WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amepokea msaada wa vitabu 895 vyenye thamani ya sh.
milioni 6.5/- ikiwa ni jitihada ya wadau mbalimbali kuchangia shule ya
msingi aliyosoma ya Kakuni iliyoko kijiji cha Kibaoni, wilayani Mlele,
mkoani Katavi.
Waziri
Mkuu amepokea msaada huo jana mchana (Jumanne, Mei 26, 2015) kwenye
shule mpya ya msingi Kakuni ambayo bado inaendelea kujengwa kwenye
kijiji cha Kibaoni.
Akizungumza
katika hafla hiyo fupi mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu
Pinda aliishukuru kampuni ya General Booksellers Ltd ya kutoka Dar es
Salaam kwa msaada huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa
kuitimiza ndoto yake aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.
“Wazo
la ujenzi wa shule mpya ya msingi Kibaoni lilitokana na ukweli kwamba
nilisoma na kumaliza kwenye shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni mtumishi wa
Serikali, ni Mbunge na sasa hivi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania nilijiuliza hivi shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi?”
“Nilijiuliza
sana ni jambo gani ambalo naweza kulifanya la kusaidia wanakijiji
wenzangu na kata nzima ya Kibaoni kama shukrani kwa kunilea na
kunifikisha hapa nilipo. Ndipo wazo la kujenga shule niliyosoma
likazaliwa kama mwaka mmoja na nusu uliopita,” alisema Waziri Mkuu
wakati akiwahutubia wazazi, walimu na wanafunzi.
Mapema,
akiwasilisha msaada huo, mwakilishi wa kampuni ya General Booksellers
Ltd, Bw. Joachim Masaburi alisema wameamua kuchangia vitabu hivyo kwa
kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto lakini pia wanatambua juhudi za
Serikali za kutoa elimu bora.
Akitoa
mchanganuo wa vitabu hivyo, Bw. Masaburi alisema: “Kuna vitabu 600 kwa
ajili ya shule ya awali ambavyo kati yake 300 ni vya ngazi ya chini
(nursery) na vitabu vingine 300 ni vya ngazi ya juu (pre-school). Vyote
ni vya hisabati, Kiingereza na sayansi”.
“Kwa
shule ya msingi wao tunawapatia kivunge cha kufundishia mfumo wa mwili
wa binadamu kama sehemu ya masomo ya sayansi, hiki kina thamani ya sh.
550,000/-,” alisema.
Pia
kampuni hiyo ilitoa msaada wa vitabu vingine 295 vya Baiolojia,
Fizikia, Uraia, Kiswahili kwa ajili ya shule ya sekondari ya Mizengo
Pinda iliyoko kijijini hapo.
Hadi
sasa majengo yaliyokamilika kwenye shule hiyo ni madarasa 14, jengo la
utawala lenye ofisi za walimu na maktaba mbili (wanafunzi na walimu),
jengo la TEHAMA la wanafunzi lenye darasa moja, ukumbi mdogo na ofisi za
walimu na jengo moja la choo lenye matundu 48. Pia ujenzi wa nyumba
sita za walimu uko kwenye hatua ya kuezeka. Nyumba hizo zinajengwa na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Ujenzi wa choo kingine chenye matundu
48 umeanza.
Waziri
Mkuu aliwaomba wananchi wengine wamsaidie kutimiza ndoto yake kwani
bado anakabiliwa na kazi ya kuweka umeme, maji, kujenga nyumba nane za
walimu, bwalo na jiko, karakana nne za ufundi, ujenzi wa kituo cha
walimu cha mafunzo ya muda mfupi na utunzaji taarifa (Resource Centre),
viwanja vya michezo vya kisasa vinavyozingatia michezo yote, mfumo wa
uvunaji maji ya mvua, mfumo wa maji safi na maji taka, nyumba mbili za
walinzi na uzio wa shule.
Alitaja
vitu vingine ambavyo bado vinahitaji kuchangiwa ni meza za walimu – za
ofisini na darasani, viti vya walimu – vya ofisini na darasani, madawati
ya shule ya msingi na ya awali, meza na viti vya maktaba zote mbili,
meza na viti vya bwalo – shule ya msingi na shule ya awali.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MEI 27, 2015.
No comments:
Post a Comment