MABOMBA YA GESI YASHUSHWA :NAIBU WAZIRI MHE. KITWANGA APOKEA SHEHENA YA MWISHO YA MABOMBA YA GESI BANDARI YA MTWARA. - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Friday 7 February 2014

MABOMBA YA GESI YASHUSHWA :NAIBU WAZIRI MHE. KITWANGA APOKEA SHEHENA YA MWISHO YA MABOMBA YA GESI BANDARI YA MTWARA.


Naibu Waziri Mhe. Charles Kitwanga (wa pili kutoka kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Wilman Kapenjama Ndile, (wa kwanza kulia) wakipata   maelezo kutoka kwa mtaalamu Abshakim Marunda kuhusu namna kisima cha  gesi cha nchi Kavu kinavyofanya kazi. 
Kwa mujibu wa Maelezo ya Mjiologia Mwandamizi wa TPDC Bw.George Ngwale hayupo pichani ameeleza kuwa, Mnazi Bay ina jumla ya visima vitano kati ya hivyo visima vine vina gesi  inayochimbwa na kisima kimoja kikavu. 
Aidha gesi inayopatikana katika  eneo hili inauzwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao wanatumia  kuzalisha umeme unaosambazwa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Wa kwanza  kushoto ni Katibu wa Mhe. Naibu Waziri Bw. Mjengwa Ngereja.

Na Asteria Muhozya, Mtwara
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Mhe. Charles Kitwanga, amepokea Shehena ya mwisho ya mabomba ya gesi katika bandari ya Mtwara na kueleza kuwa, ujio wa miundo mbinu hiyo ni neema kwa uchumi wa Tanzania.
Aliongeza kuwa, hiyo ni hatua kubwa katika kufikia malengo tarajiwa ikizingatiwa kwamba, kukamilika kwa mradi huo kutachochea na kufungua njia mbalimbali za uchumi unaoendana na sekta ya gesi na mafuta.

“Ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha gesi ni jambo jema kwa Tanzania, tunataka kuingia katika uchumi wa kati wa dola elfu tatu au karibu ya hapo, tunataka pato la mtanzania liongezeke. Sasa bila kuwa na umeme haya yote hatutayafikia. Gesi itazalisha mengi, tunataka tufikie lengo letu. Alisema.’’ Mhe. Kitwanga.
Aidha, aliongeza kuwa, kuzalishwa kwa gesi  na kusambazwa katika maeneo mbalimbali chini kutasaidia kufungua fursa nyingi ikiwemo  kuongezeka kwa viwanda ambavyo vitakuwa na uhakika  wa kupata umeme unaotokana na gesi.
Vilevile, alieleza kuwa, mbali na matumizi ya viwandani gesi inatarajiwa kutumiwa katika mahitataji mbalimbali yakiwemo matumizi ya majumbani.
 “Nataka kuwaeleza wana Mtwara, si kwamba gesi itachukuliwa yote, hapana. Tunachotaka kufanya ni kuisambaza maeneo mbalimbali lengo letu ni kukuza uchumi wetu kwa kutumia gesi hata Mtwara viwanda vitajengwa na fursa mbalimbali zitakuwepo”. Alisema.
Akieleza mafanikio ambayo yamekuwepo kutokana na shughuli za gesi kutumia bandari ya Mtwara, Meneja wa Bandari Bw. Absalim Bohella alieleza kuwa, ujio wa gesi na mradi unaotekelezwa Mkoani humo umekuwa neema kwa bandari hiyo kutokana na kuongezeka kwa mapato yanayotokana na bandari hiyo pia  kutumiwa kwa shughuli mbalimbali za gesi.
Aliongeza kuwa, tayari bandari ya Mtwara imevuka malengo ya ukusanyaji
mapato waliojiwekea ambapo hadi sasa tayari zaidi ya Tsh. Milioni mia tano kimekusanywa. 
Aidha, aliongeza kuwa, mradi wa gesi umewaongezea watumishi wa bandari hiyo ujuzi kutokana kufanya shughuli tofauti tofauti zinazohusiana na gesi ikiwemo upakuaji wa bidhaa zinazopitia katika bandari hiyo kwa shughuli.
“Bandari bila rasilimali watu si kitu. Kwa wafanyakazi waliobobea wamepata ujuzi zaidi na sasa wanao uwezo wa kuhudumia shughuli zote za bandari”. Aliongeza.
Akielezea hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa katika ujenzi wa miundombinu ya gesi, Mtaalamu wa Masuala ya Gesi na Msimamizi Mkuu wa Mitambo ya Kusafisha Gesi Mhandisi Sultan Pwaga alieleza kuwa, shughuli za uwekaji mabomba ya gesi unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2014 ambapo pia inatarajiwa mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu shughuli za usimikaji mitambo utakamilika.
 Vile vile, ameongeza kuwa, shehena hiyo iliyopokelewa katika bandari ya Mtwara ni ya mwisho lakini mabomba ya mwisho ya mradi yatapokelewa tarehe 10 Februari, 2014 katika bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, aliongeza kuwa, miundombinu hiyo ndio kichocheo cha gesi asilia
na lengo la mradi huo ni kuhakikisha kuwa, mitambo inajengwa mahali ambapo gesi asilia inachimbwa.
Mbali ya kupokea Shehena za mabomba ya mwisho ya gesi, Mhe. Kitwanga
ametembelea eneo la Mnazi Bay ambako gesi asilia na kuuzwa katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo shirika hilo linaitumia gesi hiyo kuzalisha umeme kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Vilevile, Mhe. Kitwanga alitembelea katika eneo la Madimba kunakojengwa
kambi za wafanyakazi na panapotarajiwa kujengwa mitambo ya kusafisha gesi.

No comments:

Post a Comment