Ndugu
zangu, Kwa niaba ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia kwenu
wanahabari ninaomba nitoe salam za mwaka za Shirikisho la mpira wa miguu
Tanzania TFF.
Awali
ya yote tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametulinda kwa mwaka mzima na
kupitia Baraka zake tumeweza kuwa na nguvu, uwezo na hekima za kutimiza
majukumu yetu mbalimbali katika kipindi hiki cha mwaka 2015. Tuzidi
kumuomba atuvushe salama mwaka 2015.
Ninaomba
nichukue fursa hii kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa kukamilisha
mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Ninampongeza Mh. Dr John Pombe
Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hongera sana Mama Samia Suluhu kwa kuwa Makamu wa Rais na hongera kwa
mwanamichezo mwenzetu Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kushinda
ubunge jimbo la Ruangwa na kwa uteuzi wa kuwa Waziri wetu Mkuu.
Hongera
za kipekee kwa Mheshimiwa Nape Nnauye kwa uteuzi wa kuwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na hongera pia kwa Mama Anastasia
Wambura kwa kuteuliwa kuwa naibu waziri wa wizara hii muhimu kwa
mustakabali wa afya na ajira kwa vijana na utangazaji wa jina la Nchi
yetu ya Tanzania nje ya mipaka ya nchi. Ninashukuru Mh. Waziri Nnauye
majuzi alinipatia fursa ya kuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa vyama vya
Kitaifa vya michezo ya kukutana naye na kujitambulisha rasmi kwake,
ahsante sana.
Ndugu
zangu, Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania lipo kwa ajili ya
kuendeleza na kusimamia mpira wa miguu Tanzania. Tunafanya hivyo kwa
niaba ya Watanzania wote wapenzi wa mpira wa miguu. Kwa kutambua uzito
na umuhimu wa jukumu hili ndio maana wakati wote TFF inafanya jitihada
za dhati kuhakikisha timu zetu za Taifa zinafanya vizuri.
Kwa
sasa tunazo timu za Taifa kumi ambazo ni za soka la ufukweni wanawake na
wanaume, umri chini ya miaka 17 wanawake na wanaume, umri chini ya
miaka 20 wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 23 wanawake na wanaume
na mbili za wakubwa za wanawake na wanaume. Katika kuingiza timu kwenye
mashindano ya kimataifa tumekuwa tukizingatia vigezo kadhaa lakini
kikubwa ikiwa ni utayari wa timu kushiriki mashindano na uwezo wa
kugharamia mchezo wenyewe.
Kwa
wastani gharama za kushiriki mkondo mmoja wa mechi ya Kimataifa kwa
kucheza nyumbani na ugenini ni takribani shilingi million mia moja (USD
50,000.-), hii inajumuisha gharama za kambi, usafiri kwenda ugenini,
posho, nauli na posho za waamuzi na kamisaa, malazi ya waamuzi na
kamisaa nk. Kwa kuwa timu yenye udhamini kwa sasa ni timu ya Taifa
wanaume tuu hivyo TFF imekuwa inabeba yenyewe gharama nyingine zote kwa
timu zote zilizobakia. Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utashuhudia
ufadhili unapatikana kwa timu zetu nyingine za Taifa.
Ninaomba sasa nichukue fursa hii kuzungumzia maeneo kadhaa ambayo yamehusu mpira wetu na taasisi yetu kwa mwaka 2015:
1. Timu ya Taifa ya wanaume “Taifa Stars”
Baada
ya timu yetu ya Taifa, Taifa Stars kutofanya vizuri katika michuano ya
COSAFA huko Afrika Kusini mwezi Mei mwaka huu na baadae kufuatia kufanya
vibaya katika mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano ya CHAN,
Kamati ya Utendaji ya TFF ilichukua maamuzi ya kusimamisha ajira ya
kocha wa kigeni Martin Nooj na badala yake kuingia mkataba na makocha
wazawa Boniface Charles Mkwasa akisaidiana na Hemed Morocco.
Tangu
walimu hawa wamechukua timu ya Taifa Stars tumefungwa mechi mbili tuu za
mashindano dhidi ya Algeria na Malawi ugenini, tumetoka sare na Uganda
ugenini, tumetoka sare na Nigeria na Algeria nyumbani na kuwafunga
Malawi nyumbani.
Aidha
timu ya Kilimanjaro Stars chini ya kocha Abdalla Kibadeni na msaidizi
wake Juma Mgunda katika mashindano ya CECAFA Challenge katika mechi nne
ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja kwa muda wa mchezo (Open
Play) ingawa ilitolewa kwa penati tano tano katika hatua ya nusu
fainali. Katika mashindano hayo Taifa Stars ilishinda mechi mbili na
kutoka sare mbili. Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha hawa wazawa
kiwango cha Tanzania FIFA kimekuwa kikipanda mara zote.
Tunawapongeza
sana makocha wetu hawa na benchi zima la ufundi. Kwa sasa tunajiandaa
na mechi mbali mbali za kufuzu kucheza fainali za Afrika Afcon 2017
nchini Gabon. Mechi hizi ni dhidi ya Tchad tarehe 25/03/2016 ugenini
Ndjadema na mechi ya marudiano siku tatu baadae hapa Dar es Salaam
tarehe 28/03/2015.
Imani
yetu ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi. Katika kujiandaa na
mchezo wetu dhidi ya Nigeria, Taifa Stars iliweka kambi nchini Uturuki
na pia timu iliweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mechi dhidi ya
Algeria. Kambi hizi zimesaidia sana kuimarisha timu yetu kabla ya mechi
hizi kubwa mbili. Katika kujiandaa na mechi dhidi ya Tchadi mwezi Machi
mwakani ratiba ya ligi kuu ikiruhusu timu itaweka kambi pia nje ya nchi.
2. Timu ya Taifa Wanawake “Twiga Stars”.
Timu
yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars chini ya kocha Rogasian Kaijage
ilifanikiwa kuiondoa Zambia na hivyo kufuzu fainali za michezo ya Afrika
Kusini Kongo Brazaville. Katika fainali hizi Tanzania ilifungwa na
Ivory Coast na Nigeria na kutoka sare na Congo, hivyo kutolewa kaika
hatua za makundi. Tunaamini uzoefu uliopatikana katika mashindano hayo
utaimarisha timu na kufanya Twiga Stars iweze kushiriki fainali ya
Afrika ya mpira wa wanawake nchini Cameroon mwaka 2016.
Hatua
ya awali Tanzania itapambana na Zimbabwe mwezi Machi 2016 na mshindi wa
michezo huo atacheza hatua ya pili dhidi ya mshindi kati ya Namibia na
Zambia.
3. Udhamini na michuano mipya.
Kwa kipindi hiki cha mwaka 2015 tumefanikiwa katika maeneo yafuatayo:
3.1 Kufufua Kombe la Shirikisho Azam Sports Federation Cup.
Kwa
kushirikiana na mdhamini Azam Sports Kombe la Shirikisho limefufuliwa na
kuboreshwa. Kwa mwaka huu tumeanza na timu 64 ambazo ni za ligi kuu
(16), Ligi daraja la kwanza FDL (24) na Ligi daraja la pili SDL (24).
Ili kupanua uwigo wa ushiriki wa Mikoa yote kwa misimu ya usoni timu
mabingwa wa mikoa (RCL) nazo zitashirikishwa katika mashindano haya ili
kila mkoa wa Tanzania upate fursa ya kushiriki katika mashindano haya.
Fainali itachezwa mwezi Mei na bingwa wa Kombe hili ataiwakilisha
Tanzania katika kombe la Shirikisho la Afrika CAF Confederation Cup.
3.2 Udhamini Ligi daraja la kwanza.
Tumefanikiwa
kupata wadhamini wawili kwa ligi daraja la kwanza FDL. Tumempata
STARTIMES ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi na pia kampuni ya Television
ya Sahara Media kupitia STAR TV imepewa haki za kuonyesha mechi hizi
moja kwa moja. Haya ni mafanikio makubwa kwa ligi ya daraja la kwanza.
Tunaishukuru kampuni ya Geita Gold kwa kuidhamini timu ya daraja la
kwanza ya Geita Gold Sport na tunazidi kutoa wito kwa washirika wengine
wazidi kujitokeza kudhamini timu zetu.
3.3 Mkataba wa Vodacom na Ligi Kuu.
Kampuni
ya Vodacom baada ya mazungumzo marefu tuliafikiana na kutuliana saini
ya mkataba mwingine wa miaka mitatu wa udhamini wa ligi kuu wenye
ongezeko la thamani ya udhamini kwa asilimia 40%. Jitihada zimefanyika
kuvutia wadhamini wengine nao waje waongeze udhamini kwa ligi kuu.
Tunaishukuru kampuni ya ACACIA ambayo imejitolea kuidhamini klabu ya
ligi kuu ya Stand United haya ni mafanikio makubwa kwa ligi yetu na
tunazidi kuvipa moyo vilabu vizidi kupata wadhamini zaidi.
Tunayashukuru
sana makampuni yote ambayo yamejitokeza kudhamini vilabu mbali mbali na
tunazidi kutoa wito kwa makampuni mengine yajitokeze kutoa udhamini
ikiwa ni sehemu ya kutangaza biashara na kukuza jina la chapa zao.
3.4 Udhamini tarajiwa.
Tunatarajia
kupata wadhamini kwa ajili ya Ligi Kuu ya vilabu vya wanawake (Women
Premier League) pamoja na ligi kya vilabu vya ligi kuu ya vijana chini
ya umri wa miaka 20 (U-20).
Jambo
hili likifanikiwa matumaini yetu ni kuwa tutaanzisha ligi mpya mbili
mwaka 2016, Ligi ya vilabu vya wanawake (Women Premier League) na ligi
ya vilabu vya ligi kuu ya vijana umri chini ya miaka 20 (U-20). Mechi
hizi nazo zitakuwa zinaonyeshwa moja kwa moja kwenye television.
Kwa
matarajio haya sasa ni vyema uongozi wa kila mkoa kufanya jitihada za
kuhakikisha vilabu vya mpira vya wanawake vinaanzishwa ili tuweze kuwa
na ligi ya ushindani.
Ninaomba
nichukue fursa hii kuwashukuru washirika wetu wote, ambao kama sio
kujitolea kwa haya mafanikio tusingeweza kuyafikia/kuyapata.
Ahsante Kampuni ya Bia Tanzania kwa kupitia bia ya Kilimanjaro Lager.
Ahsante Vodacom.
Ahsante Azam Tv kwa kupitia channel ya Azam Sports HD.
Ahsante Startimes Media kwa kupitia king’amuzi cha STARTIMES.
Ahsante Sahara Media kwa kupitia Star Tv.
Ahsante AIRTEL kwa kutuletea Airtel Raising Star kwa mara nyingine mwaka huu.
Ahsante Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF.
4. Soka la Vijana.
4.1 Fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17 (U-17) mwaka 2017 Madagascar.
Kikosi
chetu cha Taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17)
kinachojiandaa na hatua za mtoano mwezi Juni, 2016 ilikuwa kifanye ziara
ya kimichezo katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, lengo ilikuwa
kuwapatia vijana hao uzoefu wa Kimataifa. Wakati tayari kikosi
kimejiandaa na kukabidhiwa bendera, akaunti za TFF zilifungiwa na
mamlaka za mapato TRA na hivyo safari kuvunjika kwa ukosefu wa fedha.
Mpango mkakati ni kuwa mwezi Aprili, 2016 timu hii itaweka kambi nje ya
nchi ili kujiandaa na hatua ya mtoano (qualifiers).
4.2 Fainali za Afrika U-17 mwaka 2019.
Maandalizi
ya fainali hizi ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji yanaendelea vizuri
vikao na Wizara tayari vimeanza kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu
ya awali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Pia maandalizi ya
timu itakayoshiriki fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya
miaka 13 (U-13) kujumuishwa pamoja katika shule ya Alliance jijini
Mwanza. Imani yetu ni kuwa Tanzania tutafanikiwa kuandaa mashindano
mazuri mwaka 2019 na pia kunyakua kombe hili.
4.3 Vituo vya mikoa vya kukuza na kuendeleza vipaji.
Azma
ya TFF ni kuhakikisha kuwa kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa
kinakuwa na kituo mama cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira.
Mkataba wa mfano (template) umekwisha pelekwa katika kila mkoa ili vyama
vya mkoa ambavyo havina vituo vyake basi viingie mkataba wa ushirikiano
na kituo kimoja kwa lengo la kukifanya kiwe kituo mama cha mkoa.
Kupitia vituo hivi TFF itaweza kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira
wa vijana katika mikoa yetu, kuongeza nguvu kwa kuvipatia vifaa na
walimu. Mipira 5,000 ya 3 na 4 ya ukubwa (size), koni 3,000, beeps 2,000
tayari vimeagizwa toka nje ya nchi kwa kutumia vyanzo vya fedha vya TFF
yenyewe bila kuomba msaada kutoka popote kwa ajili ya kuendeleza
program hii. Tayari kila mkoa una mwalimu angalau mmoja aliyefanya kozi
ya FIFA ya ukocha wa vijana isipokuwa mikoa miwili tu ya Manyara na
Njombe, jitihada zitafanyika nao wapate walimu stahiki.
Hivyo
mtaji wa kutosha tunao wa kuanzisha vituo hivi. Pindi vituo hivi
vikiimarika yataanzishwa mashindano ya kiumri (age categories) baina ya
vituo hivi kuanzia ngazi ya mkoa, kanda na hatimaye Taifa. Ninatoa wito
kwa viongozi wenzangu wa mikoa tujizatiti tuweke nguvu katika
uwanzishwaji na uendelezaji wa vituo hivi ambavyo vitakuwa chachu kuu ya
kutoa wachezaji wa Taifa wa kike na wakiume. Baada ya mazungumzo haya
nitawakabidhi viongozi wa vyama vya mpira vya mkoa wa Manyara na Dar es
Salaam mpira mmoja mmoja ikiwa ni ishara ya kuanzishwa rasmi kwa program
hii ya kitaifa.
5. Kozi mbalimbali.
Kwa
kushirikiana na CAF na FIFA Shirikisho letu limeandaa, kuratibu na kutoa
kozi mbali mbali za waamuzi na makocha katika ngazi mbalimbali.
Jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha mikoa iliyokuwa na hazina ndogo
ya makocha na waamuzi inapewa fursa ya kuratibu kozi hizi. Tunashukuru
viongozi wote wa mikoa na wilaya ambao tumeshirikiana nao kutimiza azma
hii. Juhudi zinaendelea ili tuweze kupata makocha, waamuzi, madaktari wa
michezo na watawala zaidi. Ninaomba tuwape moyo wakina mama wazidi
kujitokeza kwa wingi kufanya kozi hizi maana wao ndio nguzo kuu ya
kuendeleza mpira wa wanawake nchini mwetu. Ninatoa rai kwa waajiri, hasa
wakurugenzi wa Halmashauri ambao ni waajiri wa walimu wanaofundisha
mpira mashuleni, wazidi kutupatia ushirikiano kwa kutoa ruhusa kwa
waajiriwa wao pindi wanapoomba kuhudhuria kozi mbalimbali zitolewazo na
TFF.
6. Bodi ya Ligi na Vilabu.
Utendaji
katika bodi yetu umeimarishwa kwa kutoa ajira kwa mtendaji mkuu Ndugu
Boniface Wambura. Mipango ya kuimarisha sekretariet ya Bodi ikiwa ni
pamoja na kupata nafasi kubwa zaidi ya kufanyia kazi iko mbioni.
Matarajio yetu ni kuwa chombo hiki kikiweza kuimarika kitakuwa ni chachu
ya kuandaa ligi zilizo bora zaidi na zenye ushindani.
Pamoja
na jitihada za kutafuta wadhamini wa mashindano mbalimbali
yanayohusisha vilabu, jitihada pia zinaendelea kufanyika kuhakikisha
vilabu vyetu vinaimarisha utawala bora. Kufuatia CAF na FIFA kuanzisha
utaratibu wa kutoa leseni kwa vilabu (Club Licencing) jitihada sasa
zinafanyika kuhakikisha vilabu vinaelimishwa kwa kina juu ya mahitaji ya
leseni hizi. Katika utaratibu wa leseni za vilabu, vilabu vyetu sasa
vitalazimika kuwa na ofisi, watendaji wa kuajiriwa, kuwa na maeneo ya
kufanyia mazoezi, kuwa na program ya maendeleo ya vijana, kuajiri walimu
wenye sifa n.k. Tunaamini utaratibu wa leseni za vilabu ukitekelezwa
ipasavyo uendeshaji wa vilabu vyetu utaboreshwa na hivyo kuongeza tija
kwa vilabu vyetu.
7. Tiketi za Eletroniki.
Kutokana
na matatizo yaliyojitokeza matumizi ya tiketi za eletroniki
yalisimamishwa na mmiliki wa uwanja wa Taifa ambaye ni Serikali. Baada
ya mazungumzo na mtoa huduma ambaye ni Benki ya CRDB ilikubaliwa
atafutwe mshauri mwelekezi (Consultant) kwa kupitia mfumo mzima ili
kubaini matatizo na baadae kutoa ushauri wa namna ya kuboresha mfumo
huo. Tenda ya kumpata mshauri huyu ilikwishatangazwa na kinachofuatia ni
TFF kwa kushirikiana na CRDB kuteua mshauri huyo. Imani yetu ni kuwa
kazi ya mshauri ikikamilika basi mwongozo utapatikana ili utekelezaji wa
uboreshaji wa mfumo ukamilike na matumizi ya tiketi za eletroniki
yaweze kuendelea.
8. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira (Football Development Fund).
Baada
ya mfuko huu kuanzishwa kikatiba katika mkutano mkuu uliopita, kamati ya
utendaji ya TFF iliteua wajumbe wa kamisheni ya uendeshaji wa mfuko huu
chini ya Mwenyekiti Ndugu Tido Mhando na Mtendaji Mkuu Henry Tandau.
Mfuko huu tayari umefanikiwa kupata ofisi yake na shughuli zake zitaanza
punde baada ya kuwekewa vitendea kazi. Lengo la mfuko huu kama
ilivyoanishwa ni kuwa chanzo kikuu cha kupata rasilimali kwa ajili ya
maendeleo ya mpira wa miguu nchini mwetu. Ninaomba tuwaunge mkono na
kuwapa ushirikiano watendaji wa mfuko huu huku tukitambua kuwa maendeleo
ya mpira yanahitaji rasilimali nyingi.
9. Kufungiwa akaunti za TFF.
Kutokana
na madeni ambayo yamekuwa kwenye mafaili ya mamlaka ya mapato kwa
kipindi karibia miaka mitano iliyopita, mamlaka ya mapato nchini TRA
iliamua kuzifungia akaunti zetu na pesa yote kuhamishiwa Benki kuu.
Mazungumzo yanaendelea kati ya TFF, Mamlaka ya mapato na Wizara husika
ili fedha hizi ziweze kurudishwa. Tunaushukuru uongozi wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao wametusaidia kutuongoza namna
ya kukabiliana na changamoto hii.
OMBI KWA SERIKALI.
Duniani
kote, iwe katika nchi tajiri au maskini, michezo huendelezwa kwa
ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na taasisi zinazoendesha shughuli
za michezo husika. Tunaiomba serikali tuzidi kushirikiana kwa karibu
katika kuandaa timu zetu za Taifa, kuboresha miundo mbinu ya kuchezea
mpira, kusaidia upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa gharama nafuu, kuto
fursa kwa waajiriwa wake, hasa walimu, wafanye kozi mbalimbali za
ukocha na uamuzi. TFF itafarikika sana iwapo itapewa fursa na Serikali
ya kuratibu na kusimamia mpira wa miguu katika mashindano ya Taifa ya
shule za msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA). Tunaamini TFF
ikipewa fursa hiyo itaongeza uweledi katika usimamizi wa mashindano hayo
na kuhakikisha vipaji vinaibuliwa kila mwaka kuliko ilivyo sasa.
Ndugu
zangu, wakati tunauaga mwaka 2015 na kuelekea kuingia mwaka 2016
ninaomba nimalizie kwa kutoa wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu
Tanzania tuzidi kushirikiana, penye makosa tukosoane japo kwa staha na
penye kuhitaji ushauri tushauriane.
Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utakuwa ni mwaka wa mafanikio kwa mpira wetu.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Ibariki Afrika.
Ahsanteni,
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
Dar es Salaam.
30 Desemba, 2015.
No comments:
Post a Comment