Makamu wa Rais-Utawala wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) William Kallaghe (wapili
kushoto) akipokea sehemu ya fedha taslim Tsh milioni 20 zilizotolewa na kampuni
ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kusaidia maandalizi
ya mashindano ya mwaka huu ya Riadha ya Kitaifa yatakayoanza leo katika uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaaam. Kulia ni Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/
Pan African Power Solutions (PAP), Bw. Joseph Makandege, akifuatiwa na Msaidizi
wa kampuni hiyo Rajiv Bhesania na kushoto ni Katibu Mkuu wa RT, Suleiman
Nyambui.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui (wapili
kushoto) akipokea sehemu ya fedha taslim Tsh milioni 20 zilizotolewa na kampuni
ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kusaidia maandalizi
ya mashindano ya mwaka huu ya Riadha ya Kitaifa yatakayoanza leo katika uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaaam. Kulia ni Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/
Pan African Power Solutions (PAP), Bw. Joseph Makandege, akifuatiwa na Msaidizi
wa kampuni hiyo Rajiv Bhesania na kushoto ni Makamu wa Raisi-Utawala wa RT,
William Kallaghe.
============== ========== ===========
SHIRIKISHO la Riadha
Tanzania (RT) limepokea shilingi milioni 20 kutoka katika kampuni ya ufuaji
umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL) kwa lengo la kusaidia uandaaji wa mashindano
ya Riadha ya Kitaifa yanayoanza leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa RT,
Suleiman Nyambui aliwaeleza waandishi wa habari kuwa fedha hizo zilipokelewa
zitasaidia katika maandalizi ya mbio hizo kubwa za kitaifa ambazo zitatumika
katika kuwaandaa wanariadha watakaoiwakilisha nchi katika mashindano mbali
mbali ya kimataifa.
Bw. Nyambui alisema
kuwa zaidi ya wanariadha 400 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo
zitakazofanyika kwa siku mbili na zaidi ya waamuzi 200 watakuwa tayari
kuhakikisha wanaofanya vizuri wanachaguliwa na kupewa mafunzo zaidi kwa ajili
ya mashindano ya baadae.
Alibainisha kuwa
ufadhili wa kampuni ya IPTL utasaidia kwa kiasi kikubwa kulipia gharama za maandalizi
na uendshaji wa tukio hilo, na hivyo kuisaidia RT kufikia malengo yake katika mashindano
ya mwaka huu ya kitaifa.
"Mashindano ya
mwaka huu ya riadha ya kitaifa yanaanza kesho (leo jumamosi) katika uwanja wa
taifa wa Dar es Salaam, ambapo mikoa yote 30 nchini Tanzania inatarajiwa
kushiriki.
"Tunategemea
wanariadha wetu wa taifa kuonyesha uwezo wao kabla hawajasafiri kwenda Scotland
kwa ajili ya mashindani ya Jumuiya ya Madola yaliyopangwa kufanyika mwezi wa
Julai tarehe 23 mpaka Agosti tarehe 3,"alisema Nyambui.
Licha ya mashindano
hayo ya kitaifa kutumiwa na RT kama nafasi ya kupasha misuli moto kwa wanariadha
watakaoiwakilisha nchi kwa mashindano yajayo ya jumuiya ya madola, mashindano
hayo yatawapatia wanariadha wanaochipukia nafasi ya kuonyesha ujuzi wao.
Aliongeza kuwa mbio
hizo zitatumika katika kuchagua timu ya kitaifa ya wanariadha watakaoiwakilisha
nchi katika mashindano mbali mbali ya kimataifa kama vile ya Ukanda wa Tano, Mashindano
ya Dunia na Afrika yatakayofanyika baadae mwaka huu.
Kwa upande wake,
Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/ Pan African Power Solutions (PAP), Bw.
Joseph Makandege alisema kuwa kampuni yake imekubali kudhamini mashindano hayo kama
njia ya kuipa RT nafasi ya kutambua vipaji vipya na pia kuwaandaa wanariadha wa
kitanzania kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.
"Riadha ni eneo
mojawapo ambalo Tanzania inaweza kulitumia ili kujiweka katika ramani ya dunia
ya michezo. Miaka iliyopita, wanariadha wetu walililetea heshima kubwa taifa
hili. IPTL inaamini kuwa bado kuna vipaji vingi vinavyoweza kuchukuliwa
na kutumika katika kuipeperusha vyema bendera yetu ya taifa katika mashindano mbali
mbali ya kimataifa.
"Udhamini wetu
pia unalenga katika kuwatengenezea nafasi za ajira vijana wa kitanzania.
Tunajua kuwa vijana wetu wengi wana vipaji, ambavyo vinapotea tu. Kama RT
watasaidiwa kuviinua vipaji hivi, vijana wengi watajipatia chanzo cha mapato
yao kupitia riadha. Hili linaendana na sera yetu ya kurudisha kile tukipatacho
kwa jamii ambayo pia imejikita katika kuiwezesha jamii inayotuzunguka
kiuchumi," alisema.
Wakati huo huo, Makamu
wa Rais- Utawala wa RT , William Kallaghe aliishukuru IPTL kwa msaada wake,
huku akiongeza kuwa mashindano ya kitaifa ya riadha ya mwaka huu yatakuwa
tofauti na yaliyopita, kwa kuwa yatatumika kuiandaa timu ya taifa kwa
ajili ya mashindano yajayo ya kimataifa ya mwakani au miaka miwili ijayo.
No comments:
Post a Comment