Ndugu na jamaa wa marehemu Victoria Silvester (53), wakiwa ndani ya
chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya KCMC, huku wakiwa
wamevaa magunia walipokwenda kuuchukua mwili kwa ajili ya mazishi,
mkoani Kilimanjaro jana. Picha na Dionis Nyato.
Moshi. Ilikuwa ni
kama kutekeleza maandiko ya Biblia yanayosema “jifungeni nguo za
magunia, ombolezeni na kulia kwa uchungu”, wakati ndugu walipokwenda
Hospitali ya Rufaa ya KCMC kuchukua mwili wa marehemu.
Walikuwa wamevalia magunia, lakini sababu ya kuvalia nguo hizo haikuwa
kama maandiko hayo yanavyosema kuwa “kwa sababu hiyo jifungeni nguo za
magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana
haikugeuka na kutuacha”.
“Tumejiuliza maswali mengi, tumeshindwa kupata majibu. Tumejiuliza tuvae
nguo gani hatukupata majibu. Kwa kuvaa hivi tunataka hao wauaji wajue
damu hii itawalilia popote walipo,” alisema Beata Kiria, ambaye ni dada
wa Victoria Sylvester aliyeuawa na watu wasiojulikana na mwili wake
kuzikwa nusu kiwiliwili.
Beata na ndugu zake walifika kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kuuchukua mwili huo wakiwa wamevalia magunia.
Tukio hilo lilitokea jana kati ya saa 4:30 asubuhi na saa 6:00 mchana
wakati ndugu hao walipofika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali,
huku baadhi yao wakiwa pekupeku na kusababisha watu wengi waliokuwa eneo
hilo pamoja na watumishi wa hospitali kuwashangaa.
Wakiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, ndugu hao walilia wakipaza
sauti wakitaka wauaji wa mwanamke huyo wakamatwe kabla ya kuchukua mwili
na kuondoka nao.
Victoria (53), mkazi wa Kijiji cha Masherini, Umbwe eneo la Kibosho
aliuawa kwa kukatwa mapanga usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita na baadaye
wauaji kuuzika mwili wake nusu na kuacha kiwiliwili nje ya nyumba
waliyokuwa wakiishi, jambo lililoibua utata mkubwa ndani ya familia
hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Kiria alisema walichagua mavazi hayo baada ya kukosa vazi lingine.
“Tulitafakari tuvae nguo gani ili kumuenzi marehemu lakini hatukupata
jibu, ndiyo tukaamua tuvae magunia kuonyesha kuwa waliomuua ndugu yetu
thamani yao inafanana na magunia haya,” alisema Kiria.
Imezoeleka misiba mingi ndugu huvaa suti nyeusi kwa wanaume huku
wanawake wakivalia mavazi meusi au meupe ambayo baadaye hujifunika na
vitambaa vyeusi au vyeupe kwa akina mama.
Kiria, ambaye alizungumza kwa niaba ya familia, alilitaka Jeshi la
Polisi kuhakikisha linawatafuta na kuwakamata watu waliohusika na mauaji
hayo.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema
wanamshikilia mume wa marehemu, Silvester Mmasi na mtumishi wao ambaye
hakumtaja kwa ajili ya mahojiano kuhusu mauaji hayo na polisi inaendelea
kuwatafuta washukiwa wengine.
Source :MWANANCHI
No comments:
Post a Comment