasha mshumaa kwenye kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo, Butiama. Wengine wanaoonekana na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa ALAT na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Bw. Kailima amebainisha kuwa NEC itaendelea kumuemzi Baba wa Taifa kwa yale aliyoyafanya na kuyasimamia kwa manufaa ya taifa huku akitoa wito kwa viongozi wa vyama vya Siasa wawe na kiasi na waridhike na vile walivyonavyo.
“Suala la kuridhika na kuwa na kiasi linapaswa kuzingatiwa, wanasiasa wanapaswa kuwaheshimu wananchi wanaowachagua kupitia chaguzi mbalimbali, matokeo yanapotoka kama ni sahihi basi wanasiasa wakubaliane na maamuzi yao” Ameainisha Kailima. 
Kwa upande wake Mhifadhi wa Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Bw. Jacob Thomas amesema kuwa watanzania wanayo mengi ya kujifunza kupitia vitu alivyoviacha Baba wa Taifa ambavyo vimehifadhiwa katika Makumbusho hiyo.
Amesema kuwa maisha ya uadilifu aliyoishi enzi za uhai wake na mchango wake katika kuiletea maendeleo Tanzania na Bara la Afrika vinapaswa kuenziwa kwa nguvu zote na viongozi wa Tanzania. 
“Ninyi mliopata nafasi ya kuitembelea makumbusho hii mmejifunza vitu vingi kumhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba alikuwa ni mtu wa namna gani kwa viwango vya Afrika na dunia kutokana na kumbukumbu ya uadilifu aliyoiacha ndani na nje ya mipaka ya Tanzania”
Muongoza wageni wa maeneo ya historia nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwitongo Butiama Bi. Gaudensia Waziri akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani (mwenye kofia) kuhusu Kaburi na historia ya Chifu Burito aliyekuwa chiefu wa Kabila la Wazanaki.
Mwongoza wageni na Mhifadhi wa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere Butiama, Jacob Thomas akitoa maelezo kuhusu picha za kumbukumbu za Baba wa Taifa kwa Mkurugenzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani na watumishi wa NEC walioitembelea makumbusho hiyo eneo la Mwitongo, Butiama –Musoma.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa NEC waliotembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mwitongo, Butiama. 

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi waandishi wa habari wa mkoa wa Mara waliotembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mwitongo, Butiama. Watendaji wa NEC wako mkoani Mara kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment