MICHEZO, RIADHA :KAMPUNI YA IPTL YATOA TSH MILIONI 20 KWA RT KUSAIDIA MAANDALIZI YA MASHINDANO YA RIADHA YA KITAIFA - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


12 Jul 2014

MICHEZO, RIADHA :KAMPUNI YA IPTL YATOA TSH MILIONI 20 KWA RT KUSAIDIA MAANDALIZI YA MASHINDANO YA RIADHA YA KITAIFA

 Makamu wa Rais-Utawala wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) William Kallaghe (wapili kushoto) akipokea sehemu ya fedha taslim Tsh milioni 20 zilizotolewa na kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kusaidia maandalizi ya mashindano ya mwaka huu ya Riadha ya Kitaifa yatakayoanza leo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaaam. Kulia ni Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/ Pan African Power Solutions (PAP), Bw. Joseph Makandege, akifuatiwa na Msaidizi wa kampuni hiyo Rajiv Bhesania na kushoto ni Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui.
 Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui (wapili kushoto) akipokea sehemu ya fedha taslim Tsh milioni 20 zilizotolewa na kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kusaidia maandalizi ya mashindano ya mwaka huu ya Riadha ya Kitaifa yatakayoanza leo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaaam. Kulia ni Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/ Pan African Power Solutions (PAP), Bw. Joseph Makandege, akifuatiwa na Msaidizi wa kampuni hiyo Rajiv Bhesania na kushoto ni Makamu wa Raisi-Utawala wa RT, William Kallaghe.
==============  ==========  ===========
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) limepokea shilingi milioni 20 kutoka katika kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL) kwa lengo la kusaidia uandaaji wa mashindano ya Riadha ya Kitaifa yanayoanza leo jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui aliwaeleza waandishi wa habari kuwa fedha hizo zilipokelewa zitasaidia katika maandalizi ya mbio hizo kubwa za kitaifa ambazo zitatumika katika kuwaandaa wanariadha watakaoiwakilisha nchi katika mashindano mbali mbali ya kimataifa.

Bw. Nyambui alisema kuwa zaidi ya wanariadha 400 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo zitakazofanyika kwa siku mbili na zaidi ya waamuzi 200 watakuwa tayari kuhakikisha wanaofanya vizuri wanachaguliwa na kupewa mafunzo zaidi kwa ajili ya mashindano ya baadae.

Alibainisha kuwa ufadhili wa kampuni ya IPTL utasaidia kwa kiasi kikubwa kulipia gharama za maandalizi na uendshaji wa tukio hilo, na hivyo kuisaidia RT kufikia malengo yake katika mashindano ya mwaka huu ya kitaifa. 

"Mashindano ya mwaka huu ya riadha ya kitaifa yanaanza kesho (leo jumamosi) katika uwanja wa taifa wa Dar es Salaam, ambapo mikoa yote 30 nchini Tanzania inatarajiwa kushiriki.

"Tunategemea wanariadha wetu wa taifa kuonyesha uwezo wao kabla hawajasafiri kwenda Scotland kwa ajili ya mashindani ya Jumuiya ya Madola yaliyopangwa kufanyika mwezi wa Julai tarehe 23 mpaka Agosti tarehe 3,"alisema Nyambui.

Licha ya mashindano hayo ya kitaifa kutumiwa na RT  kama nafasi  ya kupasha misuli moto kwa wanariadha watakaoiwakilisha nchi kwa mashindano yajayo ya jumuiya ya madola, mashindano hayo yatawapatia wanariadha wanaochipukia nafasi ya kuonyesha ujuzi wao.

Aliongeza kuwa mbio hizo zitatumika katika kuchagua timu ya kitaifa ya wanariadha watakaoiwakilisha nchi katika mashindano mbali mbali ya kimataifa kama vile ya Ukanda wa Tano, Mashindano ya Dunia na Afrika yatakayofanyika baadae mwaka huu.

Kwa upande wake, Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/ Pan African Power Solutions (PAP), Bw. Joseph Makandege alisema kuwa kampuni yake imekubali kudhamini mashindano hayo kama njia ya kuipa RT nafasi ya kutambua vipaji vipya na pia kuwaandaa wanariadha wa kitanzania kwa ajili ya mashindano ya kimataifa. 

"Riadha ni eneo mojawapo ambalo Tanzania inaweza kulitumia ili kujiweka katika ramani ya dunia ya michezo. Miaka iliyopita, wanariadha wetu walililetea heshima kubwa taifa hili. IPTL inaamini kuwa  bado kuna vipaji vingi vinavyoweza kuchukuliwa na kutumika katika kuipeperusha vyema  bendera yetu ya taifa katika mashindano mbali mbali ya kimataifa.

"Udhamini wetu pia unalenga katika kuwatengenezea nafasi za ajira vijana wa kitanzania. Tunajua kuwa vijana wetu wengi wana vipaji, ambavyo vinapotea tu. Kama RT watasaidiwa kuviinua vipaji hivi, vijana wengi watajipatia chanzo cha mapato yao kupitia riadha. Hili linaendana na sera yetu ya kurudisha kile tukipatacho kwa jamii ambayo pia imejikita katika kuiwezesha jamii inayotuzunguka kiuchumi," alisema.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais- Utawala wa RT , William Kallaghe aliishukuru IPTL kwa msaada wake, huku akiongeza kuwa mashindano ya kitaifa ya riadha ya mwaka huu yatakuwa tofauti na yaliyopita,  kwa kuwa yatatumika kuiandaa timu ya taifa kwa ajili ya mashindano yajayo ya kimataifa ya mwakani au miaka miwili ijayo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad