Na Mwandishi Wetu, Bahi.
Zaidi ya wananchi 2,500 wa Kata ya Ilindi, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wamenufaika na mradi wa ikolojia, bioanuai na uhifadhi wa mazingira unaotekelezwa kupitia kilimo jumuishi cha alizeti, Lozera pamoja na ufugaji wa nyuki, hatua inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha ya wananchi.
Wanufaika hao wamenufaika kupitia mradi unaotekelezwa na kikundi cha Chamlagwa Live, unaochanganya shughuli za kilimo na uhifadhi wa mazingira ili kuongeza kipato na kulinda rasilimali asilia.
Wakizungumza mara baada ya kutembelewa na wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji wa Programu ya Ruzuku Ndogo kutoka za mfuko wa mazingira Duniani (GEF SGP) ambazo zinasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, baadhi ya wanakikundi wa Chamlagwa Live wamesema mradi huo umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao na kipato cha wanakikundi pamoja na jamii inayowazunguka.
Mratibu wa kikundi hicho, kutoka shirika la Chamwiilee Agro-Live Group, Michael Mlonga, amesema mradi huo umeimarisha uwezo wa wakulima katika uzalishaji wa alizeti na kuwasaidia kuanza shughuli za ufugaji nyuki ambazo zimeongeza thamani ya mazao yao.
Naye mwanakikundi, Rose Sudai, amesema kupitia mradi huo wamepata maarifa ya kilimo bora na namna ya kuhifadhi mazingira huku wakiongeza kipato chao kupitia mazao ya alizeti na bidhaa za nyuki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Programu ya Ruzuku Ndogo za mfuko wa mazingira Duniani (GEF SGP) kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda, amesema lengo la ziara yao ni kukagua utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kuona namna inavyowanufaisha wananchi kiuchumi sambamba na kuhifadhi mazingira.
Amesema miradi hiyo inalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo kwa njia endelevu huku wakipambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naye mratibu wa kitaifa wa Programu ya Ruzuku Ndogo za Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF SGP) kutoka UNDP na mtaalamu wa masuala ya ufugaji nyuki, Faustine Ninga, amesema kilimo cha alizeti kinapofanyika sambamba na uwekaji wa mizinga ya nyuki shambani husaidia kuongeza uchavushaji wa mazao hayo na hivyo kuongeza uzalishaji.
Ameongeza kuwa nyuki hupata chakula cha kutosha kutoka kwenye mashamba ya alizeti huku wakulima wakinufaika na mazao mawili kwa wakati mmoja ambayo ni alizeti na asali.
Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 kuanzia Septemba 2024 na umefadhiliwa kwa kiasi cha dola za Marekani 50,000.
Kupitia ruzuku hiyo, wakulima hao wamefanikiwa kununua shamba ekari 13 kwa ajili ya kilimo darasa na uzalishaji wa mazao, kununua mashine ya kuchuja mafuta ya alizeti pamoja na mizinga 50 ya nyuki.
Aidha, wamegawa mbegu bora za alizeti kwa wakulima wa Wilaya ya Bahi ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta kupitia mashine waliyonunua.
Hata hivyo mashirika ambayo ni wadau wa maswala ya mazingira yanayotekeleza miradi hiyo yamejengewa uwezo na taasisi isiyo ya kiserikali ya jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF) ili kuweza kutoa matokeo bora ya uhifadhi wa bioanuai endelevu Tanzania.
Mradi huu ni mojawapo ya miradi 48 iliyofadhiliwa na shirika la Maendeleo Duniani UNDP-GEF SGP(2023-2025) na kuraibiwa na ofisi ya makamu wa Rais (VPO).






No comments:
Post a Comment