Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele.
Ngorongoro ni moja kati ya wilaya tano zinazounda Mkoa wa Arusha. Upande
wa Kaskazini inapakana na nchi ya Kenya, Mashariki kuna Wilaya ya
Monduli, Kusini kuna Wilaya ya Karatu na Magharibi kuna Mkoa wa Mara.
Pia Ngorongoro ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Kaika
Saning’o Telele kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), likiwa na jumla
ya wakazi 129,776, wengi wakiwa ni kutoka jamii ya Kimasai kwa mujibu
wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002.
Wiki iliyopita, Uwazi lilifanya ziara jimboni humo na kuzungumza na
wananchi mbalimbali ambao walieleza kero zinazowasumbua, kubwa ikiwa ni
mgogoro sugu wa ardhi na jinsi mbunge wao anavyoshughulikia kero zao.
MATATIZO YA WANANCHI
Katika ziara hiyo, Uwazi lilizungumza na wananchi mbalimbali ambao wengi
kilio chao kikubwa kilikuwa ni mgogoro mkubwa wa ardhi unaoendelea wa
Pori Tengefu la Loliondo ambapo wanalalamika kwamba serikali kwa
kushirikiana na makampuni ya kigeni ya uwindaji, wanataka kuwapora ardhi
yao bila kuzingatia sheria, jambo linalotishia usalama wa wananchi na
mali zao.
“Tupo hapa tangu enzi za ukoloni, leo tunaambiwa eti haturuhusiwi
kuchunga mifugo yetu kwa sababu hili ni pori tengefu, wanataka tukalishe
wapi mifugo yetu? Huu ni uonevu,” Daudi Ole Sayinka, mkazi wa Loliondo
aliliambia Uwazi.
Uwazi liliendelea na ziara yake ambapo lilibaini matatizo mengine mengi
yanayowasumbua wananchi wa eneo hilo ambapo kutokana na utata uliopo
kwenye eneo la Pori Tengefu la Loliondo, wakulima na wafugaji wameanza
kugombea sehemu za malisho na kilimo, huku wakulima wakilalamika kwamba
wafugaji wa Kimasai wanaingiza mifugo kwenye mashamba yao, jambo
linalosababisha machafuko ya mara kwa mara kati ya jamii hizo mbili.
Mwamko mdogo wa kielimu jimboni humo ni tatizo lingine ambapo watoto
wenye umri wa kuandikishwa shule, wamekuwa wakinyimwa fursa hiyo na
badala yake kupewa kazi ya kuchunga mifugo, jambo linalosababisha watu
wengi washindwe kusoma na kuandika, huku mahudhurio shuleni yakiwa
hafifu.
Uhaba wa walimu, madarasa na vifaa vya kujifunzia ni tatizo lingine
lililobainishwa na wananchi wa jimbo hilo huku pia suala la
kutonufaishwa na rasilimali zilizopo jimboni humo, zikiwemo mbuga za
wanyama na Kreta ya Ngorongoro kukionekana kuwasononesha wananchi wengi.
“Jimbo letu lina rasilimali lukuki lakini sisi wala hatufaidiki, hata
kuwinda vitoweo haturuhusiwi wakati kuna wageni wanakuja hapa na
wanapewa vibali vya kuwinda na kutalii watakavyo, tunaomba serikali
ituangalie kwa jicho la huruma,” Matei Sanko aliliambia Uwazi.
Kero nyingine ni uduni wa huduma za afya, ubovu wa miundombinu kwenye
baadhi ya maeneo na wanyama wakali wanaovamia maboma ya wafugaji na kuua
mifugo pamoja na binadamu. Uhaba wa maji safi na salama kwenye baadhi
ya maeneo, ni kero nyingine jimboni humo.
Baada ya kuzungumza na wananchi mbalimbali, Uwazi lilimtafuta mheshimiwa
mbunge wa jimbo hilo, Telele ili kupata ufafanuzi wa kero zilizoibuliwa
na wananchi wake.
Hata hivyo, juhudi za kumpata mbunge huyo ziligonga mwamba kutokana na
simu yake kuita muda wote alipopigiwa bila kupokelewa. Hata mwandishi
wetu alipomtumia ujumbe mfupi wa maandishi na kumuorodheshea kero za
wapiga kura wake, mbunge huyo hakujibu chochote mpaka gazeti hili
linakwenda mitamboni.
Juhudi za kumtafuta mbunge huyo bado zinaendelea ili atoe ufafanuzi wa
kero za wapiga kura wake, likiwemo suala sugu la mgogoro wa ardhi
Loliondo.
CREDIT:GPL
No comments:
Post a Comment