Matukio : Ban Ki Moon Awageukia Viongozi wa Madhehebu ya Dini Duniani - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 23 April 2015

Matukio : Ban Ki Moon Awageukia Viongozi wa Madhehebu ya Dini Duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban  Ki Moon akiwa na  Viongozi wa Madhehebu  mbalimbali ya Dini mara baada ya  viongozi hao wa dini kuzungumza katika mkutano wa ngazi ya juu uliojadili  pamoja na mambo mengi kuongezeka kwa vurugu zitokanazo na itikadi kali za kidini na ukereketwa wa kupindukia na  nini kifanyike kukabiliana na  changamoto hiyo. katika picha hii yupo pia Rais wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa, Bw. Sam Kutessa ambaye ndiye aliyandaa mkutano huo.
Na  Mwandishi Maalum, New York
 Kufuatia ongezeko la  makundi ya dini  yenye itikadi , matukio ya  kigaidi,  kukosekana  kuvumiliana na maridhiano,  Katibu Mkuu wa     wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amewageukia viongozi wa  madhebu ya  mbalimbali  dini  duniani akiomba busara zao na uongozi wao.
Amesema, busara na uongozi wa madhehebu  hayo ya dini  unahitajika sana  katika kuhubiri na kueneza kuvumiliana,  maridhiano,  stahimili,  kuheshimiana na kujenga utamaduni wa kuzungumza   miongoni wa  jamii bila ya kujali dini zao au rangi zao.
Ban Ki Moon ametoa wito  huo  siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  wakati wa mkutano wa  ngazi ya juu  uliojadili kwa kina kuhusu dhana ya  kukuza uvumilivu na maridhiano mkazo ukiwa katika kujenga jamii yenye Amani, jumuishi na namna ya kukabiliana na vurugu zitokanazo na itikadi kali za kidini.
Mkutano huo  ambao ulianza siku ya  jumanne  uliandaliwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Bw. Sam Kutesa  kwa kushirikiana na  Taasisi ya  Muungano wa  Ustaarabu  ambapo washiriki mbalimbali  wakiwamo  viongozi wa madhehebu ya dini walipata fursa ya kutoa tathmini ya hali ya sasa  na hatari inayoikabili dunia na watu wake hasa kutokana na kukithiri kwa wimbi la machafuko   na mauaji kwa visingizio mbalimbmali.
Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi ni miongoni mwa  washiriki waliochangia majadiliano hayo ambapo alielezea uzoefu wa  Tanzania juu ya namna ambavyo madhehebu ya dini  ya kiislamu na kikristo  yalivyoanzisha na kuenzi misingi ya majadiliano katika kutafuta suluhu na maridhiano ya changamoto mbalimbali.
Akizungumza  siku hiyo ya jumatano ambapo viongozi wa madhehebu ya dini walipata fursa ya kutoa maoni, mitizamo na mapandekezo yao. Ban Ki Moon alisema:
“ Waheshimiwa viongozi wa dini, leo naomba  busara zenu na uongozi wenu, kuna maeneo mawili ambayo mnaweza kuleta  matokeo. Moja  tunahitaji kueneza na kukuza majadiliano miongoni mwa  madhehebu ya dini ili kupunguza   sitofahamu na mihemuko  baina ya waumini wa dini .” akasema Ban Ki Moon
Jambo  la pili ambalo amelieza kuwa viongozi wa dini  wanaweza kutekeleza ni  kuzungumzia mazingira yanayotoa fursa kwa   vikundi vyenye itikadi kali ya kushawishi na kuvutia wafuasi wapya. 
Amesema Ban ki Moon  ,  viongozi   wa madhehebu ya dini,  wanaupeo mkubwa wa kutambua  viashiria vya uwepo wa vurugu na vuguvugu la waumini wao kurubuniwa na  kuwa na mwelekeo wa itikadi kali za kidini.
“Ninawaomba  mtumie ushawishi wenu wa kiroho na  uadilifu , kupinga maelezo yao kwa kusimamia katika  kiasi na maelewano ya pamoja. Na   kuongeza.  Sauti zenu ni muhimu sana katika  kukemea kauli za kibaguzi na kutafuta msimamo wa pamoja”.  amesisitiza katibu  Mkuu
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa,  ameeleza kwamba  ni vema kila mmoja wetu akajiuliza ni nini kinachoshawishi au vutia  itikadi kali na ukereketwa wa kupindukia.
Akasema   wengi wanaojiunga na makundi  yenye itikadi kali ni vijana lakini  hivi sasa  kuna wimbi la wanawake wanaojiunga jambo alilosema  linatisha Zaidi.  
Ban Ki Moon  amesema,  makombora yanaweza kuwauwa magaidi. Lakini anashawishika kuamini kwamba utawala bora ndio utakaomaliza ugaidi kwa kusimamia misingi ya  utawala wa sheria, haki za binadamu,  kumaliza umaskini,  na kuondoa pengo la kati ya walio nacho na wasionacho.
Katibu Mkuu amewaeleza viongozi hao wa dini kwamba anakusudia kuunda Jopo la washauri la viongozi wa dini na wengine litakalotoa mwongozo wa namna ya  kushughulikia changamoto mbalimbali.
Aidha  amebainisha kwamba baadaye mwaka huu atawalisha Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia  vurugu zinazosababishwa na  ukereketwa wa kupindukia.
Viongozi wa madhehebu ya dini  waliozungumza katika mkutano huo, walisisitiza sana kuhusu umuhimu wa  utoaji wa elimu na mafunzo yanayozingatia au kujielekeza  katika  kukuza misingi ya  kustahimiliana na kuheshimiana  kwa  misingi ya tofauti za kidini, kiimani, uhuru wa  mtu kuabudu bila ya kujali tofauti ya rangi yake au nchi anayotoka.
Wamesisitiza kwamba elimu hiyo inapashwa kutolewa kuanzia katika shule za awali hadi vyuo vikuu, jambo ambalo wanaamini kwamba kama likifanyika kwa umakini siyo tu litawaepusha  vijana kujiingiza katika  misimamo ya itikadi kali na ukereketwa wa kupindukia lakini pia utaifanya dunia kuwa mahali salama.
Vile vile wamesisitiza kuwa, hakuna dini yoyote inayohubiri chuki, kubaguana au kuuana, bali dini zote  na vitabu vya dini vinasisitiza katika  kuishi kwa upendo, Amani,  kuvumiliana na kuridhiana kwa kuwa wote ni watoto wa mungu.

Vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya  kijamii pia viliguswa katika majadiliano hayo, ambapo wazungumzaji wengi walivitaka   viwe sehemu ya utoaji wa elimu na kujenga misingi ya  ustaarabu wa kuvumiliana na kujiepusha kuwa vipaza sauti au wasemaji au wachochezi wa  itikadi kali za kidini na ukereketwa wa kupindukia.

No comments:

Post a Comment