UCHUMI WETU :SEKTA BINAFSI YAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA CHINA - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 26 June 2014

UCHUMI WETU :SEKTA BINAFSI YAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA CHINA

 
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kushoto) akielezea jambo kwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Prof. Lucian Msambichaka (katikati) na Mkurugenzi Mstaafu wa TIC na pia Balozi wa heshima wa Botswana hapa nchini, Eng. Emmanuel Ole Naiko wakati wa kongamano la pili la biashara kati ya Tanzania na China lililomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
 
Na Mwandishi Wetu-Dar Es Salaam
Sekta binafsi nchini imekaribisha wawekezaji kutoka China kuwekeza nchini kwa faida ya pande zote mbili.Akiongea na waandishi wa habari mwishoni mwa kongamano la pili la biashara kati ya Tanzania na China Jumatano wiki hii jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi  Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye alisema taasisi hiyo inakaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo katika juhudi za kufikia maendeleo endelevu hapa nchini.
“Sisi kama sekta binafsi tunasisitiza uwekezaji mzuri unaolenga kuiendeleza Tanzania...tunawakaribisha wawekezaji hawa kuja kufanya kazi hapa,” alisema.Kongamano hilo lilishirikisha kampuni zaidi ya 100 kutoka China na kampuni zaidi ya 120 za kitanzania.Hadi sasa China imesajili miradi 522 TIC yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2.4 ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 77,335.
Hata hivyo, Bw. Simbeye aliwaambia waandishi kuwa uwekezaji huo bado ni mdogo ukilinganisha na ukubwa wa uchumi wa taifa hilo.“Tunahitaji uwekezaji wao ufikie dola za kimarekani bilioni 5 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” alisema.Alisema sekta binafsi inapenda waje kuwekeza zaidi katika sekta ya viwanda na siyo kutumia fursa waliyopewa na watanzania kuja kuuza tu bidhaa zao.
Pia alisema wanapokuja kuwekeza ni vema wakatumia fursa hiyo kuwasaidia watanzania kupata ujuzi na teknolojia kupitia miradi ya ushirikiano (ubia) ili taifa liweze kupiga hatua. Alisema taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na wawekezaji hao kutoa msaada na mwongozo wowote utakaohitajika ili kuendeleza miradi watakayotaka kuanzisha hapa nchini.
“Tunazidi kupigania mazingira bora ya biashara ambayo yanaendelea kuboreshwa hivyo wawekezaji wa ndani na nje wachangamkie fursa zilizopo,” alisema.Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Bw. Raymond Mbilinyi alisema Tanzania imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya biashara ambayo yanavutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuja kuwekeza  kwa faifa ya nchi na wawekezaji.“Mazingira yetu ya kufanya biashara yameboreshwa sana na tunaendelea na juhudi kuyaboresha zaidi,” alisema.
Alisema katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Tanzania inaendelea kupambana na changamoto zinazokabili mazingira ya kufanya biashara.Alisema changamoto hizo ni pamoja na kuzidi kuboresha mazingira ya uanzishaji biashara na upatikanaji wa ardhi ili wawekezaji wasitumie muda mwingi.
“Maeneo mengi hayajapimwa hapa nchini,hivyo serikali inaendelea kulifanyia kazi jambo hilo ili wawekezaji wasipate usumbufu wa ardhi ya kuwkeza,”alisema.Pia serikali inaendelea kupunguza mianya ya rushwa ambayohuongeza gharama za kufanya biashara na kuwakatiza wawekezaji kuja kuwekeza.
Alisema TNBC kama chombo kinachokutanisha sekta binafsi na umma kinaendelea kuangalia kero na maeneo yanayofanya mazingira ya biashara na uwekezaji kutokwenda vyema ili kuibadilisha Tanzania.
Kongamano hilo la siku tatu lilofunguliwa na Makamu wa Rais wa China Bw, Li Yuanchao liliandaliwa na TIC kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Baraza la Biashara China Afrika (CABC) na kudhaminiwa na Stanbic Bank Tanzania.

No comments:

Post a Comment