Matukio : Taasisi za serikali za shauriwa kufuata miongozo na viwango katika matumizi ya TEHAMA - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


3 Mar 2016

Matukio : Taasisi za serikali za shauriwa kufuata miongozo na viwango katika matumizi ya TEHAMA

 Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa na taasisi za Serikali katika kuimarisha matumizi sahihi na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kuendesha mifumo ya Tehama Serikalini. Kushoto ni Mkurugenzi wa Usimizi wa Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wakala hiyo. 
 Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano huo.
 Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wakala hiyo Bw. Benedict Ndomba akifafanua kuhusu mpango wa Serikali wa kuimarisha mawasiliano katika mifumo ya TEHAMA Serikalini.

Na Beatrice Lyimo - Dar es Salaam
 
Wakala ya Serikali mtandao (e-Government Agency) imezishauri Taasisi zote za Umma ,Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekreterieti za Mikoa, Wakala na Mamlaka za Serikali ,Bodi, Tume, Mabaraza, Mifuko, Mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufuata miongozo na viwango vilivyotolewa Wakala hiyo katika uanzishaji na usimamizi wa mifumo ya Tehama Serikalini.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto alipokuwa akitoa maelekezo na ufafanuzi wa taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa na taasisi hizo kwa lengo la kuimarisha matumizi sahihi na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kuendesha mifumo ya Tehama Serikalini.

Bi. Mshakangoto amesema kuwa miongozo na viwango hivyo vinalenga kuziwezesha taasisi za umma kujenga mifumo inayoendana na mahitaji halisi ya taasisi husika na kuepuka mifumo inayojengwa kwa shinikizo la wafanyabiashara, wafadhili au kwa matakwa ya mtu binafsi.

“ Taasisi zote zikitumia miongozo ya viwango tuliyoweka, Serikali itakuwa na uwezo wa kuepuka urudufu wa mifumo na kupunguza gharama kubwa za uendeshaji kwa kuwa na mifumo endelevu yenye gharama halisi inayofuata viwango vya Usalama katika kulinda taarifa na data za Serikali”  Alifafanua Meneja huyo.

Amezishauri taasisi hizo kuwasilisha maandiko ya mifumo mipya ya TEHAMA na kujaza taarifa za mifumo au miradi ya TEHAMA iliyopo katika mfumo wa kukusanya na kutunza taarifa za miradi ya TEHAMA Serikali ili iweze kuthibitishwa iwapo imefuata miongozo na viwango vilivyowekwa kabla ya kujengwa na kusakinishwa.

Akitoa ufafanuzi kuhusu wafanyabiashara wanaojihusisha na miradi au utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA Serikalini amesema kuwa wanashauriwa kufuata miongozo na viwango hivi ili kujua mahitaji halisi ya Serikali na kuweza kujenga mifumo ya TEHAMA endelevu na inayoleta tija kwa umma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimizi wa Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wakala hiyo Bw. Benedict Ndomba ameeleza kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa mifumo yote ya TEHAMA ya Serikali inakuwa na mawasiliano na kubadilishana taarifa mbalimbali.

Amesema kuwa Serikali imekuwa ikiweka msisitizo wa matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kupata huduma za Serikali kwa gharama nafuu kwa njia ya Mtandao.

Wakala ya Serikali Mtandao (e-Government Agency) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2012 kwa sheria ya Wakala za Serikali Na. 30, Sura ya 245 ya mwaka 1997. Wakala hii ina majukumu na mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao nchini Tanzania.

Post Top Ad