Maisha : Habibu Foundation yaadhimisha siku yao kwa kutoa misaada wilayani Mwanga - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


19 Apr 2016

Maisha : Habibu Foundation yaadhimisha siku yao kwa kutoa misaada wilayani Mwanga


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Green Bird Education Institute & Habibu Foundation, Juma Mndeme, mwenye miwani akizungumza jambo baada ya kumaliza kukabidhi misaada ya mabenchi ya kukalia, sabuni na vinywaji kwa Kituo cha afya Mwanga, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro. Aliyeshika majaketi ni Mganga Mkuu Msaidizi wa Kituo hicho Honest Temba na aliyeshika simu ni Meneja Uhusiano wa Habibu Foundation, Julysiza Mangiseni.

Na Mwandishi Wetu, Mwanga

MAADHIMISHO ya Siku Maalum ya Habibu Day wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro yamefanyika kwa mafanikio kwa kushirikisha matukio mbalimbali yakiwamo ya kutoa misaada katika kituo cha Afya Mwanga, kutoa misaada jeshi la Polisi, pamoja na kufanyika mijadala mbalimbali ya kielimu iliyoendeshwa na wanafunzi wa shule za sekondari wilayani humo.
Katika muda wa mijadala, wanafunzi hao walitumia muda mwingi kuzungumzia mfumo wa kielimu nchini Tanzania sanjari na upangaji wa matokeo ya mitihani kutoka Division na GPA iliyoondolewa rasmi katika mfumo huo nchini hapa, huku mgeni rasmi akiwa ni Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyata kilichopo Arusha, Profesa Ward Mavura.

Meneja Uhusiano wa Taasisi ya Elimu ya Green Bird Education Institute & Habibu Foundation, Julysiza Mangiseni, akizungumza jambo kwenye maadhimisho hayo yaliyoanzia kutoa zawadi mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa Habibu Foundation akizungumza
Mkuu wa Polisi wilayani Mwanga, Pili Mande akipokea sehemu ya zawadi kutoka kwenye Taasisi ya Elimu ya Green Bird
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Green Bird kilichopo wilayani Mwanga wakielekea kwenye Kituo cha Afya cha Mwanga kwa ajili ya kupeleka zawadi mbalimbali kama ishar ya kumuenzi muasisi wao marehemu mzee Habibu Mndeme. Picha zote na Mpiga Picha Wetu.Awali ratiba ilianza rasmi saa 12 asubuhi kwa wanafunzi wa shule za sekondari za Green Bird Girls, Green Bird Boys, Green Bird Collage zinazomilikiwa na taasisi ya Habibu Foundation kutembelea katika maeneo ya Ofisi ya polisi Mwanga na kituo cha afya Mwanga, pamoja na kutoa misaada kama vile mabechi ya kukalia wagonjwa, sabuni, vinywaji pamoja na vifaa ya ofisi kwa jeshi la Polisi Mwanga.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa wa Taasisi ya Elimu ya Green Bird Education Institute & Habibu Foundation,, Juma Habibu Mndeme, alisema kwamba lengo la kufanyika kwa maadhimisho hayo ni kukutanisha pamoja wadau wa elimu wilayani Mwanga sanjari na kumuenzi mwanzilishi wa taasisi yao marehemu Habibu Mndeme aliyefariki Dunia mwaka 2010) na kuacha taasisi hiyo inayomiliki pia shule wilayani Mwanga.

“Tumekuwa tukiadhimisha matukio haya kila mwaka lakini tunaendelea kuboresha hatua kwa hatua, maana lengo la taasisi ni kukuza kiwango cha elimu kwa wilaya ya Mwanga na Tanzania kwa ujumla, ndio maana mijadala ya kielimu ilihusisha wanafunzi mbalimbali kutoka ndani ya Mwanga na nje pia, ikiwamo jijini Arusha.

“Sisi kama waendeshaji wa shule zote za Green Bird tunajivunia kufanyika maadhimisho haya kwa mafanikio makubwa, bila kusahau ulinzi madhubuti kutoka kwenye jeshi la polisi kuanzia asubuhi hadi usiku, huku tukiona ushindani mkubwa, uzoefu na umakini kwa kila aliyeshiriki kuonyesha ujuzi na uwezo wake, hususan katika suala zima la kielimu,” Alisema Mndeme.

Naye Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Profesa Ward Mavura ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Jomokenyata cha jijini Arusha, aliitaka jamii ya wilaya Mwanga kuiunga mkono taasisi hiyo kwa ajili ya kuiweka katika mazingira mazuri katika utoaji wa huduma zake.

Akizungumzia tukio hilo na utoaji misaada kwenye jeshi la Polisi wilayani Mwanga, Mkuu wa Polisi Mwanga, Pili Mande, aliishukuru Taasisi ya Habibu kwa kuwekeza katika elimu na kuisaidia jamii kwa mambo mengi, jambo linalotakiwa kuungwa mkono na kuendelezwa kwa manufaa ya Mwanga na Tanzania kwa ujumla.

Naye Meneja Uhusiano wa wa Taasisi ya Elimu ya Green Bird Education Institute & Habibu Foundation,, Julysiza Mengiseni, alisema kwamba kufanyika kwa mafanikio kwa maadhimisho hayo ni hatua nzuri ya kuhakikisha dira ya kuifanya taasisi yao iwe kioo cha elimu wilayani Mwanga na Tanzania kwa ujumla.

“Taasisi inaendelea kutoa elimu bora kwa kuweka miundo mbinu mizuri katika shule zake za sekondari na chuo pia hapa wilayani Mwanga, ambapo kwa pamoja tunasonga mbele kutolkana na ushirikiano mkubwa tunaopata kutoka serikalini na kwa wananchi wote,” Alisema Julysiza.

Kwa mujibu wa Julysiza, elimu inayotolewa kwenye shule zinazomilikiwa na taasisi yao ni bora na imechangia katika uandaaji wa watoto kwa makundi mengi ya kielimu kama vile sekondari na chuo kinachofundisha biashara, elimu na afya.

Post Top Ad