Mkurugenzi
Mtendaji wa Uvinza FM Radio, Nuru Kalufya akisimamia usajili wa
washiriki wa mafunzo ya Maadili, Jinsia na Kuandika Habari za Migogoro
yaliyoanza katika kijiji cha Uvinza, wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
tarehe 24 Septemba hadi 01 Oktoba 2014.
Na Mwandishi wetu, Uvinza.
Imethibitishwa
kwamba mfumo dume ulioota mizizi katika jamii kwa kisingizio cha mila,
desturi na dini unachangia kwa kiasi kikubwa katika unyanyasaji wa
mtoto wa kike na mwanamke nchini.
Hayo
yalithibitishwa na washiriki wa mafunzo ya maadili na jinsia
yanayofanyika katika kijiji cha Uvinza mkoani Kigoma wakati wakichangia
mada ya Jinsia na Vyombo vya Habari iliyowasilishwa na mkufunzi kutoka
Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Bi Rose
Haji Mwalimu.
Mshiriki
kutoka Loliondo Joseph Munga ambae alizungumzia jinsi gani mfumo dume
mgando unavyonyima haki za mtoto wa kike wa Kimasai, alisema kwamba
mtoto wa kike hapaswi kwenda shule, kuna kiwango cha juu cha shinikizo
la ndoa za utotoni, ukeketaji na wanawake kutokuwa na mamlaka ya kufanya
maamuzi.
“Ubaguzi
unaanza katika familia, mtoto wa kike hana haki ya kuchagua mume
anayemtaka au lini aolewe. Mtoto huyo huyo ni lazima akeketwe kwa sababu
mtoto wa kike asiyekeketwa anaonekana ni laana katika familia na hawezi
kupata mume. Kutokana na sababu hizo watoto wa kike huridhia kukeketwa
ili waondoe laana hiyo lakini pia kwa kushinikizwa na wazazi wa kike.”
Hadi
leo haijathibitishwa ni laana gani huwapata wasichana wasiokeketwa kwa
maana kuna baadhi yao ambao hawakukeketwa, wameolewa na wanaendelea na
maisha ya kawaida.
Mshauri
na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa
Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya
Maadili, Jinsia na Kuandika Habari za Migogoro katika maandalizi ya
uchaguzi mkuu 2015.
Akizungumzia
kuhusu uwakilishi kufikia 50/50 ifikapo mwaka 2015, Munga alisema
kwamba bado kuna changamoto kubwa kwa mwanamke wa Kimasai kusimama na
kugombea nafasi za uongozi kutokana na wanawake kutopewa nafasi ya kutoa
maamuzi katika jamii ya Kimasai. Mathalani, moja ya tabia za mfumo
dume mgando katika jamii hiyo ni mila na tamaduni za Kimasai ambapo
mwanamke haruhusiwi kushiriki katika uongozi wa rika “laigwanang” kwa
sababu jamii ya kimasaia inamlinganisha mwanamke na kumchukulia kama
mtoto mdogo “nagara, ngara au ngarai”.
“Nafasi ambazo mwanamke anaweza kufaidika nazo ni zile za kuteuliwa tu basi,” alifafanua Munga.
Naye
mshiriki kutoka kisiwani Tumbatu Ali Khamis alisema kwamba katika jamii
yao mwanamke hana haki ya kutoa maamuzi katika ngazi ya familia na
haruhusiwi kuhudhuria vikao vya harusi na misiba. Katika uongozi hali
pia hairidhishi.
“Katika
kisiwa cha Tumbatu viongozi wote wa ngazi za juu katika siasa ni
wanaume. Ukianzia Afisa Tawala, masheha na madiwani ni wanaume, yupo
mwanamke mmoja tu ambae ni wa kuteuliwa,” alisema Khamis.
Pemba
ina majimbo 18 lakini hakuna mwanamke wa kuchaguliwa kisiasa wakati huo
huo kisiwa cha Unguja ambacho kina majimbo 32 kuna wanawake watatu tu
wa kuchaguliwa.
Mshauri
na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO akisisitiza jambo katika
mafunzo yanayowashirikisha waandishi wa habari na watangazaji kutoka
redio jamii nane nchini.
Mshiriki
mwingine kutoka Uvinza mkoani Kigoma Leah Kalokoza alisema kwamba
unyanyasaji kijinsia ni wa kiwango cha juu katika jamii inayouzunguka
mji huo. Alisema kuwa mgawanyo wa kazi katika familia hauna uwiano kati
ya mwanamke na mwanaume maneno ambayo pia yalithibitishwa na Balozi wa
Barabara ya Kasulu Bi. Tabu Ramadhani.
“Wanawake
ndio wanaotafuta riziki hususan kuvuna chumvi kazi ambayo ni ngumu
sana, kulima na kulea watoto. Wanaume kazi yao ni kuuza chumvi hiyo,
kukaa magengeni na kula hotelini wakati watoto nyumbani hawana chakula,
kwa kweli wanatunyanyasa waume zetu.”
Tegemeo
kubwa la kipato cha Uvinza ni chumvi pamoja na kwamba kwa kiasi kikubwa
kipato hicho kimeshuka baada ya kiwanda hicho kubinafsishwa na
mwekezaji mwenye asili ya Kiasia.
Akizungumzia
uhuru wa kujieleza, Leah Kalokaza alisema kwamba wanawake hawaruhusiwi
kuwasiliana na vyombo vya habari bila idhini ya waume zao. Tamko la
Dunia la Haki za Binadamu kuwa na Haki ya Uhuru wa Kujieleza Ibara ya
19, linasisitiza uhuru wa kujieleza ni haki ya kila mtu, awe mwanamke au
mwanamume.
Kutoka
Mpanda mkoani Rukwa wanawake wananyanyaswa kwa kunyimwa elimu, kutokuwa
na haki ya kumiliki kama ilivyo katika jamii nyingine na pia utu wao
hudhalilishwa pale mabango katika nyumba za kulala wageni huwa yanakuwa
na picha au ujumbe dhahiri wa mfumo dume.
Mambo
mengine yanayochangia udhalilishaji wa wanawake ni nyimbo mbalimbali
ambazo humsifu mwanamume na kumkashifu mwanamke hususan sehemu za
Usukumani.
“Kwa
mfano, kuna Wimbo unaosema, ‘kuzaa mtoto wa kiume jamii yote
inafurahia, kuzaa mtoto wa kike ni maandalizi ya sherehe. Hii inaonyesha
ni kwa namna gani mwanamke katika tamaduni za Kisukuma hana hadhi hata
mbele ya mtoto aliyemzaa mwenyewe,” alisema Anatory John.
Mkoa
wa Shinyanga umekumbwa na wimbi kubwa la mauaji ya vikongwe wanawake
kwa tuhuma za uchawi, lakini ikija kwenye uganga wa jadi hawatambuliki.
“Waganga
wengi wa Kisukuma ni wanaume kwa imani kwamba wanawake hawana uwezo wa
kuzungumza na mizimu au miungu”, alielezea Anatory.
Vyote
hivyo ni viashiria vya mfumo dume au mawazo mgandoyanayoendeleza tabia
ya kumwona mwanamke ni mtu duni na mwanamume ni mtu mwenye uwezo wa
pekee.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea kupata darasa kutoka Mkufunzi wao Bi. Rose Haji Mwalimu Uvinza mkoani Kigoma.
Kipengele
cha Vyombo vya Habari katika Itifaki ya SADC kuhusu Jinsia na maendeleo
kinaazimia kuhakikisha kuwa jinsia inaingizwa katika habari,
mawasiliano na sera za vyombo vya habari, mipango, vipindi, sheria na
mafunzo kulingana na Itifaki ya Utamaduni, Habari na Spoti.
Azimio
la Jinsia na Maendeleo lililotolewa na Viongozi wa Umoja wa Maendeleo
Kusini mwa Afrika au Serikali (SADC) linasisitiza uwakilishi wa uongozi
katika ngazi ya maamuzi 50/50 ifikapo mwaka 2015.
Warsha
ya Maadili na Jinsia inalenga kuwapa uwezo waandishi na watangazaji wa
redio za jamii nchini kuandika habari zinatoa changamoto za
mfumodume/mgando na matumuzi ya Lugha nyepesi inayohusisha jinsia zote
bila kubagua hasa katika kipindi hiki tunakoelekea katika uchaguzi wa
serikali za mitaa na uchaguzi wa raisi mwaka 2015.
Warsha hii ya siku nane ilijumuisha waandishi wa habari wa redio jamii 48 kutoka redio 8 za jamii Tanzania Bara na Visiwani.
Mradi
huu unatekelezwa kwa pamoja kati ya UNESCO na Vyombo vya habari Jamii
chini ya mtandao wa COMNETA na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP.
Washiriki wa mafunzo ya Maadili na Jinsia katika vyombo vya habari wakiwa katika vikundi kazi.
Mshiriki
wa mafunzo kutoka Redio Loliondo FM, Joseph Munga akichangia mada ya
Jinsia na vyombo vya Habari katika mafunzo ya siku nane ya kuzipa uwezo
redio jamii kuandika habari chanya cha uchaguzi na migogoro.
Mshiriki
kutoka Tumbatu FM Radio Kisiwa cha Tumbatu, Unguja Ali Khamis
akizungumzia changamoto za mfumo dume na mawazo mgando yanayodumaza
maendeleo ya mwanamke.
Pichani
ni mshiriki na mwandishi wa habari Uvinza FM Radio, Uvinza- Kigoma Leah
Karokaza akichanganua masuala yanayoendeleza unyanyasaji wa kijinsia
wilayani Uvinza.
Anatory John kutoka Baloha FM Radio, Kahama akichanganua baadhi ya misemo na nyimbo zinazomdhalilisha mwanamke.
“Mabango
yanayotundikwa katika nyumba za kulala wageni yanadhalilisha sana
wanawake”, ndivyo asemavyo Sharifa Selemani kutoka Mpanda FM Radio,
Mpanda mkoani Rukwa katika picha.
Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa mradi wa kuzipa uwezo uwezo redio jamii katika mchakato wa uchaguzi mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment