Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) itaanza kutoa Vitambulisho vipya vya
Taifa vyenye saini kwa wananchi wote waliokamilisha taratibu za usajili
na utambuzi na kuchukuliwa alama za kibaiolojia (Alama za vidole, Picha,
Saini ya Kielektroniki).
Kwa
mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Bw. Andrew Massawe; utekelezaji
wa zoezi hilo utaanza rasmi Jumanne tarehe 14 Septemba 2016 katika
ofisi zote za NIDA zikiwemo ofisi za Wilaya zilizoanza usajili Tanzania
Zanzibar na mikoa ya Dar-es-salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro,
Tanga, Arusha, Kilimanjaro, na Ruvuma) pamoja na waheshimiwa Wabunge
Dodoma.
Waombaji
wote ambao Vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa
maandishi (SMS) katika simu zao za kiganjani (mkononi) kufahamishwa
kufika katika vituo vya Usajili kuchukua Vitambulisho vyao.
Kuhusu
wananchi ambao tayari wana Vitambulisho visivyo na saini; Bw. Massawe
amesema…. “ Mamlaka inakusudia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani
visivyo na saini, ila kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea
kutumika sambamba na vipya wakati taratibu za kuendelea kuvibadilisha
zikiendelea” alisisitiza.
Amesema
kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za
mwombaji zilizomo ndani ya kifaa maalumu kilichofichwa kwenye kadi ya
mtumiaji (chip); ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea
kutumika katika huduma mbalimbali zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla
ya kupata huduma.
Akizungumzia
wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa, Bw. Massawe amesisitiza kwamba
wananchi wote ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na
kuendelea; kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, kuendelea
kujitokeza kwa wingi kusajiliwa ili kupata Vitambulisho vya Taifa kwani
zoezi la usajili ni endelevu.
“Kwa
wale wananchi ambao walisajiliwa kupitia Daftari la Mpiga kura NEC;
NIDA iko mbioni kuanza kutoa nambari za utambulisho wakati tukiendelea
kukamilisha taratibu za usajili ili kupata utambulisho kamili na kuanza
kunufaika na matumizi mapana ya Utambulisho wa Taifa wakati taratibu za
uzalishaji wa Vitambulisho zikiendelea”.
Wananchi
wanakumbushwa kutunza vizuri Vitambulisho vyao ili kuepuka gharama
kwani kitambulisho cha Taifa kwa mara ya kwanza kitatolewa bure na iwapo
kitapotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji akilipie.
Kwa
sasa vitambulisho vya Taifa vimeanza kutumika katika baadhi ya huduma
nchini hususani kwenye mabenki kwa ajili ya kufungua akaunti na
kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupatiwa huduma. Taratibu za
kupanua wigo wa matumizi ya Vitambulisho kielektroniki kwa kushirikiana
na Taasisi mbalimbali zinaendelea.
No comments:
Post a Comment