Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Matukio
ya kutishia amani ya nchi na usalama wa raia yatapungua kama mabalozi
wa nyumba kumi watafanya kazi zao kwa uaminifu kwani wao ni viongozi wa
kwanza walio karibu na wananchi hivyo basi wanatakiwa kuwafahamu wakazi
wa maeneo yao.
Hayo
yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar, Vuai Ally Vuai wakati akifungua semina ya siku moja ya
uwezeshaji wa chama hicho kwa mabalozi (viongozi wa mashina) wa wilaya
ya Lindi mjini.
Vuai
alisema Balozi ni kiongozi wa kwanza anayetakiwa kujua idadi ya wakazi
wake, kazi wanazozifanya na majina yao kitendo ambacho kitasaidia
kuimarisha usalama wa eneo husika lakini miaka ya hivi karibuni wameacha
kufanya kazi hiyo kwa uadilifu na kuviachia vyombo vya dola pekee.
“Jukumu
la kulinda amani ya nchi na usalama wa taifa letu ni la kila mtu,
lakini hivi sasa kazi hiyo vimeachiwa vyombo vya dola pekee, mabalozi
fanyeni kazi ya kuwatambua wakazi wa maeneo mnayoishi hii itasaidia
kumtambua mualifu pale atakapofika katika eneo lenu”, alisema Vuai.
Alisema
kikao cha kwanza cha CCM ni kikao cha shina hivyo basi mabalozi ni
viongozi wa muhimu ndani ya shina wanatakiwa kutetea ilani ya uchaguzi
ya mwaka 2010 na kutowaachia viongozi wakuu wa chama pekee kufanya kazi
hiyo.
Vuai
alisisitiza, “Muwe na uthubutu wa kujibu hoja potofu za wapinzani na
kutokubali wawapotoshe wananchi juu ya mafanikio yaliyofanywa na
Serikali. Kipindi cha uchaguzi kikifika endeleeni kuwahimiza na
kuwasimamia wananchi wakapige kura ili wasipoteze haki yao ya msingi ya
kupiga kura”.
Aliwataka
mabalozi hao kuhakikisha wakati wa kujiandikisha katika daftari la
kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo
mwakani wawahimize wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha majina yao.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia
wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete alisema mabalozi ni msingi na
nguzo ya chama bila ya mabalozi chama hakiwezi kwenda vizuri ni kama
vile binadamu anaweza kuwa na kila kitu lakini kama hana miguu hawezi
kutembea.
Aliwapongeza
kwa ushindi walioupata wakati wa uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa
Serikali za mitaa na kusema kuwa upendo na mshikamano ni msingi wa
ushindi na usiri na uadilifu ni nyenzo muhimu katika utendaji wao wa
kazi.
“Katika
semina hii mtafundishwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi na
wajibu wenu kwa Chama na Jamii inayowazunguka hivyo basi muwe wasikivu
na kuyashika yale mtakayofundishwa na watoa mada”, alisisitiza Mama
Kikwete.
Akiongea
kwa niaba ya wajumbe walioshiriki semina hiyo Rashid Thabit kutoka kata
ya Rahaleo alishukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa
yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi.
“Tunakushukuru
MNEC kwa ajili ya kuandaa mafunzo haya ambayo yametupa uelewa na wajibu
na kazi zetu kama mabalozi. Uwepo wako wakati wa uchaguzi uliopita
ulitufanya tukashinda kwani tulishiriki pamoja nawe katika kampeni za
kuwanadi wagombea wetu”.
Nawaomba
wajumbe wenzangu tusibweteke na ushindi huu bali tuongeze kasi na bidii
na kuweza kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo
mwakani ili tuweze kulikomboa jimbo la Lindi mjini kutoka mikononi mwa
Chama Cha Wananchi (CUF)”, alisema Thabit.
Semina
hiyo ya siku moja iliyohudhuriwa na wajumbe 993 kutoka kata zote 18 za
wilaya hiyo iliandaliwa na Mama Kikwete ambaye aliwaahidi mabalozi
kuwapa mafunzo hayo ili wajue majukumu yao ya kazi. Mada zilizojadiliwa
ni kazi na wajibu wa mabalozi na katiba mpya iliyopendekezwa.
No comments:
Post a Comment