Waziri
wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda (kulia) akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) leo mkoani Dodoma kuhusu maendeleo
ya zoezi la Sensa ya Viwanda linalofanyika nchini. Kushoto kwake ni Idd
Mruke, Meneja Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, mkoa wa Dodoma.
Meneja
wa Takwimu za Biashara na Utalii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
ambaye ni Msimamizi wa Sensa ya Viwanda nchini akiwaelezea waandishi wa
habari leo mkoani Dodoma kuhusu vigezo vilivyotumika katika kuchagua
sampuli ya viwanda vilivyochaguliwa kufanyiwa utafiti. Kushoto kwake ni Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Waziri
wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda wakati akizungumza nao
leo mkoani Dodoma kuhusu maendeleo ya zoezi la Sensa ya Viwanda
linalofanyika nchini.
Na Veronica Kazimoto,
Wito umetolewa kwa wamiliki wote wa viwanda kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wasimamizi na wadadisi wanaokusanya taarifa za Sensa ya Viwanda inayoendelea hapa nchini.
Wito
huo umetolewa leo na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah
Kigoda wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dododoma ambapo
amesema ukusanyaji taarifa kwa nchi nzima umefikia wastani wa asilimia 80.5.
"Hadi kufikia tarehe 24 Mei,
2015 jumla ya viwanda vidogo 9,540 sawa na asilimia 82 pamoja na
viwanda vya kati na vikubwa 1,158 sawa na asilimia 79 vilikamilika
kukusanywa taarifa zake. Hii inafanya ukusanyaji Takwimu kwa nchi nzima
kuwa wastani wa asilimia 80.5", amesema Dkt. Kigoda.
Aidha, Waziri Kigoda amesema licha ya mafaniko hayo, bado kuna kazi kubwa ya kukamilisha viwanda vilivyobaki ambavyo ni takriban 2,032 sawa na wastani wa asilimia 19.5.
"Hivyo, nawaasa wamiliki wote wa viwanda hususani katika mikoa ya Dar
es Salaam, Tanga, Arusha, Morogoro, Tabora, Kigoma na Manyara kutoa
ushirikiano zaidi na wa kutosha kwa zoezi hili ili ifikapo mwisho wa
mwezi huu wa Juni, 2015, tuweze kuhitimisha", amesisitiza Dkt. Kigoda.
Waziri
Abdallah Kigoda amesema lengo kuu la Sensa ya Viwanda ni kukusanya
takwimu sahihi zinazohusu Sekta ya Viwanda nchini ambazo zitawezesha
kupata viashiria sahihi vya uchumi pamoja na taarifa muhimu za viwanda
kama vile orodha ya viwanda kimkoa, anuani na mahali vilipo, aina ya
umiliki na utaifa wa wamiliki.
Taarifa
nyingine ni pamoja na mwaka ambao viwanda hivyo vimeanza uzalishaji,
shughuli kuu ya viwanda husika, idadi ya wafanyakazi, gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mapato yanayotokana na uzalishaji na gharama za uzalishaji.
Lengo lingine la Sensa ya Viwanda ni kupima
na kufuatilia mabadiliko yanayotokea katika Sekta ya Viwanda ili
kuiwezesha Serikali kuboresha sera na programu za kukuza ajira, kupanga
na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo kama vile Malengo ya
Milenia, Dira ya Maendeleo ya Tanzania, 2025, Malengo ya MKUKUTA na
Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN).
Jumla ya Wadadisi 198 wameajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kukusanya Takwimu na taarifa viwandani ambapo wanasimamiwa na Mameja Takwimu wa Mikoa, Watakwimu kutoka Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Maafisa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.
No comments:
Post a Comment