Waziri
wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amelihakikishia Shirika La Umoja wa Mataifa
la Kuhudumia Watoto (The United Nations Children's Emergency
Fund-UNICEF) kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na shirika hilo
katika harakati zake za kuboresha ustawi, kutetea na kulinda haki za
watoto duniani.
Aliyasema
hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha mwaka cha
Menejimenti ya Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika cha Shirika hilo
kilichoanza tarehe 25 Aprili na kinahitimishwa leo kwenye Hoteli ya
Ramada.
Dkt.
Mahiga alisema kuwa UNICEF ni shirika kubwa linalojulikana duniani kwa
mchango wake katika ustawi wa nchi zinazoendelea, hususan katika
kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za kimsingi.
Waziri
Mahiga aliendelea kueleza kuwa katika kuhakikisha kuwa watoto
wanapatiwa haki zao ipasavyo, hakuna budi UNICEF ikashirikiana na
Serikali husika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma
harakati hizo. Alizitaja changamoto kubwa kwa ustawi wa watoto ni
pamoja na sera, mifumo ya kisheria, ufinyu wa bajeti na urasimu katika
taasisi za Serikali. “Tunakabiliwa na changamoto nyingi katika harakati
za kuimarisha ustawi, kutetea na kulinda haki za watoto ambazo ili
ziweze kutatuliwa kwa wepesi lazima Serikali, UNICEF na wadau wengine
tufanye kazi kwa pamoja”.
Waziri
wa Mambo ya Nje aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa kuna masuala
mengi yanayosababisha matatizo kwa watoto duniani ambayo yanatakiwa
yatafutiwe ufumbuzi kwa pamoja. Masuala hayo ni pamoja na usafirishaji
haramu wa watoto, biashara haramu ya dawa za kulevya, unyanyasaji dhidi
ya wanawake, machafuko ya kisiasa, kushindwa kuwawezesha wanawake na
kuwahudumia watoto. Alisema hayo na masuala mengine yanasababisha
changamoto kubwa kwa watoto.
Aidha,
Dkt. Mahiga alizungumzia changamoto zinazowakabili watoto wa Tanzania
ambazo ni pamoja na mauaji ya watoto, hususan wenye ualbino, kuongezeka
kwa watoto wa mitaani, kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watoto ambako
kunasababisha ukosefu wa ajira, ukatili dhidi ya watoto na ukandamizaji
wa haki nyingine za watoto.
Alishauri
UNICEF iwe na mikakati mahsusi ya kushughulikia changamoto
zinazoikabili nchi husika kwa kushirikiana na taasisi za nchi hiyo. Kwa
upande wa Tanzania, alisema kuwa inakabiliwa na changamoto ya mauaji ya
watu wenye ualbino na kuongezeka kwa mahitaji katika sekta ya elimu ili
kuboresha ubora wa elimu, kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kwa
sababu ya Serikali ya awamu ya tano kutangaza elimu ya awali hadi ya
sekondari bure.
Dkt.
Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa jambo kubwa
linalomsumbua ni kuhakikisha kuwa watoto katika kipindi cha ujauzito
hadi miaka mitano wanaishi bila kupoteza maisha kutokana na magonjwa na
ukosefu wa lishe bora pamoja na kuwalinda hususan katika maeneo ya
machafuko.
Ziara ya Waziri wa Nchi wa Viwanda na Biashara wa Singapore, Mhe Dkt. Koh Poh Kun nchini Tanzania tarehe 27 Aprili 2016.
Katika
hatua nyingine, Waziri wa Nchi wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe
Dkt. Koh Poh Kun amefanya ziara ya kikazi nchini tarehe 27 Aprili 2016.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Koh amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) mjini
Dodoma. Katika mazungumzo yao, Dkt. Koh amemhakikishia Mhe. Waziri Mkuu
kwamba makampuni ya Singapore yataendelea kufanya uwekezaji katika sekta
mbalimbali nchini.
Hadi
hivi sasa Makampuni ya Singapore yaliyokwishawekeza nchini ni pamoja na
Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni
1.2 katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani
Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant)
kitakachojengwa kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na Marekani.
Aidha, kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za
Kimarekani Milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa
makampuni ya gesi.
Dkt.
Koh pia alimfahamisha Mhe. Waziri Mkuu kwamba kampuni ya Hyflux ya
Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi
(Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha
miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda
vya kati (light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi
zipatazo 37,000. Jiwe la Msingi la Mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili
2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage
(Mb).
Mbali
na ushirikiano katika sekta ya Biashara na Uwekezaji, Dkt. Koh
amemfahamisha Mhe Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania
kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na
uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta. Alisema
Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda
kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia
uendeshaji wa bandari za Tanzania.
Vilevile,
Singapore imeahidi kuandaa mafunzo mahususi kwa ajili ya Makatibu Wakuu
wa Tanzania. Mafunzo hayo ya wiki moja yatatumika kubadilishana uzoefu
na makatibu wakuu wa Singapore pamoja na Mawaziri. Dkt. Koh alisema
Serikali ya Singapore inatoa kipaumbele cha juu katika kuwajengea ujuzi
watumishi wa umma kwasababu msingi wa mafanikio ya Taifa lao ni kuwa na
rasilimali watu walio na weledi,ujuzi,uzoefu na uadilifu.
Kwa
upande wake, Mhe Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Singapore kwa
uwekezaji unaofanywa na makampuni yake nchini na kwa misaada ya kiufundi
ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Ili
kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Mhe
Waziri Mkuu ameyakaribisha makampuni mengine ya Singapore kuja nchini
kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha
viwanda, hoteli, kilimo na nishati. Aidha, alimuahidi Dkt. Koh kwamba
Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia
na kulinda uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (Bilateral Investment
Protection and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru
mara mbili (Avoidance of Double Taxation Agreement) ili kuvutia
uwekezaji zaidi kati ya mataifa hayo mawili.
Kuhusu
fursa za mafunzo, Mhe Waziri Mkuu ameiomba Serikali ya Singapore itoe
fursa zaidi katika mafunzo ya wataalam wa sekta za gesi na uchukuzi.
Awali,
Dkt. Koh alifanya mazungumzo na: Mwenyeji wake Waziri wa Viwanda
Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb), Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa (Mb), Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb) na Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb).
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam, 28 Aprili, 2016
No comments:
Post a Comment