Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro akiongea na viongozi wa Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Salaam jana (Jumanne,
Feb 24, 2015). Kulia kwake ni Naibu Waziri Ummy Mwalimu na kushoto kwake
ni Mwenyekiti wa Tume hiyo Wakili Bahame Tom Nyanduga na Katibu
Mtendaji Bi. Mary Massay. Waziri alifanya ziara katika ofisi za Tume
hiyo kubadilishana mawazo na uzoefu.
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro, Naibu wake Ummy Mwalimu
wakiwa katika picha ya kumbukumbu na viongozi wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Salaam jana (Jumanne, Feb 24,
2015). Waziri alifanya ziara katika ofisi za Tume hiyo kubadilishana
mawazo na uzoefu. Picha na Farida Khalfan, Wizara ya Katiba na Sheria.
Na Martha Komba
Serikali
imeiagiza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRGG) kuibua
masuala yanayoathiri uzingatiaji wa haki za binadamu ili hatua stahiki
zichukuliwe na hivyo kuboresha misingi ya haki na utawala bora nchini.
Akizungumza
na viongozi wa Tume hiyo jana (Jumanne, Feb. 24, 2015) jijini Dar es
Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Asha–Rose Migiro alisema
Serikali ina wajibu wa kuzingatia haki za binadamu katika utekelezaji wa
majukumu yake na hivyo na hivyo ni muhimu kwa Tume kuibua na kutoa
taarifa juu ya masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Serikali
ina wajibu wa kufanya kazi kwa kuzingatia na kulinda haki za binadamu
ili wananchi waweze kuwa na amani katika nchi yao,” alisema Dkt. Migiro
katika mikutano wa viongozi wa Tume hiyo uliohudhuriwa Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Ummy Mwalimu. Waziri Migiro alikuwa katika ziara
ya kubadilishana mawazo na uzoefu na viongozi wa Tume hiyo.
Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilianzishwa mwaka 2000 na kuanza
kazi rasmi mwaka 2002 ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa ushauri kwa
serikali na vyombo vingine vya umma na vya sekta binafsi kuhusu haki za
binadamu na utawala bora.
Akizungumza
katika mkutano huo, Naibu Waziri alisema ni muhimu kwa Tume hiyo
kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu uzingatiaji wa haki za
binadamu na utawala bora kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano
ili kuwafikia wananchi wengi kwa kasi na haraka.
“Katika
nchi yetu suala la teknolojia ya mawasiliano na habari ni muhimu sana
ili kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa kasi na kwa haraka zaidi, ongezeni
kasi ya kuitumia,” Naibu Waziri aliwaambia viongozi hao walioongozwa
na Mwenyekiti wa Tume hiyo Wakili Bahame Tom Nyanduga.
Kwa
upande, Mwenyekiti wa Tume hiyo aliwashukuru Waziri na Naibu Waziri kwa
ziara yao kwa Tume na kuahidi kutekeleza maelekezo waliyopewa pamoja na
changamoto zilizopo.
Aidha,
Wakili Nyanduga alisema kuwa Tume yake ina mpango wa kuandaa programu
ya kuelimisha umma juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwa wao pia
wana haki ya kuishi.
“Kuwaua
watu wenye ulemavu wa ngozi ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa vile
wao pia wana haki ya kuishi,” alisisitiza Mwenyekiti huyo na kufafanua
kuwa Tume inaandaa mpango wa kuelimisha umma ili kukomesha mauaji hayo.
Pamoja
na Mwenyekiti wa Tume, mkutano huo ulihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti
Bw. Iddi Ramadhani Mapuri, Makamishna Tume hiyo Bw. Mohammed Khamis
Hamad, Dkt. Kevin Mandopi, Bi. Rehema Msabila Ntimizi, Bi. Salma Ali
Hassan, Katibu Mtendaji wa Tume Bi. Mary Massay na viongozi wengine wa
tume.
No comments:
Post a Comment