Picha ya pamoja ya Wamiliki wa vituo vya makao ya watoto wakiwa na tuzo zao za makao bora ya watoto.Picha na Ferdinand Shayo
Na
Ferdinand Shayo wa Wazalendo 25 Blog ,Arusha.
Shirika la The Foundation For
Tomorrow lenye makao yake jijini Arusha,
limevitunuku tuzo vituo bora vya makao ya watoto wanaoishi katika
mazingira magumu na hatarishi katika mkoa wa Arusha. Tuzo hizo zenye lengo la
kutambua juhudi na mchango wa makao ya watoto katika kujenga jamii bora,
kulinda na kuhakikisha usalama kwa watoto zilikabidhiwa kwa washiriki na Afisa
Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Arusha Bi. Blandina Nkini kwa niaba ya mkuu wa
mkoa wa Arusha.
Akizungumza katika hafla ya utoaji
wa tuzo hizo, iliyofanyika katika ofisi ya shirika hilo jijini Arusha, Bi.
Nkini alisema kuwa uangalizi wa watoto ni
muhimu sana katika ustawi wa taifa kwa kuwa ndio unaojenga msingi wa
taifa kwa kuwapa watoto malezi bora. "Viongozi wa taifa letu hutokana na
malezi na makuzi bora waliyoyapata utotoni", alisema.
Naye mkurugenzi mkazi wa shirika
hilo ndugu, Kennedy Oulu aliwahimiza washiriki wa tuzo hizo kuendelea
kuunganisha juhudi zao katika kushughulikia changamoto ziwapatazo watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi.
"Inahitaji huruma, upendo na
msukumo wa kweli katika kuwasaidia watoto hawa. Licha ya kuwa tatizo la watoto
waishio katika mazingira magumu na hatarishi ni kubwa na ni vigumu kutokomeza,
muunganiko wa juhudi za kila mmoja wetu litawezesha kuweka mchango mkubwa
katika kupunguza tatizo lililopo", alisema Oulu.
Aidha Oulu aliongeza kuwa, haki za
watoto katika nchi yetu zinakiukwa sana, si kwa watoto waishio katika mazingira
hatarishi tu, bali hata kwa wale wasio katika mazingira hayo. Aliongeza kuwa,
tafiti zinaonesha kwamba kuna ukiukwaji mkubwa zaidi kwa watoto waishio kwenye
makao ya watoto kuliko walio majumbani na sehemu zingine. Hili linatokana na
dhamira na malengo tofauti ya wale wanaoanzisha na kuendesha makao hayo.
"Haki za watoto zinakiukwa kwa
sababu wanajamii kwa kiasi kikubwa hawatambui kuwa watoto pia wana haki zao!
Sheria za watoto (LCA 2009) zimeweka wazi haki za mtoto na matokeo ya ukiukwaji
wake. Sisi tunaowalea watoto na jamii kwa ujumla hatuna budi kuzitambua,
kuzifuata na kuhakikisha utekelezaji wa haki za watoto". Alisema Oulu.
Vituo vya makao ya watoto vipatavyo
12 kutoka wilaya za Meru, Monduli na Karatu vilishiriki katika mchakato wa tuzo hizo kwa mwaka huu, ambapo kituo cha
SMALL STEPS FOR COMPASSION (www.smallstepsforcompassion. org) kilichopo Usa River wilaya ya Meru ndicho
kilichoibuka mshindi wa jumla kimkoa, huku kituo cha RIFT VALLEY CHILDREN FUND
(www.tanzanianchildrensfund. org) kikishinda tuzo ya mshindi wa wilaya ya Karatu
na MAJENGO CHILDREN'S HOME chenye makao yake katika mji wa Mto wa Mbu kikiwa
mshindi wa wilaya ya Monduli.
Akiongea wakati wa kuhitimisha
hafla ya kukabidhi tuzo hizo, Bi. Nkini alilipongeza shirika la The Foundation
For Tomorrow kwa kutoa tuzo hizo ambazo mchakato wake huwezesha vituo vingi
kuboresha huduma zao kwa watoto. Aidha alimsihi mkurugenzi wake ndugu Oulu kuwa
aangalie pia uwezekano wa kutoa elimu ya malezi bora ya watoto kwa vituo vyote
vilivyopo Arusha kadri inavyowezekana kwani elimu hii ni muhimu sana kuweza
kufikiwa kwa vituo vyote. Aidha aliviasa vituo hivi kujisahihisha pale kunapo
mapungufu na kuboresha huduma zao kwa watoto. Naye mkurugenzi wa shirika hilo,
ndugu Oulu alimhakikishia Bi. Nkini kuwa shirika hilo lipo tayari kutoa elimu
hii kwa vituo vilivyopo Arusha wakati wowote litakapoalikwa iwapo ofisi ya
Ustawi wa Jamii mkoa wa Arusha ikiandaa mafunzo ya namna hii.
Tuzo hizi zimepangwa kutolewa kila
mwaka na kushirikisha mikoa mingine zaidi kwa ushirikiano wa shirika la The
Foundation For Tomorrow, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kupitia Ofisi za
Ustawi wa Jamii Wilaya, Vituo vya Makao ya Watoto na jamii kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment