Naibu
Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka Australia
Magharibi Kim Hames (kushoto) akimweleza Waziri wa Nishati na Madini,
George Simbachawene (Kulia) maeneo ambayo nchi ya Australia ingependa
kuwekeza.
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene (Kulia) akimshukuru Naibu
Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka Australia
Magharibi Kim Hames (kushoto) mara baada ya kumkabidhi zawadi. Wengine
ni ujumbe ulioambatana na Naibu Waziri Mkuu huyo.
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene ( wa pili kutoka kulia) Naibu
Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka Australia
Magharibi Kim Hames ( wa tatu kutoka kulia) wakiwa katika picha ya
pamoja na ujumbe kutoka Australia uliohudhuria kikao hicho.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameitaka nchi ya Australia
kuimarisha uwekezaji katika sekta za nishati na madini nchini ili ziweze
kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Simbachawene
aliyasema hayo katika kikao chake na Naibu Waziri Mkuu wa Australia
Magharibi, Kim Hames na ujumbe wake aliyemtembelea ofisini kwake kwa
ajili ya kupata taarifa za maeneo yanayohitaji uwekezaji nchini.
Alisema
uhusiano kati ya Tanzania na Australia ni wa muda mrefu, ambapo
Australia imekuwa ikiwekeza nchini kupitia sekta ya madini kupitia
makampuni yake ya madini na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aliendelea
kusema kuwa kupitia makampuni ya madini ya Australia, huduma za jamii
kama vile miundombinu, elimu na afya zimeboreshwa.
Wakati
huo huo Afisa Mtendaji kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) Prof.
Abdulkarim Mruma akielezea ushirikiano kati ya wakala huo na Australia,
alisema kuwa nchi ya Australia kupitia chuo chake cha Cuten
ilishirikiana na GST katika kufanya utafiti wa madini katika ukanda wa
dhahabu ulioko kusini mwa Dodoma uliopelekea kugundulika kwa madini ya
dhahabu na almasi.
Aliongeza
kuwa kupitia utafiti wa madini katika ukanda wa dhahabu ulioko Dodoma
watumishi wawili kutoka wakala huo walifanikiwa kupata shahada za
uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Cuten.
Aliongeza
kuwa, nchi ya Australia imekuwa ikitoa ufadhili kwa watumishi wake
kusomea katika musala ya uchenjuaji madini na maabara katika ngazi za
shahada na uzamifu.
Profesa
Mruma aliiomba nchi ya Australia kuendelea kusaidia Wakala huo kwa
vifaa vya kisasa vya jiofizikia na kemia pamoja na mafunzo yanayohusu
madini katika ngazi mbalimbali.
Naye
Mkuu wa Chuo cha Madini, Sudian Chiragwile aliongeza kuwa, chuo
kilikabidhiwa mgodi wa Resolute uliokuwa unamilikiwa na kampuni ya
Golden Pride ya Australia ambapo wamekuwa wakiutumia kwa ajili ya
mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.
Alisema
mgodi wa Resolute ulioachwa bado una eneo kubwa linaloweza kuchimbwa
madini na kuwataka wawekezaji kutoka Australia kujitokeza na kuwekeza
kwenye shughuli za madini.
Naibu
Waziri Mkuu wa Australia ambaye pia ni Waziri wa Afya na Utalii kutoka
Australia Kim Hames alisema kuwa, nchi ya Australia ipo tayari
kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji hususan katika sekta za
nishati na madini na kuongeza kuwa katika kuboresha sekta ya madini,
kutakuwa na programu za kubadilishana utaalam na uzoefu kwa wataalam
kutoka Tanzania na Australia.
Hames
alisisitiza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za
madini na kuahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuinua
sekta ya madini nchini.
No comments:
Post a Comment