WAZIRI
MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano
imedhamiria kuhakikisha kila kinachokusanywa kama mapato ya nchi
kinatumika kwa maslahi ya Watanzania wote na si kwa manufaa ya wachache.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Novemba 29, 2015) wakati akifunga
maadhimisho ya miaka 20 ya Dayosisi ya Pwani ya Kanisa la African Inland
Church Tanzania (AICT) kwenye ukumbi wa PTA, viwanja vya Mwalimu
Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Serikali
imeanza kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali na kuepuka
matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma. Nia yetu ni kuhakikisha kila
kinachopaswa kukusanywa kama mapato ya nchi, kikusanywe na kitumike kwa
masuala ya msingi kwa ustawi wa Watanzania wote na si kwa watu
wachache,” alisema.
Akifunga
maadhimisho hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri
Mkuu alisema Serikali imedhamiria kupambana na maovu yote na kuondoa
kero zinazowaumiza wananchi wa kawaida. “Wako watu wanaoamini kwamba
hatuwezi, nawaomba waondoe hiyo dhana. Wako watu wanaodhani kwamba
kwamba utawala huu ni wa watu wapole, nao pia waondoe hiyo dhana,”
alisema huku akishangiliwa na mamia ya waumini waliohudhuria sherehe
hizo zilizoanza Novemba 27, 2015.
“Tunawaomba
Watanzania wote mtuunge mkono kwenye vita hii na mtuwezeshe kuifanya
kazi hiyo. Tunaomba waumini wote mtuombee katika sala zenu za kila siku
ili tuweze kuongoza kwa haki na kuwaletea Watanzania wote maendeleo,”
aliongeza.
Akinukuu
kitabu cha Mithali sura ya 29 mstari wa pili, Waziri Mkuu alisema:
“Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi, bali mwovu atawalapo, watu
huugua. Mtuombee viongozi wenu tuwe waadilifu na wenye kutenda haki.
Nasi tutaendelea kuwa waadilifu ili watu wetu wasigue,” alisema.
Aliwataka
viongozi wa kanisa hilo waendelee kuisaidia Serikali katika kujenga
kundi la watu wenye maadili mema ili walisaidie Taifa kuwa na watu
waadilifu na hivyo kupunguza kero nyingi zinazoikabili jamii.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini wa kanisa la hilo
kutoka mikoa mbalimbali, Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT, Askofu Silas
Kezakubi alisema Kanisa hilo litaendelea kumuombea Rais Dkt Magufuli na
viongozi wenzake ili wawe na afya njema, wawe na hekima na kuahidi
kwamba wataendelea kuwaweka chini ya ulinzi wa Mungu siku zote.
Alisema
wao kama kanisa wanaamini kwamba Serikali ya awamu ya tano ina nia ya
kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu lakini akasisitiza kuwa siri
ya bidii na uadilifu inapatikana kwenye neno la Mungu.
Akisoma
risala ya kanisa hilo, Askofu wa AICT Dayosisi ya Kibaha, Askofu
Charles Salalah alisema kanisa halina budi kushirikiana na Serikali kwa
sababu wote wanawahudumia watu walewale isipokuwa katika malengo
tofauti.
Alisema
kanisa hilo linahubiri maadili mema na bidii katika kazi kwa vile
linaamini kuwa maendeleo hayadondoki kutoka juu wala hayaoti kama uyoga
bali yanapatikana kwa watu kufanya kazi.
Akisisitiza
kuhusu uadilifu, aliwataka wazazi kudumisha ndoa zao ili watoto wapate
malezi mema kutoka kwa baba na mama na kwamba baba na mama wasipokaa
vizuri, watoto hawawezi kuwa waadilifu.
“Wazazi
tunao wajibu wa kupanda mbegu bora ya uzalendo kwa watoto wetu. Endapo
tutapanda mbegu mbaya ya kuwagawa watoto wetu kwa itikadi tofauti, ni
lazima tujue kuwa tutavuna tunachopanda.”
“Tukumbuke
kuwa tunalo Taifa moja tu la Tanzania. Hata kama watoto wetu watakuwa
na upenzi na vyama vyao, ni lazima tuwalee katika misingi ili wakue
wakijua Taifa letu ni moja tu. Ndiyo maana tunaweka mkazo kwenye familia
kwa sababu maadili mema yanaanzia nyumbani,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment