Sune Mushendwa
Kwa
miaka nenda rudi, wasanii wa kitanzania walikuwa na kilio kinachofanana.
Ungekaa pembeni bila kuwaona, ungedhani kutokana na mwangwi wa kilio
chao, anayelia ni mmoja. Hapana. Wote walikuwa [na pengine bado
wanaendelea kulia] kutokana na kunyonywa “jasho lao”.
Kimsingi “jasho” wanalolilia limekuwa ni soko na usambazaji. Kipaji
unacho na watu wanakubali kazi zako.
Tatizo
utaifikishaje kazi yako kwa mashabiki zako? Ni wazi kwamba unahitaji
msaada wa kimasoko na usambazaji. Kusema utaweza kufanya kila kitu peke
yako ni kujidanganya.Nani? Yupo wapi na utampa kazi zako kwa thamani
gani? Kilio chao kilianzia hapo.
Wengine
wakaamua kuachana na muziki [wengine muziki umewaacha wao] kutokana na
ukosefu wa soko la uhakika na kuona kadhaa ya kupanga foleni ukisubiri
“hela yako”.
Mabadiliko
ya masoko ya kazi za wasanii duniani kutoka kwenye mifumo ya
ki-analojia kwenda kwenye dijitali na pia kutoka katika mifumo ya vitu
kama CD mpaka kwenda kwenye matumizi ya simu na vikabrasha vingine vya
mikononi, kulimaanisha kwamba soko la wasanii wa kitanzania [na Afrika
kwa upana wake] lilikuwa linazidi kufifia. Hakuna tena shabiki anayetaka
kubeba furushi la CD. Inakuwaje?
Hapo
ndipo baadhi ya vijana wakaona fursa kuthibitisha kwamba penye tatizo
ndipo pa kukimbilia.Fursa ni kama dhahabu au almasi.Huwezi kuiokota
kando ya bahari ikiwa imetupwa ufukweni na mawimbi ya bahari. Wazo la
fursa likazaa Mkito.Com mahali ambapo wasanii sasa wanapumua na huku
changamoto pekee ni kuwashawishi mashabiki kupakua kazi zao kutoka
Mkito.Com. Kila mara shabiki anapofanya hivyo, msanii ananufaika na
kupata nguvu zaidi ya kuingia tena studio kunogesha mambo.
It’s a win win situation.
Sune Mushendwa [pichani juu] ni mwanzilishi-mwenza wa Mkito.Com.
Kujua
mengi zaidi nilimtafuta na kupiga naye story kidogo. Ameelezea mengi.
Nakukaribisha usome mahojiano yangu naye ili ujue yote ambayo umekuwa
ukitaka kuyajua kuhusu Mkito.Com .Twende pamoja;
BC:
Sune karibu sana ndani ya BongoCelebrity. Hii ni mara yako ya kwanza
hapa na bila shaka wasomaji wangependa kupata japo kwa kifupi tu
historia yako. Ulizaliwa wapi,ukakulia wapi na kusomea wapi na mambo
kama hayo?
SM:
Asante sana kwa kunikaribisha. Mimi nimekulia Arusha na ndipo niliposoma
pia. Baada ya sekondari nilienda kusoma chuo kikuu nchini Finland
ambako mama yangu ndipo anapotokea.
BC:
Wajasiriamali wengi ambao nimewahi kufanya nao mahojiano huniambia
kwamba waliamua kufanya wanachokifanya baada ya kukosa au kubughudhiwa
na kitu fulani.Huwa kuna kisa au mkasa nyuma ya pazia. Kwa upande wa
Mkito kuna kisa au mkasa wowote? Ilikuwaje mpaka ukasema Aha…Mkito
ikaanza? Na hili jina lilikuja namna gani?
SM:
Baada ya kutoka masomoni nilianzisha studio ya muziki Arusha.Lakini
tatizo kubwa lililoonekana moja kwa moja ni kwamba wasanii pamoja na
studio zinapata tabu sana katika kusambaza na kuuza kazi zao. Niliona
tunahitajika njia ya kuweza kusambaza muziki kirahisi na pia kuingiza
kipato kwa msanii. Baada ya research na maandalizi ya zaidi ya miaka 4
ndipo Mkito.com ilipozaliwa tarehe 30 April 2014.
BC: Mpaka sasa Mkito imefanikiwa kuwa na wasanii wangapi? Nini masharti ya msanii kujiunga au kuweka kazi zake katika Mkito?
SM:
Kuna wasanii takriban 600 waliojiunga mpaka sasa na wanaongezeka kila
siku. Masharti ya kujiunga ni marahisi, uwe umerekodi wimbo anghalau
mmoja wenye ubora. Baada ya hapo msanii anaweza kujitengenezea akaunti
yake kupitia tovuti www.mkito.com na
kupakia[upload] nyimbo zake mwenyewe. Msanii baada ya hapo anaweza
kufuatilia mauzo yake mwenyewe kupitia akaunti yake aliyoitengeneza.
BC:
Bado nikiwa katika swali au maswali ya wasanii. Msanii akishaingia
katika mkataba au makubaliano na ninyi, bado anakuwa na haki na uhuru wa
kuendelea kusambaza kazi zake katika platforms zingine kama vile
iTunes,Spotify,Google Play nk?
SM: Tunaamini kuwa kazi ya msanii ni mali yake pekee kwahivyo hatumzuii
msanii aliyejiunga nasi kusambaza kazi zake kwa njia yoyote nyingine
aipendayo. Kama huduma yetu ni bora basi tunaimani msanii mweyewe
atachagua kutumia huduma zetu siyo mpaka tumfunge kupitia mikataba.
BC:
Nilisoma mahali kwamba mlipoanzisha Mkito lengo lilikuwa kuwa na
watumiaji waliojiandikisha [registered users] milioni 1 katika mwaka wa
kwanza. Mpaka sasa mmefikia wapi katika lengo hilo?
SM: Nilishasoma hilo mimi pia lakini siyo ukweli kuwa lengo ni kufikisha
watumiaji milioni 1. Lengo ni kufikisha watumiaji waliyojiandikisha
laki 5 ndani ya mwaka moja. Tumekaribia nusu ya hiyo idadi mpaka sasa na
dalili zote ni kuwa tutafika na kuvuka hiyo idadi.
BC:
Kuna baadhi ya wasanii ambao nimeongea nao kuhusu huduma kama hii ya
Mkito na nyinginezo wanasema kwamba huduma hizi kimsingi zinawapunja au
kuwadhulumu kwa sababu hamuendi nao bega kwa bega katika matayarisho ya
muziki [kwa maana ya gharama na karaha zote za maandalizi] bali nyie
mnasubiri wapike kisha muwasaidie tu kupakua huku nanyi mkijitengenezea
faida. Unawaambiaje wasanii kama hao na kuna tofauti gani kubwa kati ya
wasambazaji wale wa zamani na nyie hapo?
SM:
Mkito.com ni kampuni ya usambazaji wa muziki na siyo studio ya kurekodi
au kampuni ya management. Kwa maana hiyo sisi faida tunaingiza katika
uuzaji wa muziki kupitia tovuti yetu tu. Kama tungehusika na kurekodi na
management ya wasanii basi tungedai makato kwenye mauzo yote kama ring
tones, CD, shows n.k. lakini kama nilivyosema faida yetu ni katika
uuzaji wa muziki tu.
Kuhusiana na tofauti ya Mkito.com na makampuni mengine; tangia mwanzo
tumehakikisha kuwa mauzo yote yanawekwa wazi ili msanii ajue muda wote
kuwa mauzo yake yakoje. Hili bado sijaona likifanyika na wengine ingawa
ni la muhimu sana. Inabidi kujiuliza madhumuni ya haya makampuni
kutokuweka mauzo wazi.
BC:
Kwa mtu ambaye hajui Mkito ni nini na angependa kufahamu zaidi na hata
kujiunga na huduma ya Mkito[nazungumzia mtu mtumiaji wa kawaida] ungempa
maelezo gani kwamba Mkito ni nini na nini ategemee pindi atakapoingia
Mkito.com?
SM:
Mkito.com ni huduma ya kwanza nchini ya kusambaza muziki kidigitali
ambapo mtu anaweza kupakua nyimbo kwa sh 250 tu kupita simu yake au
computer. Pia nyimbo zote zinapatikana bure lakini zinaambatanishwa na
matangazo mafupi ya kibiashara. Haya matangazo katika nyimbo za bure
ndiyo yanawalipa wasanii. Ni muhimu kujua kwa Watanzania wote kuwa ni
jukumu letu kulinda muziki wetu na unavyopakua nyimbo kupitia Mkito.com
unakuwa unauhakikia kuwa msanii analipwa kwa kazi yake na wewe pia
unasaidia kuuendeleza muziki wa Kitanzania.
BC:
Bila shaka kwenye biashara kama ya Mkito ambayo kwa ukaribu sana
inahusiana na tekinolojia za mitandaoni,matatizo hujitokeza.Kuna mtu
kushindwa kupakua[download] wimbo au nyimbo na kuna kero zingine
nyingi.Mkito mnashughulikiaje matatizo kama hayo? Na kimsingi ni
changamoto gani ambazo mnakabiliana nazo kila siku au mara kwa mara?
SM:
Kuna maelfu ya aina tofauti za simu na computer ambazo kila siku
zinatumika kupakua nyimbo Mkito.com. Sasa ni vigumu kuhakikisha kuwa
tovuti itafanya kazi na kila aina ya simu lakini kwa kiasi kikubwa sana
tumefanikiwa kutatua matatizo yanapojitokeza. Pia tunayo huduma kwa
wateja ili mtu akipata shida anaweza kutuandika barua pepe au kupiga
simu na tunamsaidia kutatua tatizo lake haraka.
BC:
Kwa upande wa muziki, wasanii,wasimamizi [managers] wao nk nikikupa
nafasi hii kuongea nao moja kwa moja ungewaambia nini au ungewapa
ushauri gani kuhusiana na suala zima la muziki nk?
SM:
Muziki ni biashara, wote tunafahamu hilo. Kwahiyo ninawakaribisha
wasanii wote kuja kujiunga Mkito.com tuwasaidie kutangaza, kusambaza na
kuuza muziki wao. Nafahamu kuwa wengi wanakuwa na wasiwasi kuwa
wataibiwa – hili siyo kweli kwa upande wa Mkito.com, labda
waliotutangulia. Kama nilivyokwisha sema kila kitu kinawekwa wazi na
kama wewe ni msanii mwenye kazi nzuri basi kuwa na imani kuwa unaweza
kujipatia kipato kizuri kutokana na mauzo ya muziki wako kupitia
Mkito.com
BC:
Shukrani sana kwa muda wako Sune. Nakutakia kila la kheri katika kazi
zako
Asante sana. Lakini na mimi nikuulize wewe swali moja. Je, umeshapakua
nyimbo ngapi mpaka sasa kupitia Mkito.com ili kuwapa support wasanii wa
Tanzania?
BC:
Mpaka leo,nimeshapakua nyingi.Sikumbuki idadi kamili. Lakini mchango
wangu zaidi ni kuwajulisha watumiaji wengine [wasomaji wangu kwa mfano]
juu ya kazi mpya za wasanii na wapi pa kuzipata.
Asante kwa swali zuri Sune.
No comments:
Post a Comment