MAGAZETINI : WAZIRI MKUU AENDA KITETO KUTAFUTA SULUHU YA MAPIGANO KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Wednesday, 15 January 2014

MAGAZETINI : WAZIRI MKUU AENDA KITETO KUTAFUTA SULUHU YA MAPIGANO KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda / Picha na Maktaba






Dodoma/Arusha. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo anakwenda Wilaya ya Kiteto, Arusha kutafuta suluhu ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika Hifadhi ya Embroi Murtangosi yaliyosababisha vifo vya watu 10.

Mwandishi wa Habari wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Irene Bwire alisema jana: “Ni kweli Waziri Mkuu atakwenda kutembelea wilayani Kiteto ili kuongoza juhudi za kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.”

Polisi waanzisha msako

Maofisa wa Polisi kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo wanaongoza operesheni ya kuwasaka wahusika wa mapigano hayo kwa kutumia helikopta.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa alisema msako huo unaongozwa na Kamishna wa Operesheni wa Polisi, Simon Sirro... “Operesheni inaendelea porini lakini hadi sasa hatujakamata mtu. Mapigano yanayoendelea Kiteto ni ya kuviziana.”

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbulla amezitaka pande zote kuacha vita na kuwataka waliovamia ardhi ya Kiteto kuondoka kwa hiari.

Chadema waibana Serikali

Waziri Kivuli wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kumaliza mgogoro huo.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Kamili alisema licha ya Bunge kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza migogoro ya wakulima na wafugaji nchi nzima, hali bado ni tete katika eneo hilo.

Alisema Serikali inatakiwa kujitafakari juu ya uwezo wake wa kushughulikia matatizo ya haraka, badala ya kuwa mabingwa wa kushughulika na matokeo ya tatizo.

Mgogoro

Mgogoro huo ulioanza mwaka 2006, unatokana na wafugaji na wakulima kugombea ardhi kwenye eneo la Hifadhi ya Embroi Murtangosi.
Mapigano kati ya pande hizo mbili yamesababisha watu wanaokadiriwa kufikia 30 kuuawa.
Hifadhi hiyo yenye hekta 135,000, ina vyanzo vingi ya maji na madini ya aina ya chumvi, haitakiwi kuguswa kwa shughuli za kilimo wala ufugaji.
Wafugaji wanashinikiza utekelezaji wa amri ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, ambayo mwaka 2009 iliwaamuru wakulima kuondoka katika eneo hilo.
Mwaka 2006, wakulima waliishtaki Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto katika Mahakama ya Wilaya na kushinda kesi.
Halmashauri ilikata rufaa Mahakama Kuu lakini wakulima waliibuka washindi tena. Ilikata rufaa Mahakama ya Rufani ambako ilishinda na wakulima walitakiwa kuondoka. Chanzo MWANANCHI

No comments:

Post a Comment