Mkuu
wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki akizungumza na wajumbe wa
Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es salaam kwenye kikao cha kwanza cha
Bodi hiyo kwa mwaka 2016. Kulia ni Zungu Azzan na Kushoto ni Bw. Edward
Otieno Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo.
Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala Bw.Isaya Mngurumi akichangia jambo kuhusu
uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Manispaa yake wakati wa
Kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dar es salaam.
Mkuu
wa Wilaya ya Temeke Sophia Mjema akichangia jambo wakati wa wakati wa
Kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dar es salaam kwa mwaka
2016.
Baadhi
ya Wabunge wa jiji Dar es salaam wakifuatilia kikao cha Bodi ya
Barabara Mkoa wa Dar es salaam. Kutoka kulia ni Mhe. Bonnah Kalua -
Mbunge wa Segerea, Mhe. Faustine Ndugulile - Mbunge wa Kigamboni, Mhe.
Zungu Azzan – Mbunge wa Ilala na Mhe. Abdallah Mtolea – Mbunge wa
Temeke.
Meneja
wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam Muhandisi Julius Ndyamkama
akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara mkoa wa Dar
es salaam kuhusu miradi ya ujenzi wa Barabara inayosimamiwa na Wakala
hiyo.
Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Mkuu
wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki amepiga marufuku utoaji wa
vibali vya malori ya mizigo na magari yenye uzito wa zaidi ya tani 10
kuingia katika barabara zote zinazosimamiwa na Manispaa za jiji la Dar
es salaam zilizojengwa kwa kiwango cha lami kufuatia barabara hizo
kuharibika kwa kipindi kifupi kutokana uzito jambo linaloisababishia
Serikali hasara.
Aidha,
ameziagiza manispaa za jiji hilo kuweka alama za barabarani zinaonyesha
zuio kwa magari yote yenye uzito wa zaidi ya tani 10 kupita kwenye
barabara hizo ili wamiliki na madereva watakaokiuka agizo hilo
wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Akizungumza
na wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es salaam kwenye kikao
cha kwanza kwa mwaka 2016 Mhe. Sadiki Meck Sadiki amesema kuwa Manispaa
za jiji hilo zinatenga fedha nyingi za kujenga barabara mpya na kufanya
matengenezo ya zile zilizopo ambazo nyingi zinaharibiwa na malori ya
mizigo.
Amefafanua
kuwa matumizi hayo mabaya ya barabara kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na
ukiukwaji wa sheria za barabarani ambapo malori makubwa ya mizigo
huegesha na kuziba maeneo ya waenda kwa miguu jambo linalowanyima haki
wananchi kutumia maeneo yaiyotengwa kwa ajili yao.
Amesema
baadhi ya magari yenye uzito wa tani 40 hudiriki kupita kwenye barabara
za huduma (Service road), madaraja na wakati mwingine maeneo ya waenda
kwa miguu jambo linalosababisha uvunjaji wa kingo za barabara na
milingoti ya taa za barabarani na kuongeza kuwa vitendo hivyo
vinaisababishia Serikali hasara kutokana na gharama ya matengenezo.
“Kuanzia
leo katika mkoa wangu ni marufuku kutoa vibali vya magari yenye uzito
wa zaidi ya tani 10 kuingia kwenye barabara zetu, tunataka barabara zetu
zidumu, hatuwezi kuvumilia vitendo vya watu wachache wanaokiuka sheria
za barabarani kuharibu barabara zetu, lazima tuchukue hatua Manispaa
zinajitahidi kujenga bararaba lakini hazidumu” Amesisitiza Mhe. Sadiki.
Amesema
barabara zinazosimamiwa na Manispaa za Dar es salaam zina uwezo wa
kuhimili uzito wa tani 10 na kubainisha kuwa kwa kipindi kirefu malori
ya tani 40 yamekuwa yakipita kwenye barabara hizo na kuzifanya manispaa
kunajenga barabara hizo kila mwaka.
Mhe.
Sadiki amesema kuwa ipo haja ya mamlaka zinazohusika na miundombinu ya
barabara katika jjiji la Dar es salaam kwa kuwatumia wataalam wa sheria
kuanza kuangalia uwezekano wa wamiliki wa vyombo vinavyosababisha
uharibifu wa miundombinu ya barabara kulipa gharama za uharibifu huo.
Kuhusu
ulinzi na Usalama watumiaji wa barabara za jiji amelitaka Jeshi la
Polisi kuendelea kuchukua hatua na kufanya Operesheni dhidi ya madereva
wa pikipiki (Bodaboda) na Bajaji wanaopitisha vyombo vyao vya usafiri
kwenye njia za waenda kwa miguu na kusababisha usumbufu na ajali za mara
kwa mara kwa wananchi wanaotumia njia hizo.
Pia
amezitaka Manispaa za jiji hilo kushirikiana na Wakala wa Barabara
(TANROADS) mkoa wa Dar es salaam kusimamia maeneo yote yanayotakiwa
kujengwa miundombinu ya Barabara ili yasivamiwe na wananchi pamoja na
kuwachukulia hatua wananchi wanaofanya biashara katika maeneo
yasiyoruhusiwa ya hifadhi za barabara na njia za waenda kwa miguu.
‘‘Ninaiagiza
manispaa ya Kinondoni kuondoa wafanyabishara wote walioko eneo la kituo
cha kuzalishia umeme Ubungo, eneo lile ni hatari kwa usalama na maisha
yao, kukaa pale ni kinyume cha sheria’’ Amesisitiza.
Aidha,
amesema mwaka 2016 mkoa wa Dar es salaam umetenga jumla ya Shilingi
bilioni 343.5 ikilinganishwa na shilingi Biliobi 266.6 zilizotengwa
mwaka mwaka 2015/2016 kutekeleza ujenzi na matengenezo ya barabara
katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo lengo likiwa kupunguza msongamano
wa magari.
Kuhusu
Kikao hicho cha kwanza cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es salaam
kwa mwaka 2016 amesema pamoja mambo mengine kimepokea na kujadili
tarrifa utekelezwaji wa ujenzi wa miradi ya barabara kwa mwaka
2015/2016 pamoja na kupokea Mpango wa matengenezo ya barabara kwa mwaka
2016/2017.
Ametoa
wito kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam kuzingatia usafi wa mazingira
kwa kulinda miundombinu ya barabara na kuepuka kutupa taka kwenye
mifereji ya kupitisha maji ili kuzuia mlipuko wa magonjwa ukiwemo
ugonjwa wa Kipindupindu.
No comments:
Post a Comment