Na Halima Mlacha - Habari Leo
HATUA iliyochukuliwa na Chadema dhidi ya
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe na Mjumbe wa zamani wa
Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo, haitofautiani na waliyochukuliwa Katibu
Mkuu wa zamani, Dk Aman Kabourou na Makamu Mwenyekiti wa zamani, Chacha
Wangwe.
Hayo yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu
wa chama hicho, Tundu Lissu, wakati akijibu hoja zilizotolewa juzi na
viongozi waliovuliwa madaraka kwa madai ya kukichafua chama na kufanya
uhaini.
Lissu alikanusha madai ya Zitto kwamba
alichukuliwa hatua kutokana na msimamo wake kuhusu kutochukua posho za
vikao na suala la ukaguzi wa ruzuku za vyama vya siasa, akisema kiini ni
waraka wa siri waliouandaa dhidi ya uongozi wa juu wa Chadema.
“Nasisitiza kuwa hawa wamechukuliwa
hatua kwa sababu za kukiuka maadili ya chama na mashitaka yote 11
yanayowakabili kila mmoja, yametokana na yaliyomo kwenye waraka wa siri
waliouandaa na si suala la posho wala PAC,” alisisitiza Lissu.
Alisema hatua zilizochukuliwa na Kamati
Kuu (CC) ya chama hicho dhidi yao ni halali na si mara ya kwanza kwa
viongozi wa chama hicho kuvuliwa madaraka kwa kuwa ilifanyika dhidi ya
Kabourou mwaka 2004 na Wangwe mwaka 2007.
“Na kwa nyaraka nilizosoma, Zitto
alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu wakati Kabourou na Wangwe walipovuliwa
nyadhifa zao, sasa kama Kamati Kuu mwaka 2004 na 2007 ilikuwa sahihi kwa
nini mwaka 2013 isiwe sahihi? Hawana hoja katika hili,” alisisitiza
Lissu.
Kabourou hivi sasa yuko CCM. Kuhusu hali
ya chama hicho kutokana na mgogoro huo, Lissu alifafanua kuwa Chadema
imestahimili mambo mengi makubwa yakiwamo ya Wangwe na Zitto na siku
zote imekuwa ikiendelea.
Kuhusu mkakati ulioandaliwa alisema ni
wa makusudi kwa kuwa chama kilishatangaza mwaka jana Mwongozo kwa
wanachama wanaotaka kugombea uongozi yakiwamo masharti ya wahusika kuwa
wazi na kutotumia fursa hiyo kukashifiana “kama waraka huo wa siri
uliomkashifu Mwenyekiti Freeman Mbowe.
“Waraka huu umetoa matusi mazito dhidi
ya Mwenyekiti wetu, ikiwamo kuitwa kuwa ana elimu ya chini na ana akili
ndogo na nzito, halafu mtu huyo huyo aliyetoa matusi hayo dhidi ya
kiongozi wake wa chama anadai eti anakiheshimu chama, kwa hili
tumewashitukia,” alisema.
Kuhusu suala la ruzuku, Lissu
alibainisha kuwa chama hicho kimefuata taratibu zote kama vyama vingine
za kukaguliwa, isipokuwa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), iliyolazimisha vyama vya siasa kujikagua kwa fedha zao,
wakati kazi hiyo ni yake kwa mujibu wa sheria.
Alisema wakati Zitto akianzisha hoja ya
ukaguzi wa hesabu za vyama na kuvishutumu kuwa havijakaguliwa, Msajili
wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi alishamwandikia barua CAG ya kumtaka
kufanya kazi yake ya ukaguzi kwa mujibu wa sheria.
“Sasa kinachoshangaza hayo anayosema
tayari sisi tulishayafanyia kazi na nyaraka zipo, tatizo lake hakanyagi
hapa ofisini haya atayajuaje? Lakini pia kuhusu kujiondoa kwenye saini
ya kuchukua fedha, hilo nalo si kweli, kwani hakuwahi kuwa mmoja wa
wanaosaini sasa atajiondoaje?” Alihoji.
Alisema alichofanya Zitto kuhusu suala
la hesabu za Serikali ni kutumia fursa ya PAC kuchafua chama. Siku 14
Mapema, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika,
alisema hatma ya viongozi hao waliovuliwa madaraka itajulikana baada ya
siku 14, watakapowasilisha utetezi wao kwa chama hicho.
Hali hiyo inatokana na uamuzi wa
Sekretarieti ya chama hicho iliyokutana juzi, kubariki uamuzi wa CC ya
chama hicho kuwavua nafasi zote za uongozi mbunge huyo na mwenzake, kwa
kuwaandikia rasmi barua ya mashitaka yenye makosa 11 kwa kila mmoja.
Sekretarieti hiyo, ilipitia uamuzi huo
na kuridhia barua hizo za mashitaka na kutoa siku 14 kwa watuhumiwa
kujitetea kwa maandishi. Mnyika alisema pamoja na barua hizo ambazo
wanatarajiwa kukabidhiwa leo, pia watuhumiwa hao watapewa fursa ya
kujitetea mbele ya CC.
“Sekretarieti imejiridhisha kuwa
watuhumiwa hawa wawili wanastahili kujibu makosa yanayowakabili na
kueleza ni kwa nini wasichukuliwe hatua za ziada ikiwamo kuvuliwa
uanachama,” alisema Mnyika.
Mnyika alisisitiza kuwa mashitaka
yanayowakabili Zitto na mwenzake, yamejikita zaidi kwenye waraka na si
ambayo walizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari siku mbili
zilizopita.
Aidha, alitetea uamuzi wa CC ya chama
hicho wa kuwachukulia hatua Zitto na Dk Kitilla kuwa ulifuata taratibu
na kanuni zote za chama hicho na ulikuwa wa haki. Alisema kwa mujibu wa
kanuni za chama hicho ibara ya 5.4 CC bila kuathiri Katiba, inaweza
kumvua wakati mwanachama, nafasi ya uongozi pale atakapothibitika kwenda
kinyume na taratibu za chama.
Aidha, alisema Ibara ya 6.36 ambayo
inaainisha mamlaka ya uwajibishwaji, inabainisha kuwa viongozi
waliochaguliwa na Mkutano Mkuu wanaweza kuvuliwa madaraka yao na mkutano
huo, lakini waliochaguliwa na Baraza Kuu kama Zitto na Dk Kitilla, CC
inaweza kuwavua wakibainika kwenda kinyume.
“Hii kanuni ya 6.52 iliyotumiwa na
mwanasheria wao, Albert Msando, inayosema kuwa mwanachama haruhusiwi
kuchukuliwa hatua hadi atakapoandikiwa barua ya mashitaka kujitetea,
ilishafanyiwa marekebisho siku nyingi na kuongezwa kifungu ‘d’
kinachobainisha kuwa CC itachukua uamuzi itakapoona inafaa,”
alisisitiza.
Mnyika alihadharisha juu ya waraka
uliosambazwa na kutumika kwenye vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii, kuwa umeghushiwa na kuhaririwa na kwamba waraka halisi chama
hicho kinao na una madai na mikakati mizito dhidi ya chama hicho, hasa
viongozi wake wakuu.
Katika hatua nyingine, Lissu alidai kuwa
mkutano wa Zitto na Dk Kitilla wa waandishi wa habari haukujibu hoja
yoyote zaidi ya kupindisha lengo na ukweli.
Alisema viongozi hao hawakuvuliwa
madaraka yao kutokana na sababu walizoainisha bali walichukuliwa hatua
hiyo, kutokana na ushiriki wao katika mpango wa kufanya mapinduzi ya
uongozi ndani ya chama, jambo aliloliita ni kinyume na Katiba, taratibu
na itifaki ya chama.
Uchaguzi Juni Wakati huo huo, Mkurugenzi
wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila alizungumzia
ratiba ya uchaguzi wa kitaifa ndani ya chama ambao utafanyika kwa siku
nane kuanzia Juni 26 hadi 30 mwakani huku wa ngazi ya vitongoji
ukifanyika Desemba 15 hadi Januari 15, mwakani. Chanzo: Habari Leo, Gwiji la Habari Tz
No comments:
Post a Comment