Maisha ni safari ya aina yake. Ndani ya safari moja, zipo nyingine nyingi. Pengine ukweli huo ndio chanzo cha ule usemi kwamba safari moja huanzisha nyingine. Kilicho muhimu ni kwanza kuianza safari yenyewe[moja].
Ninachokiongelea hapo juu kina ukweli zaidi katika maisha ya Salma Msangi ambaye leo kwa wengi ni mtangazaji wa luninga na radio mwenye tabasamu zito, wepesi wa kuelewa mazingira na mwenye kuipenda kazi yake na kuwapenda mashabiki,watazamaji wa vipindi vyake vya kwenye luninga na wasikilizaji wa vipindi vyake radioni.
Mara ya kwanza nilimuona Salma akiwa binti mdogo tu aliposhiriki shindano la kumtafuta mrembo wa Wilaya ya Ilala[ Miss Ilala]. Ilikuwa mwaka 2003. Ukumbi ulikuwa ni Diamond Jubilee. Endapo kungekuwa na mizani ya kupima nani angefika mbali sio tu katika shindano lile bali maishani kwa ujumla, bila shaka Salma angekuwemo. Kilichomtofautisha yeye na wengine si urembo. Ni kujiamini. Bado ninakumbuka jinsi alivyojibu swali. Jibu lake halikuwa jibu sahihi kupita yote. Lakini jinsi alivyolijibu, ilitosha kumuweka katika ukurasa mwingine.
Ndivyo safari yake ilivyoanza. Safari ile ikaanzisha safari nyingine na nyingine mpaka kufikia hapa alipo. Leo hii Salma Msangi ni mtangazaji anayefahamika na mwenye wafuasi wake lukuki ilhali akiendelea kujifunza mambo mengi zaidi na hivyo kuongeza maarifa kila kukicha.
Hivi karibuni nilipata bahati ya kufanya naye mahojiano ambayo utayasoma hivi punde. Endapo uliwahi kutamani kujua amefikaje hapo alipo,fursa ndio hii. Endapo unataka kujua Salma ana mtizamo gani kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii kama vile wanawake, mitandao ya kijamii, wasanii nk, fursa ndio hii. Kikubwa zaidi, Salma ana ushauri ambao naamini kila mtu anapaswa kuusoma hususani vijana.Uuze “sembe” au ufanyeje? Ungana nami….
BC: Salma, karibu sana ndani ya BC na shukrani nyingi kwa kukubali kufanya nami mahojiano haya. Mambo yanakwendaje?
Salma: Mambo sio mabaya tunashukuru tunasonga. Ahsante sana Jeff, Kaka hahaa.. kwetu kumoja weweee au sio? Nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kutaka kufahamu kidogo kuhusu mimi. Mara nyingi huwa sipendi interview na nimekuwa nazikwepa kweli. Huwa naogopa maswali lakini nitajaribu.
BC: Naam, kweli kabisa mimi na wewe njia moja.Salma Msangi ni nani? Alianzia wapi mpaka kufikia hapa alipo?
Salma: Salma Msangi ni msichana aliyezaliwa miaka 29 iliyopita katika wilaya ya Same Mjini mkoa wa Kilimanjaro. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi Masandare hapo hapo Same kabla ya kuhamia jijini Dar Es Salaam kuungana na mama yake mzazi kwa ajili ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Kabla ya hapo Salma alilelewa na Mama yake mkubwa ambaye alikua ameolewa na Mjerumani. Hii ni baada ya mama yake mkubwa kuamua kumchukua kwasababu wakati anazaliwa mama yake alikua na umri mdogo kama wa miaka 18 hivi kwa hiyo ndugu na jamaa wakashauriana na kukubaliana kwamba kutokana na umri huo mdogo asingeweza kumpa mtoto matunzo mazuri au yanayostahili. Alikuwa bado mdogo na kwa ujumla angehitaji kuendelea zaidi na jitihada zake katika maisha.
Hivyo nilihamia Dar Es Salaam sehemu ambapo mama yangu alihamia katika harakati za kutafuta maisha. Nikajiunga na shule ya sekondari Alharamain Islamic na kumaliza elimu yangu ya sekondari pale mwaka 2001. Baada ya hapo kilichofuata ni kozi mbali mbali nilizojiunga nazo ikiwemo masomo ya IT katika chuo cha Issam Computer Networking.
Lakini wakati hata sijahitimu masomo yangu ya Information Technology ndipo nilipokutana na muigizaji maarufu Single Mtambalike almaarufu kama Richie. Hiyo ilikuwa ni mwanzoni mwa mwaka 2003. Kipindi kile alifahamika zaidi kutokana na kucheza tamthilia ya Mambo Hayo iliyokua inarushwa na kituo cha luninga cha ITV.
Akiwa na wenzie waliniona nikiwa natoka college wakavutiwa na mimi baada ya kuniona nimekaa ki mrembo mrembo lol, I mean kwa vigezo walivyokua wanavitazama; urefu, wembamba labda na u-cute (wink) na wao kwa wakati huo walikuwa wanaandaa mashindano ya urembo katika kitongoji cha Kariakoo ambacho kipo chini ya Wilaya ya Ilala.
Basi katika ushawishi wakaniambia kuwa nafaa kushiriki shindano hilo. Ilibidi kuwashirikisha wazazi wangu ambaye ni Mama na Step Dad wangu ambapo ugumu ulikuwa kwa baba kidogo lakini baadae alielewea….
Mama akiwa mdhamini wangu wa kwanza katika suala la mavazi na kila kitu nilishiriki mashindano ya kitongoji cha Kariakoo nikashinda na kupata ticket ya kushiriki mashindano ya Wilaya ya Ilala ambayo ni hatua iliyofuata. Kwa bahati nzuri niliingia katika nafasi ya tatu [Top Three] iliyonipa tiketi ya kushiriki mashindano ya taifa [Miss Tanzania] ambapo niliambulia mataji ya Top Models Of The Year, Most Charming Girl in the Camp of 2003. Taji la Miss Tanzania mwaka huo lilikwenda kwa Sylvia Bahame.
Mambo hayakuwa mabaya maana ushiriki wangu wa mashindano ya urembo ulinipa exposure ya kutosha kiasi kwamba baada ya hapo kazi ilikuwa kwangu tu kuamua au kuchagua nataka kuwa nani na kufanya nini. Katika umri mdogo wa mika 18 nilianza kupata mawazo mapya na kuona ulimwengu ulivyo.
Wakati bado ni mrembo mbichi kabisa ikiwa ni siku kadhaa tangu nitoke katika kambi ya Miss Tanzania na kumaliza shindano wasichana wanne tulipata deal ya kuwa ushers [wasichana wapamba shughuli] katika sherehe za kutimiza miaka 35 ya Scania Duniani iliyofanyika katika Hotel ya kimataifa Ya Golden Tulip Ya Jijini Dar eS salaam. Nakumbuka hiyo deal tulipewa na Ruge Mutahaba akishirikiana na Mjuni Warioba. Kwenye shughuli hiyo ndipo nilipokutana na Mkurugenzi wa kituo cha Channel Ten wa wakati huo, Franko Tramontano.
Aliponiona tu alivutiwa na mimi na akanishawishi kuwa nina uwezo wa kutangaza. Nakumbuka nilikuwa nakataa kwa nguvu zote nikijua kwamba sijawahi kufanya kitu kama hicho. Yeye aliendelea kunishawishi kwamba naweza. Basi tukakubaliana kwamba ananipa nafasi katika kituo chake ili nione na kutambua kipaji changu.
Wiki moja baadae nikakutana naye Channel Ten na huo ndio ukawa mwanzo wa mimi kuwa mtangazaji katika vipindi vya burudani. Nakumbuka kipindi nilichoanza nacho ni Music Express. Wakati huo kilikuwa kinaitwa Muziki Motomoto. Hiki ni kipindi ambacho naendelea kukifanya mpaka leo. Kwa hesabu za haraka haraka utagundua kwamba nina uzoefu sasa wa miaka zaidi ya 11.
Pia katika kipindi chote hiki nimeshafanya vipindi vingine vingi kama vile Face To Face ambacho kilikuwa kinahusu masuala ya jamii. Kwa bahati mbaya kipindi hiki hakipo tena. Bahati nasibu zote pale Channel Ten huwa nafanya mimi. Nafanya Up Coming na vipindi vya urembo kama vile Red Carpet Interviews wakati wa mashindao ya Miss Tanzania au matukio mengine makubwa kama vile Kili Music Awards bila kusahau matamasha makubwa ya wasanii na promotions zake.
Pia mimi ni news reporter huku nikiendelea kuwa Producer wa kipindi change cha Music Express kinachoruka kila siku pale Channel Ten kuanzia saa mbili kamili mpaka saa mbili na nusu [8:00pm-8:30pm]. Ni kipindi cha nusu saa. Na kila Ijumaa tunakuwa na Friday Special ambapo tunakuwa na msanii studio na kufanya naye mahojiano.
Lakini pia miaka miwili baada ya kujiunga na Channel Ten na kupata uzoefu wa masuala ya utayarishaji wa vipindi na utangazaji kwa upande wa televisheni nilijiunga na Radio Magic Fm ambayo ipo chini ya AMGL ambayo ni kampuni mama inayomiliki pia Channel Ten. Na hii ilifuatia ushawishi wa huyo huyo Tramontano.
Pale Magic FM nilianza na kipindi cha “Girls Power” ambacho kwa sasa nimekibadili na kinaitwa “Mwanamke Leo”. Nikiangalia nyuma nagundua kwamba Girls Power ingawa halikuwa wazo baya, nadhani lilikuwa la kitoto zaidi. Kwenye Girls Power tulikuwa tunaangalia namna wasichana wanavyoishi na changamoto zinazowakabili kila siku. Baadae nikaona ni vizuri zaidi kuangalia mwanamke in general na changamoto zinazomkabili tangu akiwa mdogo mpaka anapokuwa mtu mzima na hata uzeeni. Ndipo tukaona jina liwe Mwanamke Leo.
MWANAMKE LEO ni kipindi cha mara moja kwa wiki. Kinaruka siku ya Jumamosi kuanzia saa nne mpaka sita asubuhi. Pia nina Daily Show kama ilivyo kwenye TV na pia naendesha kipindi kingine cha Radio kinaitwa AFRIKA KABISA ambacho ni kipindi chenye mahadhi ya kiafrika pekee. Hiki ni kipindi cha masaa mawili kuanzia Saa Kumi na Mbili Jioni mpaka Saa Mbili Usiku kila siku.
Kumalizia ni mwaka sasa tangu nianzishe website ya www.salmamsangi.com kwa kushirikiana na mdogo wangu Mudy anayeishi Ujerumani. Yeye ndio Web-Master. Hili lilikuwa wazo lake. Aliona wakati umefika niwe na site yangu ambapo kutakuwa na mambo yanayonihusu mimi binafsi[ kwa maana ya shughuli zangu nk] na pia mengine yanayojiri ulimwenguni.
Huyo Ndio Salma Msangi na mambo lukuki anayoyafanya mpaka leo.
BC: Kila mtu huwa ana mikasa yake ya utotoni. Wewe unapokumbuka utotoni, ni mkasa gani ambao huwa unakujia kichwani mara moja?
Salma: Utundu mwingi sana. Nakumbuka jinsi nilivyokuwa namsumbua mama yangu mkubwa kwa kushinda juu ya miti kukimbia fimbo baada ya kufanya tukio. Pia nakumbuka majina ya utani niliyokuwa nimepewa kwa sababu ya umaarufu au muonekano wangu. Majina kama MACHO kwa sababu ya kuwa na mijicho mikubwa na enzi za utotoni nilikuwa nayatoa haswaa.
Jina lingine nikaitwa KISEBENGO…sikumbuki chanzo kamili cha jina hilo ila baadae ukubwani nilipotafuta maana nikahisi labda jina lilitokana na wimbo wa zamani wa bendi fulani…Orchestre Maquis Original kama sikosei. Labda walinipachika jina kutokana na kuwa muongeaji sana.
Nikaitwa KIBERENGE kwa sababu nilikuwa na kelele sana…si unafahamu viberenge vilivyo na kelele? Aahahah. Pia nina jina la MSISIRI. Hili ni jina au neno la kipare linalomaanisha mwembamba. Bila shaka hili lilitokana na umbile langu la uembamba. Hayo majina hata leo hii ukifika kwetu usishangae ukasikia mtu kaniita hivyo….
BC: Kama taifa kwenye masuala ya urembo/ ulimbwende bado hatujafikia yale matawi ya juu kabisa kama ambavyo kila mtanzania angetamani. Unadhani kama kina Uncle Hashim Lundenga wangekwambia wanaomba ushauri wako ungewaambia nini?
Salma: Tanzania ina wasichana warembo wengi sana kimtazamo ila ndani yake IQ ni ndogo sana na huku tukiamini kingereza ndio kila kitu.
Ushauri wangu wasichana waandaliwe mapema…hata miaka mitatu au minne kabla. Kuwe na chuo au namna yeyote ya kuandaa wasichana hao kutokana na vigezo vinavyohitajika huko duniani. Msichana azoee watu, ajue vitu, aweze kujifunza vitu vingi vingi, awe mchangamfu na mwenye ujasiri na mwenye kujiamini na kuwa na uthubutu. Kutokana na jinsi ambavyo nimekuwa nikifuatilia washindi wa taji la Miss World, mashindano yale ni zaidi ya urembo wa kimtazamo.
Sasa unapomtoa msichana chuo kikuu au mtaani tu bila hata kuwa na uhakika wa background yake akiwa hana kingine chochote anachokijua zaidi ya maisha yake na ya familia yake na labda masomo[kama ni mwanafunzi] kwenda kushindana inakuwa ngumu. Pia kuna haja ya kuangalia mfumo wetu wa malezi mpaka mfumo wa elimu. Hatuna utamaduni wa kujifunza na kutaka kujua mambo mengi ya duniani. Ukienda kule unakuta wenzetu wanakujua wewe na nchi yako kuliko wewe unavyoijua. Hapo kuna ushindi kweli?
Tumezubaa tukifika tunabaki kushangaa kila kitu. Kila kitu kwetu kipya. Kwa mtindo huu kwa kweli hatuwezi kushinda kamwe. Na lile tatizo la kukariri kwamba kutokana na umri unaohitajika basi mrembo awe ametoka shule au ametoka mtaani tu hana analolifanya [ili mradi ana urembo wa kimtazamo tu] na anajua kiingereza tuache.
Angalia kwa mfano mrembo anayeshikilia taji la Miss World kwa sasa kutoka Phillipines[ Miss Megan Young]…yaani ameshafanya mambo kibao. Ana uzoefu wa kutosha katika mambo mbalimbali. Keshakuwa mcheza filamu, mtangazaji sijui mshindi wa taji gani tena huko kwao nk. Sasa unaona mtu kama huyu ukimpambanisha katika masuala hayo tayari anakuwa mbele. Ana uzoefu ni mjanja. Akili inakuwa imechangamka.
Waangalie wapo warembo wengine sio lazima awe fresh from home. Anaweza kuwa anajishughulisha na mambo mengi ila kwa sababu ana vigezo wamchukue…kama wanashindwa kuwaandaa na kuwatengeneza kama vile wanavyofanya nchi kama Brazil. Wanawaandaa kwa miaka hata mitano. Sasa sisi tunamuandaa mtu kwa miezi kadhaa au mwaka kumuandaa mtu mshamba kabisa hana alijualo atajua nini ataweza nini??? Urembo ni zaidi ya mtazamo wa nje. Kuna mambo mengi.
You need to a flashplayer enabled browser to view this YouTube video
BC: Ni mambo gani ambayo unayapenda zaidi kuhusu kazi yako na yapi ambayo huyapendi?Salma: Napenda kazi yangu kwasababu kila siku inanipa fursa ya kuzungumza na jamii yangu kwa kiasi kikubwa sana kwa wakati mmoja kupitia Radio Au Tv. Kwa hiyo kama nina ka kero kangu kwa jamii, serikali au taifa nk napenyeza hapo hapo. Zaidi nipo kwenye ulimwengu wa utandawazi kabisa kwa sababu kazi yangu inanifanya niwe mpekuzi wa mambo mengi duniani kupitia mitandao nk. Kwa hiyo najikuta nipo darasani kila siku kwa sababu nakutana na mambo mapya na kujifunza mambo mapya.
Ninachokichukia kwa kweli ni aina ya watu wanaonihusu katika kazi yangu; wasanii hasa wa muziki maana ndicho ninachokifanya zaidi. Wana matatizo makubwa ya kutokuzingatia muda. Hawa-keep time kabisa. Yaani kama hawapo serious. Utakuta unamwambia msanii interview saa nne asubuhi anakuja saa saba. Unamwambia saa moja jioni Live anakuja saa mbili.
Sisi kazi zetu kila sekunde ina maana. Muda ndio kitu cha kwanza. Sasa wao hawajali. Hawajui tunaposema ni Live show au sijui ni dharau kwa sababu anahisi wewe ndio unamuhitaji au sijui ni nini. Hawa wasanii wakubwa wakati wanaanza wanakuja kubembeleza kazi zao zichezwe. Hata ukimwambia aje saa kumi alfajiri atakuja. Lakini wakishafanikiwa labda ni kutokuwa makini na nidhamu kwenye kazi au ni dharau tu. How come unajulishwa kuwa mgeni studio wiki kabla au hata mbili kisha unaendelea kukumbushwa kadiri siku zinavyosogea kisha siku ya tukio unachelewa tena sio sekunde masaa kadhaa?
Wasanii wetu hawana ratiba ni wazee wa kukurupuka hakawii akakuambia nilikua sehemu nyingine! Je ulipokubali kuja kwangu same time same day ni kwamba ulikuwa usingizini au? Yani huwa na kerwa sana na tabia ya wasanii kuwa nyuma ya wakati hasa katika kazi yangu.
Salma na Ben Pol
BC: Wow! Mbali na hilo la kutozingatia muda [kitu ambacho ni sumu
ya maendeleo], nikikuomba utoe ushauri kwao kutokana na mtizamo wako
unaotokana na jinsi ambavyo umekuwa ukiwasoma kila mnapokutana ungetoa
ushauri gani?Salma: Wafanye kazi waache kulalamika. Wawe serious. Wajue wanachokitaka na wanachokifanya. Waache ulimbukeni wa umaarufu bali wafanye kazi kutimiza ndoto zao. Wasijione maarufu bali waache washabiki wawaone maarufu.
Wapate muda wa kupumzika. Waache matumizi ya pombe na mihadarati maana wasanii wengi wa bongo wanaamini kunywa pombe kuvuta masigara mabangi kuzunguka ma club usiku kila siku ndio usanii. Watafute maarifa [knowledge] zaidi ili wawe na ufahamu zaidi ili wawe na uwezo wa kutokeza kimataifa. Wajiamini na waache kunyenyekea baadhi ya watu wanaoamini ndio wanauwezo wa kuwafikisha pale walipo.Wajitambue watambue kazi zao ili wasinyonywe, japo wanasema muziki wa bongo ni fitna ila naamini mashabiki wanajua kizuri na kibaya.
BC: Utangazaji wako hukupeleka mpaka kuwa “mwanaharakati” wa masuala ya haki za wanawake. Unapotizama Tanzania ya leo na juhudi zake za kumkomboa au kumuendeleza mtoto wa kike, ni yapi mazuri ambayo yamekuwa yakitokea katika miaka 5 iliyopita na ungependekeza nini kifanyike katika miaka 5 ijayo?
Salma: Kwanza namshukuru sana Rais wetu Mh.Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa kweli katika awamu yake ya uongozi amewapa sana nafasi wanawake hususani katika nyanja za juu. Wanawake tupo tunasikika, tuna sauti na tunasikilizwa sasa. Tumeanza kutambulika na kuheshimika.
Kazi iliyobaki ni sisi wanawake wenyewe kwa wenyewe sasa tuliopata nafasi hizo kuzitumia ili kukabiliana na changamoto nyingi zinazoikuta jamii ya wanawake wa Tanzania.Tujipendelee sasa maana tumeshapewa nafasi tusipozitumia vizuri hatuna wa kumlaumu. Ila si haba naona wanawake viongozi wanakazana hasa kupigania haki za wanawake hapa nyumbani.
Kwa kiasi kikubwa naweza sema tumepiga hatua changamoto zaidi ni vijijini ila kupitia Mfuko Wa WAMA Uliopo chini ya mwenyekiti First Lady wetu,Mama Salma Kikwetwe umefanya kazi kubwa sana katika kipindi cha miaka 5 mpaka sasa.
Matatizo ya Uzazi, vifo vya uzazi, Festula, maambukizi ya virusi vya ukimwi toka kwa mama kwenda kwa mtoto yanaanza kudhibitiwa. Ugojwa Wa Festula ambao umekua ukijitokeza kwa wakina mama wakati wa kujifungua ni moja kati ya mambo yaliyotiliwa mkazo na kweli kuna mafanikio makubwa. Takwimu mpya zinaonyesha kupungua kabisa kwa matatizo hayo. Hayo ni mafanikio,
Lakini matatizo kama ya unyanyasaji wa kijinsia, kutomiliki mali, kupigwa, kubakwa, kuzalishwa mimba za utotoni, kukimbiwa na kulea familia, kufanywa watumwa wa ngono, ukeketwaji, nyumba ntobu, elimu na mengineyo ni changamoto ambazo zinahitaji kutiliwa mkazo zaidi katika kipindi cha miaka 5 ijayo hasa kwa vijijini. Mjini angalau elimu imefika na kwa kiasi watu wanaelewa na wanawake wenyewe wameanza kujitambua na kujilinda.
Salma na Shilole.
BC: Hivi sasa kuna waandishi huru wa habari. Kuna watumiaji wa
mitandao ya kijamii na kuna bloggers. Unaonaje mwelekeo wetu katika
kutumia nyenzo hizo katika kukabiliana na maadui zetu wa siku zote kama
ujinga, maradhi na umasikini?Salma : Utandawazi ni mzuri kama tukiutumia vizuri kwa manufaa kama elimu, biashara, mawasiliano sahhi nk. Kwa nchi yetu pamoja na faida chache lakini madhara ni makubwa. Watu hawatumii mitandao ya kijamii kwa ajili ya manufaa na maendeleo yao bali kwa ajili ya uharibifu.
Tunadhihirisha maradhi yetu mitandaoni. Mambo yanayoendelea ni ya kijinga tu naweza sema. Hayana faida yeyote kupoteza muda tu na mwisho wa siku tuna baki pale pale kwenye ujinga na umasikini. Maana watu hawafanyi kazi tena wanashinda mitandaoni wakiangalia vitu vya kijinga umbea nani kafanya nini, nani katoka na nani nani kamuibia nani bwana au bibi nk. Hata huko maofisini watu hawafanyi tena kazi wapo busy na umbea mitandaoni hivyo tutegemee umasikini zaidi kwa maana tunatumia ujinga mitandaoni.
Blogger nao ili kuapa View na Visitor wengi njia rahisi ni kutafuta story za uongo zenye kudhalilisha dada zetu na ndio watu wanavyopenda. Mimi nina website, nikiweka story ya mafuriko yameikumba sehemu fulani ya Tanzania haitasomwa kama ntakavyoweka ya fulani kafumaniwa na fulani sasa hapo huoni ni tatizo? Kwa kweli tuna matumizi mabaya ya mitandao jambo ambalo linazidi kutukandamiza. Sasa kila mtu ni muandishi bila maadili ya uandishi iliyobaki ni kuchafuana ka kuharibiana na kuwekana hadharani hii si sawa. Tubadilike.
Salma na Lady JayDee
BC: Mamilioni ya vijana nchini hawana ajira. Wengi wamekata tamaa
na hata kujiingiza kwenye aidha matumizi ya madawa ya kulevya au wao
wenyewe kutumika kama wasafirishaji wa madawa hayo. Ushauri au wito wako
kwa vijana na vyombo husika ni upi?Salma: Kwanza tusikate tama. Pili tusitake maisha ya haraka haraka na tufahamu mafanikio hayaji kama ndoto kwamba ulale uamke umefanikiwa. Pigana,hangaika kwa elimu uliyonayo au hata kama hukujaaliwa sio kila aliyefanikiwa ana elimu japo elimu hurahisisha.
Tusisubiri ajira tuwe na ubunifu wa kujiajiri. Tutumie kila fursa iliyo mbele yetu hata kama ni ya kuingiza mia au kupata tu exposure. Uvumilivu, subra na kuridhika na kidogo huku ukiendelelea kufanyia kazi ndoto zako. Hakuna kinachoshindikana.
Kwa serikali iandae mifumo ya elimu kuanzia ngazi za chini itakayomfanya mwanafunzi awe na njia na uwezo wa kujitegemea bila kutegemea ajira mara baada ya masomo yake. Pia serikali ilegeze baadhi ya sheria kwa wafanya biashara wadogo wadogo ili waweze kijikwamua. Mabenki nayo yawaangalie vijana. Yawape mikopo nafuu kwa masharti nafuu ili waweze kufanya shughuli zao za kuwaingizia kipato halali.
Wazazi tuwakuze watoto katika maadili ya kujitahidi, kusoma, kufanya kazi ,kutojibweteka. Wawafundishe watoto maadili mema ili wawe na imani na subra wakiwa na hofu ya Mungu hawatafanya mabaya ila watakaa kwenye mstari. Maana kila jambo huanzia kwenye malezi. Tumemsahau Mungu turejee maadili ya dini yatatujenga na kutuendeleza.
Vijana wasiamini mijini ndio kila kitu. Kilimo ni utajiri na uti wa mgongo wa taifa. Wawezeshwe vijijini ili wakiwa huko huko waweze kuendesha maisha yao hapatakuwa na vugu vugu hili la vijana kujiingiza katika mihadarati kwa namna yeyote ile.
BC: Inajulikana kwamba wewe ni miongoni mwa watu wenye ushawishi na umaarufu katika jamii na ambao wapo ndani ya ndoa. Ukichanganya kazi yako,nyumba,familia nk unawekaje yote sawa?
Salma: Naweza. Ndoa sio kifungo. Ni makubaliano baina ya watu wawili. Ndoa haina formula kwamba lazima uwe hivi au vile. Kikubwa ni kujiheshimu maana suala la kujiheshimu si tu mpaka uwe kwenye ndoa. Kwa ujumla mwanadamu unatakiwa ujiheshimu na uwe mwaminifu kwa maamuzi uliyoamua. Ndoa ni mapenzi ya mkataba baina ya watu wawili waliopendana. Sasa kama unajua hutaweza kuwa muaminifu basi kwanini ukubali mkataba huo?
Ndoa kwangu ni vile ninavyoishi na mwenzangu.Tunapendana, tunaelewana, tunaheshimiana, tunaaminiana na tunavumiliana. Kila mmoja anakubali anachokifanya mwenzie bila kwenda kinyume na matakwa yetu wawili. Ndivyo ndoa yangu ilivyo. Mimi ni Salma Msangi kwenye kazi yangu vile utakavyoipokea.
Baada ya kazi mimi ni mke, mama wa familia ninayetambua majukumu yangu. Sina watoto kwa sasa wa kuwazaa lakini nina watoto wa kuwalea, wadogo zangu ambao mimi najivika kilemba cha ulezi. Watoto hawa wanahitaji malezi na makuzi mazuri na mimi kwao kama mfano kwao. Sasa kama nitaenda kinyume sitakua mzazi mlezi mwema. Wazazi wangu walinilea vizuri na kuniamini kunipa wadogo zangu kutokana na kuamini kutokana na malezi yao. Sitaki kuwaangusha wazazi wangu.
Mimi kama mwanamke niliyeolewa na mfanya kazi, ninayajua na kuyafahamu majukumu yangu. Najua kutofautisha muda wa kazi, muda wa familia, muda wa marafiki, muda wa jamii nk. Na ninapata muda wa kupumzika pia.
Kila kitu ni kuamua kutoka rohoni. Mtazamo wa mtu wa nje sio wa kum-judge. Maisha ni namna unavyoishi ili mradi usivunje sheria. Kuwa na mfumo wako na sio kwa sababu ya watu. Jifurahishe. Fanya unachokipenda maana maisha aliyoishi baba yako na mama yako sio yako au ya leo. Au maisha ya rafiki yako na mkewe au mumewe sio yako. Kila mtu ana utaratibu wake. Msiitafsiri ndoa vibaya.
BC: Inajulikana kwamba bado unajishughulisha na masuala ya urembo nk. Ni wabunifu gani wa mitindo unaofurahia au kuzipenda kazi zao zaidi? Unaweza kunitajia wa nyumbani Tanzania au nje ya Tanzania.
Salma: Samahani lakini kwa Tanazania sioni jipya. Siku zote nasema Tanzania hakuna wabunifu, kuna washona nguo. Imezoeleka mafundi cherehani japo si watengeneza cherehani mie nitawaita washona nguo. Katika suala la kubuni hapa hapo watanisamehe tuna safari ndefu.
Tunahitaji ubunifu zaidi na si kuchukua catalog za nje tunashona kisha models wanapita Runway tunasema ni ubunifu wa Tanzania. Nje ni wengi na wanajieleza kikubwa tuige mifano yao ila tubaki kwenye tamaduni zetu.
BC: Kama mwanamke,ni vitu gani ambavyo siwezi au sitakiwi kuvikosa kwenye pochi yako kila siku?
Salma: Imenibidi nichungulie pochi yangu angalau nione kilichopo hahaha….. Mwanamke hatakiwi kukosa, Kitambaa, kipande cha kanga au kitenge au japo mtandio, Anti Bacteria Wet Tissue, Body Spray,HandLotion, kioo, lip bum or lip shine, Pafyum, kitana,Ped, Pesa kidogo, simu of course,diary,Pen, mouth Spray au Chewing gum nadhani hivyo ni vya muhimu vingine ni ziada tu.
BC: Shukrani sana kwa muda wako Salma. Kila la kheri katika kazi zako,familia na mengineyo.
Salma: Asante sana Jeff. You are doing great Bro!
Unaweza kuungana na BongoCelebrity na Salma Msangi katika mitandao hii kwa kufuata au kutafuta [search] Salma Msangi au BongoCelebrity
No comments:
Post a Comment