
Makamu
wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkaribisha kwa mazungumzo
Ofisini kwake katika Jengo la SMZ Magogoni Jijiji Dar es salaam Balozi
wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Lu Youqing.

Balozi
wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Lu Youqing kati kati akielezea
mikakati atakayoitekeleza katika kuratibu usimamizi wa miradi ya
Zanzibar iliyopata ufadhili wa Nchi yake ya China.

Makamu
wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Lu Youqing mara baada ya
mazungumzo yao ya kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na China.Picha
na – OMPR – ZNZ.
Balozi
wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania Bwana Lu Youqing ameahidi
kufanya jitihada za makusudi katika kufuatilia taratibu za Mikataba ya
makubaliano kwa upande wa Nchi yake ili kuona kwamba miradi yote ya
Zanzibar iliyopata ufadhili wa Nchi hiyo inaanza, inaendelea na
kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza
na Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipomtembelea
Ofisini kwake katika Jengo la SMZ Magogoni Jijiji Dar es salaam Balozi
Lu Youqing aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa
Bandari ya Mpiga Duri, ukamilishaji wa ujenzi wa eneo la maegesho ya
Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar pamoja na Mradi wa Kisasa wa
mawasiliano kwenye ofisi zote za SMZ { E government }.
Balozi
Lu Youqing. alisema zipo taratibu za ukamilishaji wa Miradi
iliyoanzishwa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili ambayo imeonekana
kuchelewa kiasi kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Serikali
ya Jamuhuri ya China kwa Uongozi wa Benki ya Taifa ya China { Exim Bank
}.
Alisema
jukumu alilonalo kwa sasa ni kuzungumza moja kwa moja na Uongozi wa
Benki hiyo kupitia Wizara ya mambo ya Nje ya China ili kupata uelewa wa
masuala hayo katika azma ya kuangalia mapungufu yaliyojitokeza ya miradi
hiyo na kutafuta mbinu za pamoja za kuyakamilisha.
Balozi
Youqing Alieleza kwamba hatua hiyo inafuatia kuheshimu Vikao na
mazungumzo ya pamoja kati ya Viongozi Wakuu Rais Shii Jinping wa
Jamuhuri ya Watu wa China na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barazala
la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kuhusu Miradi hiyo ya Kiuchumi na
Maendeleo.
Alifahamisha
kwamba Historia inaonyesha wazi kwamba Visiwa vya Zanzibar vina
kumbukumbu ndefu ya kuwa Kituo cha Kibiashara Duniani kwa karne nyingi
zilizopita kikitumiwa pia na wafanyabiashara wa Bara la Asia wakiwemo
wale wa Jamuhuri ya Watu wa China.
Balozi
Youqing aliahidi kwamba kwa kutumia uwezo wake wa Kidiplomasia
atahakikisha kwamba Nchi yake inaendelea kufanyakazi pamoja na Tanzania
na Zanzibar kwa ujumla katika kuimarisha miundombinu itakayosaidia
kukuza kwa uchumi wa Tanzania hasa sekta ya Kibiashara itakayosaidia
kustawisha wananchi walio wengi.
“
Nitafanya juhudi za makusudi kwa kuuhimiza Uongozi wa Exim Benki ya
China inayoratibu uwezeshaji wa miradi ya Kiuchumi na Maendeleo katika
Mataifa rafiki hasa yale ya Bara la Afrika kukamilisha taratibu ili
kutoa fursa ya kukamilisha miradi yote iliyoanzishwa ”. Alisema Balozi
Youqing
Alisema
Benki hiyo ya Exim imekuwa na mpango Maalum kwa uratibu wa Nchi hiyo
kuunga mkono ufadhili wa Uwezeshaji wa Miradi mikubwa iliyoanzishwa na
Mataifa Rafiki na Nchi hiyo katika kipindi cha Miaka Kumi.
Balozi
wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania amwapongeza Wananchi wa
Zanzibar kwa jitihada zao za kukamilisha zoezi la Pili la Uchaguzi Mkuu
wa Mwezi Machi mwaka huu kwa misingi ya amani na utulivu.
Alisema
China imeguswa na hali hiyo kiasi kinachoonyesha kuridhika kwake na
kuwa na shauku ya kuzidi kuunga mkono maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar
katika kujikwamua Kiuchumi.
Mapema
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishukuru
Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Balozi Zake za Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla katika kusaidia miradi ya Maendeleo ya Wananchi wa
Zanzibar.
Balozi
Seif alisema China imeonyesha wazi imani yake kwa Zanzibar katika
kusaidia kuunga mkono miradi ya ujenzi wa Gati ya Kwampigaduri Maruhubi,
Maegesho ya Ndege katika uwanja wa Ndege wa Zanzibar pamoja na
ukamilishaji wa Mradi wa Kisasa wa mawasiliano kwenye Ofisi za SMZ { E.
government }.
Alisema
muendelezo wa Serikali ya China katika kuiunga mkono Zanzibar unaleta
faraja na matumaini makubwa kwa Wananchi waliowengi wa Visiwa vya
Zanzibar katika kukomboka kiuchumi.
Balozi
Seif alitolea mfano ukombozi huo ni ule ujenzi wa Gati ya Kisasa ya
Mpigaduri ambao utasaidia kukwamua msongamano mkubwa uliopo hivi sasa
katika Bandari Kuu ya Malindi hasa uhifadhi wa Makontena yanayoshushwa
na kuingia kwa kasi kubwa.
Alimfahamisha
Balozi huyo wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba hivi karibuni alijionea
hali halisi ya mrundikano wa Makontena yanayozagaa na kushindwa hifadhi
ndani ya Bandari ya Malindi hali ambayo imeleta wasi wasi mkubwa kwa
wafanyabiashara wengi walioagiza bidhaa zao kwa ajili ya Siku Kuu ya
Iddi el-Fitri.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/7/2016.
No comments:
Post a Comment