Kilimo : Nicomed Bohay Aandika Historia, Ateuliwa Kuongoza EFAFRICA Group Barani Afrika - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Monday, 14 September 2026

Kilimo : Nicomed Bohay Aandika Historia, Ateuliwa Kuongoza EFAFRICA Group Barani Afrika

 

Na Mwandishi wetu.


Katika habari njema kwa Tanzania na sekta ya fedha barani Afrika, Nicomed Bohay ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa EFAfrica Group Ltd (Group CEO), kampuni ya Pan-Afrika inayojihusisha na ufadhili wa mashine na vifaa vya uzalishaji kwa wakulima, viwanda, biashara, ujenzi na usafirishaji.


Uteuzi huo unamfanya Bohay kuwa Mtanzania anayeongoza taasisi yenye shughuli zake nchini Tanzania, Kenya, Zambia na Mauritius, huku akipewa jukumu la kuongoza mkakati wa kupanua huduma za leasing na kuongeza upatikanaji wa mashine za uzalishaji kwa maelfu ya wafanyabiashara na wakulima barani Afrika.


Akizungumza kuhusu uteuzi huo, Mwenyekiti Mtendaji wa EFAfrica Group, Dk. Michiel Timmerman, alisema Bohay ameonyesha uwezo mkubwa wa uongozi, nidhamu katika usimamizi wa taasisi na dhamira ya kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.


> “Nicomed ameonyesha uongozi wa kipekee, nidhamu katika usimamizi na dhamira ya kweli ya kuimarisha ujumuishi wa kifedha kupitia ufadhili wa vifaa vya uzalishaji. Tuna imani kuwa ataiongoza EFAfrica kufikia hatua mpya ya ukuaji na athari kubwa zaidi kwa wakulima na biashara za Afrika,” alisema Dk. Timmerman.


Bohay ni mtaalamu wa fedha za maendeleo mwenye uzoefu wa karibu miaka 30 katika sekta ya benki, biashara za kilimo na maendeleo ya ujasiriamali. Kabla ya kujiunga na EFAfrica mwaka 2021, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust Tanzania, ambako aliongoza programu mbalimbali za kuwawezesha wajasiriamali wa kilimo na kusaidia kuanzishwa kwa Agribusiness Innovation Centre.


Pia aliwahi kuongoza Idara ya Biashara za Kilimo katika Benki ya CRDB, akichangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima na biashara zinazohusiana na kilimo nchini Tanzania.


Mwaka 2021, Bohay aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Equity for Tanzania Limited (EFTA). Ndani ya kipindi chake cha uongozi, kampuni ilipanua huduma zake kwa kiwango kikubwa na kujiimarisha kama taasisi inayoongoza nchini katika ufadhili wa mashine za uzalishaji kupitia mfumo wa leasing.


Mbali na ukuaji wa biashara, EFTA iliendelea kuwa na ubora wa hali ya juu wa mikopo, ambapo taarifa za fedha za Juni 2026 zilionyesha kiwango cha mikopo chechefu cha asilimia 1 pekee.


Moja ya mafanikio makubwa ya Bohay ni kusimamia ufadhili wa zaidi ya mashine 4,000 za kilimo nchini Tanzania. Mashine hizo zinajumuisha matrekta, power tillers, combine harvesters, mifumo ya umwagiliaji na vifaa vingine vilivyosaidia kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za kilimo na kuimarisha usalama wa chakula.


Lakini mafanikio hayo hayakuishia mashambani. Kupitia mfumo wa leasing, EFTA imewezesha maelfu ya biashara kupata malori, mabasi, mashine za viwandani, vifaa vya ujenzi na mitambo ya uchakataji, hatua iliyochochea ukuaji wa biashara na kuongeza ajira katika sekta mbalimbali za uchumi.


Katika kuendeleza ujumuishi wa kiuchumi, Bohay pia alisimamia kuanzishwa kwa Mpango wa Ukodishaji wa Vifaranga na Chakula cha Kuku, uliolenga wanawake na vijana.


Kupitia programu hiyo, wanufaika hupata vifaranga vya siku moja, chakula na pembejeo muhimu kwa mfumo wa leasing bila kuhitaji mtaji mkubwa wa kuanzisha biashara, hivyo kuwapa fursa ya kujiajiri na kuongeza kipato.


Akizungumza baada ya uteuzi wake, Bohay alisema lengo lake ni kuhakikisha upatikanaji wa mashine za uzalishaji hauwi tena kikwazo kwa maendeleo ya Waafrika.


> “Tunataka EFAfrica iwe mshirika wa kwanza wa wakulima na wafanyabiashara katika safari yao ya ukuaji. Tukiwapa watu vifaa vya kuzalisha, tunawapa uwezo wa kubadilisha maisha yao, kuunda ajira na kuchochea uchumi wa Afrika,” alisema Bohay.


Uteuzi wa Nicomed Bohay unaendelea kuipa Tanzania heshima katika sekta ya fedha na maendeleo, huku ukitoa ujumbe kwamba wataalamu wa Kitanzania wanaweza kuongoza taasisi kubwa za Pan-Afrika na kuchangia moja kwa moja katika mageuzi ya uchumi wa bara.

No comments:

Post a Comment