Siasa Zetu : Wananchi wamchangia Pesa Innocent Melleck ili Achukue Fomu ya Kugombea Jimbo la Vunjo - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Saturday, 14 March 2015

Siasa Zetu : Wananchi wamchangia Pesa Innocent Melleck ili Achukue Fomu ya Kugombea Jimbo la Vunjo

Inocent Melleck akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza kumchangia fedha kwa ajili ya kuchukulia fomu za kuwania Ubunge katika jimbo la Vunjo.
Innocent Melleck akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi hao waliojitokeza kumchangi fedha kwa ajili ya kugombea Ubunge katika jimbo la Vunjo.

Baadhi ya wananchi katika Jimbo la Vunjo wakimsikiliza Innocent Melleck waliyemchangia fedha kwa ajili ya kugombea Ubunge katika jimbo hilo.
Na Dixon Busagaga
MBUNGE wa jimbo la Vunjo,Agustino Mrema(TLP) ameendelea kupata upinzani katika Jimbo lake baada ya baadhi ya wananchi kujitokeza hadharani na kumchangia pesa,Innocent Melleck Shirima kwa lengo la kumchukulia fomu wakati wa kugombea nafasi ya Ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi.
Tayari joto la uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu limeanza kushika kasi katika jimbo hilo baada ya Mwenyekiti wa Chama cha NCCR –Mageuzi,James Mbatia kuombwa na wananchi wa jimbo hilo kugombea nafasi ya Ubunge.
Mbatia ambaye aliridhia hatua ya wananchi hao na kuamua kutangaza nia ya kugombea Ubunge kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ameingia katika mgogoro na Mrema aliyedai kuwa amekuwa akichafuliwa mbele ya wapiga kura wake.
Wakizungumzia hatua hiyo ya kuchanga fedha ,baadhi ya wananchi hao wakiwemo wafanyabiashara wadogo wadogo,madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda na wakulima walisema wameamua kuchanga fedha hizo ili kumshawishi Shirima ajitikeze katika kuwania nafasi hiyo.
“Tumefikia uamuzi huu ili tuone ni namna gani tunaweza kumshawishi huyu kijana ili ajitokeze kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hili, kutokana na kumuona kuwa anafaa na ndiye anayeweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.”alisema Ikunda Moshi mkazi wa Himo kwa niaba ya wenzake.
Ili kufanikisha jambo hilo wananchi hao wamelazimika kuunda kamati maalumu ya kuratibu shughuli ya ukusanyaji wa fedha pamoja na kuhakikisha Shirima anatangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo,
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ,Elisanguo Meena alisema hadi sasa tayari wameweza kuchangisha kiasi cha Sh. Mil.2.6 kwa ajili ya uchukuaji wa fomu na kuanzisha mfuko wa kampeni katika jimbo hilo.
Kwa upande wake Shirima alisema hakuwahi kufikiri kuwa wananchi wanaweza kujitokeza kuwania ubunge katika jimbo hilo na kwamba anapokea kwa mikono miwili ombi lao hilo na atatoa majibu baada ya muda mfupi.
“Nimesikia wananchi wamenichangia fedha ili nijitokeze kuwania ubunge katika jimbo la Vunjo,kwa kweli wamefanya jambo ambalo sikuwahi kulitegemea,naomba niwajulishe kuwa wazo la kugombea Ubunge katika jimbo hili kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi bado nalitafakari”alisema Shirima.
Alisema ifikapo mwezi April mwaka huu ndio atatoa muelekeo way eye kutangaza nia ya kuwania Ubunge jimboni humo huku akitamba kuwa Chama cha Mapinduzi kina nafasi kubwa ya kushinda katika kiti cha Ubunge katika jimbo hilo.
Aidha Shirima alisema vijana wana nguvu na wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo hivyo ni vyema wananchi wote wa jimbo hilo wakamuunga mkono wakati utakapofika, ili kuweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika jimbo hilo.
Alisema katika Jimbo la Vunjo, anahitajika kiongozi atakaye waunganisha wananchi na serikali yao na ambaye atakuwa ni mcha Mungu, anayefuata maadili ya kimungu na muwazi kwa wananchi wake.
Uamuzi wa Shirima (CCM) utafanya idadi ya watu watakaokuwa wametangaza nia ya kuwania Ubunge katika jimbo hilo kufikia zaidi ya watano ,akiwemo mbunge wa sasa,Mrema (TLP) Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi taifa ,James Mbatia, Mwandishi wa kujitegemea (BBC) Exaud Makyao (Chadema) na Peter Msack (CCM).

No comments:

Post a Comment