Rais Uhuru Kenyatta na Rais Mstaafu Daniel arap Moi walipokutana ikulu, Nairobi Agosti 1, 2013. Picha/PSCU
Na BENSON MATHEKA
Kwa Mukhtasari
Serikali
ya Jubilee imejitokeza kuwa marudio ya utawala wa miaka 24 wa Rais
Mstaafu Daniel arap Moi na chama chake cha KANU. Wadadisi wanasema kuwa
licha ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu William Ruto kujidai kuwa
wanaongoza serikali ya kidijitali, wamezama katika mbinu ambazo
hazilingani na kauli mbiu hiyo yao.
SERIKALI ya Jubilee imejitokeza kuwa marudio ya utawala wa miaka 24 wa Rais Mstaafu Daniel arap Moi na chama chake cha KANU.
Hii ni kutokana na mbinu ambazo
watawala wa Jubilee wanatumia kuongoza nchi, ambazo zinalandana pakubwa
na za utawala wa Moi aliyestaafu miaka 12 iliyopita.
Wachanganuzi wa siasa wanasema sababu kuu ya
mbinu za utawala wa Moi na Kanu kujirudia ni kuwa viongozi wa Jubilee,
Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto walikuwa wanafunzi
watiifu wa Moi kuhusu siasa na uongozi, na hivyo si ajabu wanatumia
mtindo sawa na aliotumia katika utawala wake.
Wadadisi wanasema kuwa licha ya Rais
Kenyatta na Bw Ruto kujidai kuwa wanaongoza serikali ya kidijitali,
ukweli ni kuwa wamezama katika mbinu ambazo hazilingani na kauli mbiu
hiyo yao.
Mbinu ambazo Jubilee imekopa kutoka kwa KANU ni pamoja na:
KUZIMA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI
Katika utawala wa Moi, yalikuwa
makosa makubwa kwa vyombo vya habari kukosoa serikali ama kufichua maovu
na udhaifu wake. Wanahabari waliofanya hivyo waliandamwa vikali na hata
kutupwa jela. Sheria za kudhibiti vyombo vya habari zilikuwa kali na
Wakenya hawakuwa na uhuru wa kuamua habari ambazo wangetaka kupata.
Vyombo huru vya habari vilinyimwa kibali na kwa muda mrefu KBC ndiyo
pekee iliyopeperusha habari, nyingi yazo zikiwa kuhusu Moi na mawaziri
wake.
Katika utawala wa Jubilee, mambo
yamejirudia kwa Serikali kutumia mbinu mbalimbali kuzima uhuru wa vyombo
huru vya habari. Thibitisho la majuzi kabisa ni hatua ya kuzimwa kwa
televisheni nne kuu huru za NTV, QTV, KTN na Citizen. Hatua hii
imehakikisha kuwa sauti huru, upinzani na wakosoaji wa serikali hawana
nafasi ya kuwasilisha jumbe zao kwa wananchi.
Ishara nyingine ya kuzima uhuru wa
habari ilijitokeza kwenye sheria tata za usalama ambazo zina vipengele
vya kuwekea breki vyombo vya habari katika kufichua na kuripoti mambo
fulani.
Mbali na sheria hizo, kuna sheria nyingi za mawasiliano na za kudhibiti vyombo vya habari zinazotoa adhabu kali.
Masuala haya yameonekana kurudisha
nyuma mafanikio makubwa ya uhuru wa vyombo vya habari yaliyopatikana
chini ya utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, ambaye alihakikisha
ukadamizaji wa vyombo vya habari ulioshuhudiwa chini ya utawala wa Moi
umekomeshwa.
KUKADAMIZA MASHIRIKA YA KIJAMII.
Katika miaka 24 ya utawala wa Moi,
mashirika ya kijamii yalichukuliwa kama adui kwa kukosoa serikali.
Viongozi wa mashirika hayo waliandamwa usiku na mchana hasa enzi za
kutetea utawala wa vyama vingi. Kwa kukandamiza mashirika haya, sauti ya
mwananchi wa kawaida ilizimwa huku mashirika mengi yakipigwa marufuku
serikali.
Chini ya kipindi cha miaka miwili,
Serikali ya Jubilee inajaribu mbinu za kila aina kukabiliana na
mashirika ya kijamii kwa kupiga marufuku baadhi yao ikisema kwamba
hayakuwa yametimiza masharti yanayohitajika.
Pia kuna sheria ambazo
zimependekezwa za kuzima mashirika hayo, jambo ambalo wadadisi wanasema
ni katika juhudi za Jubilee kuzima wakosoaji wake. Kwa kufanya hivi,
wadadisi wanasema Jubilee itakuwa imeua demokrasia na kurudisha nchi
enzi za utawala wa kiimla.
AHADI TUPU ZA KUKABILI UFISADI
Serikali ya Moi ilikuwa mstari wa
mbele kutumia kila aina ya hafla kuwaonya maafisa wafisadi katika
serikali kwamba wangefutwa kazi wakipatikana, lakini vitendo vilikuwa
vichache mno. Kadri Moi alivyoapa kupambana na ufisadi, ndivyo wanasiasa
na maafisa wakuu walivyoutekeleza bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kashfa za mabilioni ya pesa ikiwemo ya kihistoria ya Goldenberg zilikuwa
matunda ya ufisadi huo, mashirika ya kiserikali na taasisi za kifedha
ziliporomoka kutokana na viwango vya juu vya ufisadi na hatimaye uchumi
wa nchi karibu uporomoke kabisa. Wanasiasa na watu mashuhuri walitumia
pesa walizopora kufungua akaunti za benki na kuwekeza nchi za ng’ambo
kuficha maovu yao.
Wataalamu wa uchumi na watetezi wa
haki za binadamu wanasema sawa na serikali ya Moi, Rais Kenyatta
amemwiga Moi kwa kutoa ahadi kila uchao za kupambana na ufisadi, lakini
bila kuchukua hatua zozote. Maafisa waliohusishwa na kashfa mbalimbali
wangali wanashikilia nyadhifa za juu katika serikali huku Tume ya
Kupambana na Ufisadi (EACC), Idara ya Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka ya Umma (DPP) wakisema wanaendeleza uchunguzi, ambao matunda
yake hayaonekani.
Ufisadi umerudi katika taasisi
nyingi, jambo linalonyima serikali mapato huku wafanyabiashara wakubwa
wakubwa wakikwepa kulipa kodi. Japo serikali ya Jubilee imekuwa ikiapa
kuwafuta kazi maafisa wafisadi, kufikia sasa waliotajwa hawajachukuliwa
hatua na hali inaendelea kwenye mkondo sawa na ilivyokuwa chini ya Moi.
KUBADILISHA SHERIA KIHOLELA
Ilikuwa kawaida kwa serikali ya Moi
kutumia bunge kubadilisha baadhi ya vifungu vya sheria ili kutimiza
malengo ya muda mfupi au iliyohisi ilikuwa kizingiti kuafikia malengo ya
serikali na ya kibinafsi bila kujali maslahi ya mwananchi wa kawaida.
Kwa sababu ya kuwa na idadi kubwa ya wabunge wa KANU, mabadiliko hayo
yalipita kwa urahisi na athari zake kujitokeza baadaye.
Kwa miaka miwili ambayo imekuwa
mamlakani, Serikali ya Jubilee imependekeza mabadiliko kadhaa tata ya
kisheria, ikiwemo sheria za mawasiliano na usalama ambazo upinzani na
baadhi ya wanaharakati walipinga. Hata hivyo serikali imetetea
mabadiliko ya kisheria ikisema yanalenga kuimarisha huduma na usalama
kwa Wakenya.
KUVURUGIKA KWA SEKTA YA KILIMO
Chini ya uongozi wa Moi, sekta ya
kilimo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya, ilivurugika.
Kilio kilitanda kote miongoni mwa wakulima wa kahawa, chai, sukari na
wafugaji wa ng’ombe wa maziwa. Bei zilishuka na hata malipo kukosekana,
hali iliyofanya uzalishaji wa mazao kushuka kwa kiwango kikubwa hivi
kwamba hadi sasa sekta ya kilimo ingali chini. Viwanda vya mazao ya
kilimo vilifungwa kwa mfano KCC cha maziwa na KMC cha nyama huku
mashirika ya wakulima yakiporomoka.
Kibaki alipochukua uongozi 2003
alifanya bidii kuinua kilimo kwa kufufua viwanda vya bidhaa za kilimo,
mashirika ya wakulima na kuweka sera za kuwatia wakulima moyo kama vile
kupunguza viwango vya ushuru wa pembejeo na mazao.
Lakini chini ya utawala wa Jubilee,
sekta ya kilimo imeonekana kurudia hali ya enzi za Moi ambapo ushuru wa
juu kwa pembejeo na bidhaa za kilimo umerudi, uingizaji wa bidhaa za
kigeni kama vile sukari kimagendo umeongezeka na sasa sekta za chai,
sukari, kahawa miongoni mwa zingine zinakumbwa na matatizo si haba ya
gharama za juu za uzalishaji, bei duni kwa mazao na hatari ya sekta hizi
kuporomoka. Kilio cha wakulima wapunguziwe viwango vya ushuru na kuwepo
kwa sera za kuhakikisha wananufaika na bidii yao.
HAFLA NYINGI ZA RAIS
Chini ya utawala wa chama cha Kanu,
Moi alikuwa akiongoza hafla nyingi karibu siku moja. Wapinzani
walimlaumu kwa kuingilia kazi ambazo angeachia mawaziri au maafisa wa
vyeo vya chini kama alivyofanya Kibaki chini ya utawala wake wa miaka
10. Kitengo cha habari cha Rais kilihakikisha hafla hizo zilipewa
umuhimu na vyombo vya habari.
Viongozi wa Jubilee wamerejelea
mtindo huo ambapo Rais Kenyatta amekuwa akiongoza hafla mbalimbali
karibu kila siku, ambazo zinagharimu pesa nyingi za mlipa ushuru
kutokana na maandalizi yake ya hadhi.
POLISI WENYE NGUVU KUPITA KIASI
Chini ya utawala wa Moi, maafisa wa
polisi waliogopewa kama shetani kwani walihangaisha raia jinsi
watakavyo. Utawala wa sheria ulikuwa kama ndoto kwa wengi na Wakenya
hawakuwa na uhuru wa kuendelea na shughuli zao kwa njia huru. Polisi na
maafisa wa ujasusi waliwaandama watu waliohisi walikuwa tisho kwa
serikali.
Katika kurudisha hali ya enzi hizo,
serikali ya Jubilee imechukua hatua zinazolenga kuhakikisha polisi na
maafisa wa ujasusi wanaweza kusikiliza mawasiliano ya watu binafsi,
kuwapa kibali cha kuzuiliwa washukiwa kwa muda mrefu bila kuwashtaki
miongoni mwa masuala mengine.
UKABILA KUONGEZEKA SERIKALINI
Serikali ya Moi ililaumiwa pakubwa
kwa kupalilia ukabila kwa kuwapa kazi watu kutoka baadhi ya jamii.
Kutokana na hili, watu waliohitimu walikosa kazi kwa sababu ya makabila
yao.
Japo kuna sheria ya kuhakikisha
usawa katika nyadhifa za serikali, Jubilee imelaumiwa kwa kutenga baadhi
ya jamii nchini katika uteuzi na uajiri wa maafisa wa serikali huku
jamii mbili zikichukua idadi kubwa ya ajira za juu serikalini na katika
taasisi za umma.
KUTEMBELEWA IKULU
Ilikuwa ni kawaida kwa Moi
kutembelewa Ikulu na wajumbe na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali
ya nchi. Hii ni mbinu iliyopingwa vikali na upinzani ukitilia shaka
lengo la ziara hizo. Mtindo huu ulimalizika chini ya utawala wa Kibaki
ambaye ilikuwa nadra kutembelewa na wajumbe Ikulu.
Chini ya Jubilee ziara za Ikulu
zimerudi ambapo Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akipokea wajumbe kutoka
maeneo tofauti au vikundi vya watu Ikulu.
swahilihub@ke.nationmedia.com
No comments:
Post a Comment