Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mjini (CCM) na mfanyabiashara
maarufu nchini, Mohammed Dewji ameshinda tuzo ya kiongozi bora
aliyejitolea kwa kiasi kikubwa katika jamii na kuleta mabadiliko Afrika
kwa mwaka 2014.
Tuzo hiyo iitwayo African Philanthropist of the
year Award 2014 ilitolewa na jarida la uongozi la Uingereza, jijini
Dubai hivi karibuni katika Jukwaa la Viongozi wa Afrika.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa jarida hilo, Dk Ken Giami
alisema wataalamu waelekezi walimchagua Dewji kuwa mshindi kutokana na
uongozi bora katika Kampuni yake ya Mohammed Enterprises.
Alisema kigezo kingine kilichompa ushindi ni namna
anavyojihusisha na kazi mbalimbali za kijamii. Dk Giami ambaye pia ni
mhariri mkuu wa jarida hilo, alisema uwezo wake wa uongozi katika nyanja
za biashara, michezo na uwakilishi wa wananchi bungeni vimemfanya
mfanyabishara huyo kupata uzoefu wa kutosha na hamasa ya kujitolea.
“Mchango wako katika elimu ni sehemu kubwa ya
mafanikio ukiwa mbunge hususan kwa kuendeleza ujenzi wa shule mbili hadi
12, pamoja na kujitolea Sh520 milioni katika kuendeleza sekta hiyo,”
alisema Dk Giami katika barua aliyomwandikia Dewji kuhusu ushindi huo.
Alisema mfanyabishara huyo pia amekuwa akisaidia
sekta ya afya kwa ushirikiano na Taasisi ya Bilal Muslim Mission ya
Tanzania kwa kuwaleta madaktari waliowafanyia upasuaji wagonjwa macho na
179 kupata miwani.
Alisema kiongozi huyo ambaye pia mwaka jana
alitajwa na jarida la Forbes la Marekani kuwa tajiri wa 38 Afrika,
alisaidia jimbo lake kusambaza maji safi na salama kwa kuchimba visima
vingi vya maji.
Dk Giami alisema Afrika linakuwa kwa kasi kiuchumu
na kiuvumbuzi, lakini mafanikio hayo yatakuwa na manufaa iwapo kutokuwa
na maendeleo shirikishi.
No comments:
Post a Comment