Matukio : TFFT Yatoa Tuzo kwa Vituo Bora vya Makao ya Watoto - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


22 Nov 2015

Matukio : TFFT Yatoa Tuzo kwa Vituo Bora vya Makao ya Watoto


Picha ya pamoja ya Wamiliki wa vituo vya makao ya watoto wakiwa na  tuzo zao  za makao bora ya watoto.Picha na Ferdinand Shayo
Na Ferdinand Shayo wa Wazalendo 25 Blog ,Arusha.


Shirika la The Foundation For Tomorrow lenye makao yake jijini Arusha,  limevitunuku tuzo vituo bora vya makao ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi katika mkoa wa Arusha. Tuzo hizo zenye lengo la kutambua juhudi na mchango wa makao ya watoto katika kujenga jamii bora, kulinda na kuhakikisha usalama kwa watoto zilikabidhiwa kwa washiriki na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Arusha Bi. Blandina Nkini kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha.



Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, iliyofanyika katika ofisi ya shirika hilo jijini Arusha, Bi. Nkini alisema kuwa uangalizi wa watoto ni  muhimu sana katika ustawi wa taifa kwa kuwa ndio unaojenga msingi wa taifa kwa kuwapa watoto malezi bora. "Viongozi wa taifa letu hutokana na malezi na makuzi bora waliyoyapata utotoni", alisema.



Naye mkurugenzi mkazi wa shirika hilo ndugu, Kennedy Oulu aliwahimiza washiriki wa tuzo hizo kuendelea kuunganisha juhudi zao katika kushughulikia changamoto ziwapatazo watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.



"Inahitaji huruma, upendo na msukumo wa kweli katika kuwasaidia watoto hawa. Licha ya kuwa tatizo la watoto waishio katika mazingira magumu na hatarishi ni kubwa na ni vigumu kutokomeza, muunganiko wa juhudi za kila mmoja wetu litawezesha kuweka mchango mkubwa katika kupunguza tatizo lililopo", alisema Oulu.



Aidha Oulu aliongeza kuwa, haki za watoto katika nchi yetu zinakiukwa sana, si kwa watoto waishio katika mazingira hatarishi tu, bali hata kwa wale wasio katika mazingira hayo. Aliongeza kuwa, tafiti zinaonesha kwamba kuna ukiukwaji mkubwa zaidi kwa watoto waishio kwenye makao ya watoto kuliko walio majumbani na sehemu zingine. Hili linatokana na dhamira na malengo tofauti ya wale wanaoanzisha na kuendesha makao hayo.



"Haki za watoto zinakiukwa kwa sababu wanajamii kwa kiasi kikubwa hawatambui kuwa watoto pia wana haki zao! Sheria za watoto (LCA 2009) zimeweka wazi haki za mtoto na matokeo ya ukiukwaji wake. Sisi tunaowalea watoto na jamii kwa ujumla hatuna budi kuzitambua, kuzifuata na kuhakikisha utekelezaji wa haki za watoto". Alisema Oulu.



Vituo vya makao ya watoto vipatavyo 12 kutoka wilaya za Meru, Monduli na Karatu vilishiriki katika mchakato  wa tuzo hizo kwa mwaka huu, ambapo kituo cha SMALL STEPS FOR COMPASSION (www.smallstepsforcompassion.org)  kilichopo Usa River wilaya ya Meru ndicho kilichoibuka mshindi wa jumla kimkoa, huku kituo cha RIFT VALLEY CHILDREN FUND (www.tanzanianchildrensfund.org) kikishinda tuzo ya mshindi wa wilaya ya Karatu na MAJENGO CHILDREN'S HOME chenye makao yake katika mji wa Mto wa Mbu kikiwa mshindi wa wilaya ya Monduli.



Akiongea wakati wa kuhitimisha hafla ya kukabidhi tuzo hizo, Bi. Nkini alilipongeza shirika la The Foundation For Tomorrow kwa kutoa tuzo hizo ambazo mchakato wake huwezesha vituo vingi kuboresha huduma zao kwa watoto. Aidha alimsihi mkurugenzi wake ndugu Oulu kuwa aangalie pia uwezekano wa kutoa elimu ya malezi bora ya watoto kwa vituo vyote vilivyopo Arusha kadri inavyowezekana kwani elimu hii ni muhimu sana kuweza kufikiwa kwa vituo vyote. Aidha aliviasa vituo hivi kujisahihisha pale kunapo mapungufu na kuboresha huduma zao kwa watoto. Naye mkurugenzi wa shirika hilo, ndugu Oulu alimhakikishia Bi. Nkini kuwa shirika hilo lipo tayari kutoa elimu hii kwa vituo vilivyopo Arusha wakati wowote litakapoalikwa iwapo ofisi ya Ustawi wa Jamii mkoa wa Arusha ikiandaa mafunzo ya namna hii.



Tuzo hizi zimepangwa kutolewa kila mwaka na kushirikisha mikoa mingine zaidi kwa ushirikiano wa shirika la The Foundation For Tomorrow, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kupitia Ofisi za Ustawi wa Jamii Wilaya, Vituo vya Makao ya Watoto na jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad