MAGAZETINI : MASHEIKH WASISITIZA UMOJA NA AMANI UWEPO NDANI YA NCHI YETU YA TANZANIA - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 15 January 2014

MAGAZETINI : MASHEIKH WASISITIZA UMOJA NA AMANI UWEPO NDANI YA NCHI YETU YA TANZANIA

Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (kushoto), Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik (kulia), wakiwa kwenye sherehe za Maulid kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) zilizofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam juzi usiku. Picha na Venance Nestory.
Dar es Salaam/Mikoani. Viongozi mbalimbali wa siasa na Kiislamu nchini, wamehimiza amani, umoja, mshikamano wa Watanzania ili kuliepusha taifa na balaa la kupoteza amani.
Walisema hayo katika maadhimisho ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyofanyika juzi usiku.
Rais Mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliwataka watu wa dini zote kuondoa tofauti zao ili kudumisha amani iliyopo nchini kwa muda mrefu na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban bin Simba amewataka Waislamu nchini kuepuka migogoro ndani ya misikiti inayoweza kuwagawa.
Mufti
Akihutubia mhadhara wa kitaifa wa Waislamu uliofanyika kwenye Viwanja vya Stendi ya Ujiji, Kigoma, Mufti Simba aliwataka waumini wa dini hiyo kuepuka migogoro ndani ya misikiti inayoweza kuwagawa na kuzusha vurugu miongoni mwao.
Alisema migogoro na vurugu ndani ya misikiti imesababisha Waislamu kukosa nguvu na umoja miongoni mwao na kujikuta wakipoteza fursa ya kupiga hatua za maendeleo kwa kujenga miundombinu ya kijamii kama vile shule, vyuo vikuu na hospitali.
“Ninawaasa Waislamu kuwa makini na baadhi ya watu wanaotaka kutugawa kwa masilahi yao binafsi. Tuepuke sana migogoro baina yetu ndani ya misikiti, wale wanaouza viwanja vya misikiti na mali za Waislamu hawana budi kuacha mambo hayo mara moja kwa vile ndiyo kiini cha migogoro mingi.
“Tujifunze kwa wenzetu Wakristo ambao kila wanapopata viwanja, huvitumia kujenga miundombinu ya shule, vyuo na hospitali ambazo mwishowe zinatusaidia hata sisi Waislamu kupata maarifa. Hapa ndipo tunapotakiwa tujifunze kufanya mema ndani ya jamii zetu kwa faida ya taifa na Waislamu wenzetu.”
Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Jongo aliwataka Waislamu kuacha kulalamika kwamba Serikali inawakandamiza Waislamu na kuwapendelea Wakristo akisema jambo hilo si kweli.
“Waislamu tumekuwa tukilalamika kwamba kuna mfumo-kristo unaofanya kazi ndani ya Serikali na utawala wa nchi yetu. Hizi tuhuma si za kweli na hazipo kabisa. Zaidi kinachotugharimu sisi Waislamu ni kuendekeza migogoro baina yetu na kufanya mambo yasiyo ya kistaarabu katika Jamii,” alisema Sheikh Jongo.
Alisema baadhi ya kesi zilizopo mahakamani zilizofunguliwa na Waislamu dhidi ya wenzao ni dalili ya kushuka kwa maadili na hivyo kuwa kichocheo cha kudumaza maendeleo ya Waislamu.
Pia alitaja ugomvi unaotokea ndani ya misikiti kuwa ni miongoni mwa mambo yasiyokubalika katika jamii ya Kiislamu.
Mwinyi
Akizungumza kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Rais huyo Mstaafu alisema ili kudumisha umoja wa muda mrefu wa Watanzania, ni vyema watu wa dini zote wakashirikiana katika kila jambo ili kuimarisha mshikamano. “Ni vizuri kwa Watanzania wa dini zote nchini kuondoa tofauti zao na kujenga umoja na mshikamano ili kudumisha amani. Tumeshuhudia matukio mbalimbali yanayohusishwa na masuala ya kidini kama; uchomaji moto wa makanisa yalitotokea Visiwani Zanzibar na Bara, umwagiaji wa tindikali kwa viongozi wa dini...”
Akizungumza kwa hisia, Mzee Mwinyi alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuwa wamoja licha ya kuwa kila mtu ana dini yake... “Ninaomba Waislamu na watu wa dini nyingine kuwa pamoja, tuondoe tofauti zetu kwani sisi Watanzania ni watu tuliozoeleka kwa kuwa na amani, nisingependa kuona dini zetu zinasababisha uvunjifu wa amani.”
“Mwenyezi Mungu hatukatazi, kushirikiana pamoja hivyo kwa hiyo tushirikiane, tupendane na tuimarishe umoja wetu ambao ndiyo sifa kubwa tuliyokuwa nayo kwa muda mrefu.”
Lindi
Akihutubia katika Maulid yaliyofanyika kimkoa kwenye Uwanja wa Ilulu Mjini Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Dk Nassor Hamid alisema ni wajibu wa jamii kutambua kuwa amani na utulivu wa nchi umetokana na umoja na mshikamano uliojengwa ambao hautakiwi kuchezewa na mtu, kikundi, taasisi wala vyama vya siasa.
Dk Hamid aliwataka viongozi wa dini zote kutoa elimu ya maadili kwa waumini wao ili kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa jamii.
Alisema kuna mambo mbalimbali yameanza kujitokeza katika jamii kama mavazi yasiyozingatia maadili ambayo si utamaduni wa Kitanzania na kwamba mambo hayo yanachangia ushawishi wa ngono zembe na kuongezeka kwa maambukizo ya Ukimwi.
“Ni wajibu wa kila mwananchi kuilinda amani na utulivu huo ili nchi yetu iendelee kutukuka kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu japo wapo baadhi ya watu wameanza kutaka kuharibu sifa hiyo.”
Songea
Sheikh wa Msikiti wa Wilaya ya Songea, Ruvuma, Abdallah Kitete amesema kuna kila sababu ya waumini na wanasiasa kuhubiri amani kwani pasipo vitu hivyo hakuna utawala...”Huwezi kutawala watu sehemu ambayo haina amani....”
Aliitaka jamii ijitahidi kuiga mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW), alivyoishi na watu wa dini zote bila kuwabagua huku akiwa mstari wa mbele kuhubiri upendo, amani na mshikamano na ndiyo maana dini yake ilienea dunia nzima.
Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa amesema wazazi wengi wa mkoa huo hawawakemei vijana wao wanaojiingiza katika biashara ya dawa za kulevya kwa kudhani ndiyo njia ya mkato ya kujitajirisha.
Akizungumza katika Maulid yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Tangamano, Gallawa alisema kuna taarifa kwamba idadi kubwa ya vijana wanaokamatwa na wengine kufungwa katika magereza ya ndani na nje ya nchi wengi wao wanatoka Mkoa wa Tanga na majina yao yanaonyesha kuwa ni Waislamu.
Alisema hiyo inatokana na vijana wengi wa mkoa huo kutokupenda kufanya kazi za uzalishaji mali badala yake kutafuta njia za mkato za kujitajirisha.
Zanzibar
Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Kaabi amewataka Waislamu kuimarisha amani, umoja na mshikamano kwa manufaa ya maendeleo ya visiwa hivyo na wananchi wake.
Sheikh Kaabi alisema Uislamu unasisitiza watu kupendana, kuishi kama ndugu na kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa kama alivyoonyesha kwa mfano Mtume Muhammad (SAW), katika uhai wake.
Katika Maulid hayo yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo; Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilali, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Sheikh Kaabi aliwataka Waislamu kutumia siku hiyo kukumbuka mazuri aliyoyafanya Mtume Muhammad (SAW) na kuishi kama ndugu wamoja na kujiepusha na mifarakano isiyokuwa na manufaa.
Imeandikwa na; Anthony Kayanda (Kigoma), Aidan Mhando (Dar), Burhani Yakub (Tanga), Mwanja Ibadi (Lindi) na Mwinyi Sadallah (Zanzibar). Chanzo -MWANANCHI

No comments:

Post a Comment