Pichani : Mwenyekiti wa TBN, Bw. Beda Msimbe akizungumza kwenye Mkutano wa Ikulu.
Leo Desemba 9, tunapoadhimisha miaka 64 tangu Taifa letu lipate Uhuru, Tanzania Bloggers Network (TBN) inawapongeza Watanzania wote kwa kufikia hatua hii muhimu katika historia ya Taifa letu. Hii ni siku ya kutafakari safari tuliyotoka, mahali tulipo, na mwelekeo tunaoujenga kwa pamoja.
Waasisi wetu walituwachia zawadi kubwa—Uhuru. Lakini walituonya kuwa Uhuru hauwezi kuwa kamili bila kujitegemea. Leo tunakumbusha maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusisitiza:
"Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi."
Tujenge Taifa Letu – Tusiibomoe Tanzania
Kama mtandao wa habari za kidijitali, TBN inasisitiza kuwa mafanikio yetu kama Taifa yametokana na utulivu, umoja na mshikamano. Ili kuendelea mbele, tunahitaji kudumisha amani na maridhiano—nguzo muhimu za maendeleo.
Rais mstaafu Benjamin William Mkapa alituasa kwa busara:
"Amani si kitu cha asili; tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila amani, hakuna maendeleo ya kweli."
Tukikubali kuongozwa na chuki, uchochezi na vurugu, juhudi za waasisi wetu za kupambana na ujinga, umaskini na maradhi zitapotea. Tusiitumie mitandao au uhuru wa maoni kuharibu Taifa letu; tuitumie kulijenga.
Kila Zama na Kiongozi Wake – Tuunge Mkono Mageuzi
Kila kizazi kina wajibu wake. Kama alivyoeleza Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi:
"Kila utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa hili."
Katika awamu ya sasa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaendelea na mwelekeo wa 4R: Reconciliation, Resilience, Reforms, and Rebuilding. Huu ni mwaliko kwa Watanzania wote kushiriki katika kujenga Taifa lenye maridhiano, mageuzi chanya na uimara wa kiuchumi na kijamii.
Tuna nafasi ya kuzungumza—basi tuseme kwa njia inayojenga, si inayobomoa. Kuthamini Uhuru ni kufanya kazi kwa bidii, kulinda amani, na kuacha kutumiwa kuharibu misingi ya Taifa letu.
TBN Inawatakia Maadhimisho Mema ya Miaka 64 ya Uhuru!
Tanzania Kwanza — Kazi, Utu na Mshikamano. Tusonge Mbele!
Beda Msimbe
Mwenyekiti, Tanzania Bloggers Network (TBN)

No comments:
Post a Comment